TFF Yasubiri Rekodi za Simba, Yanga

UONGOZI wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), umeweka wazi kuwa maandalizi yote ya mchezo wa Ngao ya Jamii unaotarajiwa kuzikutanisha klabu za Simba na Yanga Jumamosi hii yamekamilika na wana matumaini makubwa kuwa mchezo huo utaandika rekodi mpya ya ubora wa maandalizi yake.

Simba na Yanga, zinatarajiwa kukutana Jumamosi hii katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam, ambapo kikanuni mchezo huu ndiyo huashiria ufunguzi rasmi wa msimu mpya wa ligi.

Tayari ratiba ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara imetoka ambapo inaonyesha michezo ya kwanza inatarajiwa kuanza kuchezwa Septemba 27, mwaka huu.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Mkuu wa Idara ya Ligi, Jonathan Kassano alisema: “Kila kitu kuhusiana na maandalizi ya mchezo wa Ngao ya Jamii ambao unaotarajiwa kuzikutanisha klabu za Simba na Yanga utakaopigwa kwenye Uwanja wa Mkapa kimekamilika na kinachosubiriwa ni Jumamosi ifike utekelezaji wa mchezo huo.

“Kutokana na maandalizi ambayo tumeyafanya mpaka sasa tunaamini mchezo wa mwaka huu utaweka rekodi ambayo haikuwahi kushuhudiwa katika maandalizi ya mchezo huu kwa miaka iliyopita.”

MARCO MZUMBE, Dar es Salaam


Toa comment