The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness

0

Kutokana na kipigo hicho, Arianna alidondoka chini huku damu nyingi zikimtoka puani na mdomoni, Diego akatoka na kurudi chumbani kwake, akamuacha Arianna akiugulia maumivu makali.

“Dada Arianna! Dada Arianna! Chai tayari, bosi ame…” mhudumu wa nyumba hiyo ya bilionea Msuya alipigwa na butwaa baada ya kusukuma mlango wa chumba alichokuwa analala Arianna kwa ajili ya kwenda kumtaarifu kwamba kifungua kinywa kilikuwa tayari kama walivyoelekezwa na bosi wao kuhakikisha anakula chakula kamili.

“Mungu wangu, nini kimetokea? Alisema kwa mshtuko huku akiwa haamini alichokuwa anakiona. Arianna alikuwa amelala sakafuni huku damu nyingi zikimtoka puani na mdomoni.

“Dada! Dada, umepatwa na nini,” alisema msichana huyo kwa sauti kubwa iliyomshtua mwenzake aliyekuwa akifanya usafi, naye akaacha kila alichokuwa anakifanya na kukimbilia kule mwenzake alikokuwa anafanya usafi.

Kelele hizo zilitua kwenye masikio ya Diego ambaye naye alijifanya hajui chochote, akatoka chumbani kwake na kuelekea kule kelele hizo zilikokuwa zinasikika.
“Kumetokea nini tena?” Diego alijifanya kuuliza, wale wafanyakazi wa Msuya wakaanza kumueleza ilivyokuwa.

“Nilikuwa nimekuja kumuamsha kwa ajili ya kupata kifungua kinywa ndiyo nikamkuta kwenye hali hii.”

“Mungu wangu, Arianna! Arianna!” Diego alipiga magoti pale pembeni ya msichana huyo na kuanza kumtingisha, akijifanya hajui kabisa kilichomtokea.
“Inabidi tumpigie bosi simu aje,” alisema mfanyakazi mmoja, Diego akaingilia kati na kueleza kuwa hakukuwa na ulazima wa kufanya hivyo labda mpaka hali itakapozidi kuwa mbaya.

“Kanileteeni kisanduku cha huduma ya kwanza,” alisema Diego huku akimlaza Arianna vizuri pale chini alipokuwa ameangukia.

“Arianna! Arianna! Unanisikia… naomba ujikaze,” alisema Diego kwa sauti ya chini, muda mfupi baadaye yule mfanyakazi mwingine alileta kisanduku cha huduma ya kwanza na bila kupoteza muda, Diego akaanza kumtibu Arianna.

Alianza kwa kumsafisha damu zilizokuwa zinaendelea kutoka, kwa bahati nzuri Arianna hakuwa amepata jeraha lolote kubwa la nje, akaendelea kumsafisha kisha akamuwekea puani dawa maalum ya kuvuta, Ammonia Inhalants ambayo hutumika kuwarejeshea fahamu watu waliozimia.

Alipovuta dawa hiyo tu, Arianna alipiga chafya mfululizo kisha akazinduka na kujikuta yuko kwenye mikono ya Diego ambaye alimkazia macho kama anayemwambia ‘usimwambie mtu yeyote kilichotokea’.
“Vipi unajisikiaje Arianna?”

“Najisikia maumivu makali kichwani,” alijibu kwa tabu huku akilia kwa uchungu, ikabidi Diego awatoe kijanja wale wafanyakazi ili apate muda wa kuzungumza na Arianna. Hakutaka mtu yeyote ajue kwamba yeye ndiye aliyemfanyia ukatili huo Arianna.

“Nakuomba unisamehe mpenzi wangu, mtu yeyote akikuuliza mwambie ulisikia kizunguzungu kisha ukadondoka, nakuomba sana unitunzie hii siri, sitarudia tena,” alisema Diego kwa sauti ya kubembeleza, Arianna akawa hana cha kujibu zaidi ya kuendelea kulia kwa uchungu.

“Maji ya moto yapo tayari,” alisema mfanyakazi mmoja aliyeagizwa na Diego, kisha kazi ya kumchua Arianna maeneo aliyokuwa anasikia maumivu ikaanza mara moja.
“Eti dada Arianna kwani ilikuwaje?”

“Nilikuwa najisikia kizunguzungu nikiwa bafuni ndiyo nikadondoka na kupoteza fahamu,” alisema Arianna kwa tabu huku akijua fika kwamba anadanganya. Hakutaka Diego aingie kwenye matatizo yoyote na kwa sababu hiyo, hakuona hatari kuendelea kumlinda japokuwa alikuwa amemsababishia matatizo makubwa.

“Nakushukuru sana Arianna, ni shetani tu alinipitia, niko chini ya miguu yako,” Diego aliendelea kumbembeleza huku akimchua taratibu kwenye maeneo aliyokuwa akilalamikia maumivu.

“Naomba uende chumbani kwako nahitaji kupumzika mwenyewe,” alisema Arianna baada ya kusaidiwa kulala kitandani kwake, bila kusema kitu Diego aliinuka na kutoka, akamuacha mfanyakazi mmoja akiendelea kusafisha damu zilizokuwa zimetapakaa sakafuni.

“Dada nimpigie simu bosi aje?”
“Hapana muache aendelee tu na kazi zake, kila kitu kitakuwa sawa usijali,” alisema Arianna, akageukia upande wa pili na kuendelea kulia kwa uchungu. Kitendo kilichofanywa na Diego kilimuumiza sana moyo wake.

Muda ulizidi kuyoyoma na hatimaye jioni ikafika, Msuya akarudi kutoka kazini lakini jambo la kwanza aliloambiwa lilikuwa ni juu ya matatizo yaliyompata Arianna, akashtuka kuliko kawaida huku akianza kuwalaumu wafanyakazi wake kwa kushindwa kumpa taarifa kwa wakati.

“Mwenyewe alisema tusikwambie hakutaka kukusumbua,” alisema mfanyakazi mmoja, Msuya akakimbia mbiombio mpaka chumbani kwa Arianna na kumkuta akiwa amelala, huku akiwa amevimba sehemu alizopigwa na Diego.

“Umepatwa na nini mpenzi wangu?” alisema Msuya huku akiwa haamini alichokuwa anakiona. Kutokana na jinsi msichana huyo alivyokuwa amevimba, Msuya hakutaka kupoteza muda, akambeba juujuu mpaka kwenye maegesho ya magari, akamuingiza na kuondoka kwa kasi bila kumuaga mtu yeyote.

Akamkimbiza mpaka hospitali aliyokuwa akitibiwa yeye na familia yake ambapo jambo la kwanza ilikuwa ni Arianna kutundikiwa dripu kisha daktari akaanza kumfanyia vipimo kubaini sehemu alizokuwa ameumia.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Leave A Reply