The House of Favourite Newspapers

TFF yamfungia Kazi Ndayiragije

WAKATI Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likiendelea na mchakato wa kumtafuta kocha mkuu Taifa Stars kuna uwezekano mkubwa kocha mkuu wa muda wa timu hiyo, Mrundi, Etienne Ndayiragije akapewa mikoba hiyo moja kwa moja.

Ndayiragije licha ya kukinoa kikosi cha Stars na kufanikisha kukipeleka kushiriki hatua ya makundi ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia mwaka 2022 pia ndiye kocha mkuu wa Azam FC.

Kutokana na mafanikio hayo yakiwemo yale ya kuipeleka mbele Stars kwenye michuano ya Chan, uongozi wa TFF umeonekana kuvutiwa na kazi yake hivyo inadaiwa umepanga kumpa mazima nafasi hiyo iliyoachwa na Emmanuel Amunike raia wa Nigeria.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya TFF, ambazo Championi Jumamosi limezipata zinasema kuwa: “Kwa sasa uongozi wa TFF unatarajia kukutana na uongozi wa Azam ili kuzungumza nao na kuona ni jinsi gani ya kufanya ili Ndayiragije aweze kuchukua nafasi hiyo ya kuwa kocha mkuu wa Taifa Stars moja kwa moja.

“Kuna uwezakano mkubwa utaratibu ambao utatumika unaweza kuwa kama ule uliokuwa ukitumika nchini DR Congo, ambapo kocha mkuu wa timu yao ya taifa ndiye pia alikuwa Kocha Mkuu wa AS Vita na msaidizi wake alikuwa kocha wa TP Mazembe.

“Kwa hiyo Ndayiragije naye anaweza kuendelea na majukumu yake Azam lakini pia Taifa Stars na akawa na mikataba kutoka pande zote mbili,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Comments are closed.