The House of Favourite Newspapers

The Angel of darkness-11

0

Shambulizi la kigaidi linatokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall na kusababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Wakenya, Watanzania na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa wahanga wa tukio hilo la kikatili, wamo Watanzania, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam, mkewe, Asia Mustafa na watoto wao mapacha waliokuwa bado wachanga, Arianna na Brianna.

Kwa bahati mbaya, Ndaki na mkewe wanapoteza maisha katika tukio hilo, maiti zao na za Watanzania wengine zinasafirishwa mpaka nchini Tanzania ambako hatimaye wanazikwa.

Pacha wa kwanza, Arianna anapatikana na kurejeshwa nchini Tanzania ambako anakabidhiwa kwa ndugu zake. Bado haifahamiki pacha mwingine, Brianna yuko wapi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.
Upande wa pili, mwanamke mwenye upungufu wa akili, Mashango anamuokota mtoto mchanga kwenye shambulizi hilo la kigaidi na kutokomea naye kwenye dampo, mahali yalipo makazi yake.

Baadaye anahamia kwenye kitongoji cha watu maskini, Mathare, pembezoni kidogo mwa Jiji la Nairobi, mahali anakoweka makazi yake. Maisha yanazidi kusonga mbele.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Maisha yalibadilika, hayakuwa kama yalivyokuwa kipindi cha nyuma, zile shida walizokuwa nazo siku za nyuma, ule umaskini uliokuwa ukiwatafuna, kwa kipindi hicho ulibaki kama historia tu.
Hans yule hakuwa huyu, yule maskini ambaye aliishi na mke wake kwa matatizo makubwa, leo hii naye alikuwa miongoni mwa watu waliobadilisha magari, alikuwa miongoni mwa watu waliomiliki kiasi kikubwa cha fedha.

Siku ziliendelea kukatika, majirani waliendelea kuushangaa uzuri aliokuwa nao mtoto Arianna uliwafanya watu wengi kuweweseka kwa kuona kwamba miaka ya baadaye mtoto huyo angekuja kuwa mrembo mno.

“Ila jamani huyu mtoto ni mzuri sana, ana sura nzuri kweli, yaani nabashiri atakuja kutikisa sana hapo baadaye,” alisema msichana mmoja, alikuwa akimwangalia Arianna ambaye alibebwa na Sophia.
“Mmh! Hata mimi mwenyewe nimemuona, tena umeniwahi, nilitaka kusema hivyohivyo,” alisema msichana mwingine.

Hakukuwa na mtu aliyenyamaza, kila aliyemuona Arianna ilikuwa ni lazima ausifie uzuri wa mtoto huyo. Siku zikasonga, matumizi ya Hans na mkewe yakawa makubwa kiasi kwamba kuna kipindi mpaka ndugu zao waliwaweka kikao na kuwasisitizia kwamba zile fedha walizokuwa nazo kwenye akaunti, mali walizokuwa wakizitumia hazikuwa zao bali za Arianna waliyekuwa wakiishi naye.
“Kwani kuna tatizo mjomba?”

“Hakuna tatizo, ila kukumbushana ni muhimu sana.”
“Basi usijali! Tunakumbuka hata kabla haujatukumbusha,” alisema Hans.
Maisha ya starehe yakaanza kuwaingia, wakawa ni watu wa kuondoka nyumbani na kwenda katika baa mbalimbali na kunywa pombe kali, kila mtu aliyewaona, aliwapapatikia, wakaanzisha ukaribu kwa ajili ya kuchuma fedha tu.

Hawakuzionea huruma fedha walizokuwa nazo, hawakuwahi kufikiria kama kuna siku wangekuja kuwa matajiri kama walivyokuwa kipindi hicho, walifanya chochote kile walichotaka kufanya pasipo kuulizwa na mtu yeyote yule.

“Ulikumbuka Flying Mouflan?”
“Hapana! Kwani nayo uliniagiza?”
“Ndiyo! Kachukue kama chupa nne hivi, chukua na konyagi, leo nataka tukae nyumbani tu,” alisikika Hans kwenye simu.

“Sawa. Nitafanya hivyo. Kingine?”
“Labda na nyama choma. Ila na keshokutwa kuna safari nataka twende.”
“Wapi?”

“Kutembelea mbuga mbalimbali za wanyama, tutaanza Mikumi na sehemu nyingine, tukizimaliza, tutakwenda hata Zanzibar kuponda raha kidogo,” alisikika Hans.

Hakukuwa na kitu kingine cha kufanya kwa wakati huo zaidi ya kutumia fedha kadiri walivyoweza.
Ulevi waliokuwa nao ukaongezeka kwa kunywa pombe kali na zilizoogopeka duniani, yote hayo walikuwa wakiyafanya kwa kuwa tu walikuwa na fedha nyingi walizopewa kama walezi wa mtoto Arianna.

Baada ya siku mbili, walikuwa safarini wakielekea katika Mbuga ya Wanyama ya Mikumi iliyokuwa mkoani Morogoro. Huko, kama kawaida yao walikuwa wakiponda raha kana kwamba hakukuwa na kifo.
Walilala katika hoteli za bei mbaya huku matumizi yao yakiwa makubwa mno kiasi kwamba baadhi ya wafanyakazi katika mbuga hiyo wakahisi kwamba watu hao walikuwa watalii kutoka nchini Marekani.
Walipotoka hapo, hawakurudi nyumbani, walikwenda katika mbuga nyingine kama Serengeti, Ngorongoro na nyinginezo, kote huko, fedha ndiyo iliyokuwa ikitumika.

Walikaa huko kwa kipindi cha mwezi mzima ndipo walirejea jijini Dar es Salaam ambapo napo hawakukaa sana, walichokifanya ni kuondoka na kuelekea Zanzibar.

Hapo ndipo ndugu walipokuja juu, kilichokuwa kikiendelea kilionekana kuwa ujinga, matumizi mabaya ya fedha kwa watu hao wakahisi kabisa kwamba mwisho wake ungekuja kuwa mbaya.
“Huu ni ujinga, sisi kama ndugu tusipolivalia njuga suala hili mwisho wa siku utakuja kuwa mbaya,” alisema mjomba wake Hans.

“Ni kweli kabisa, ni lazima tuhakikishe kwamba fedha zinatumika ipasavyo. Jana nimepigiwa simu na kuambiwa Hans na mkewe wapo mbugani, jamani, huko mbugani mwezi mzima,” alisema shangazi mtu huku akionekana kukasirika.

“Ni lazima tusimame kidete, au nyie mnaonaje?”
“Upo sawa. Kama vipi tupange watu wawafuate nyumbani kuwaambia ukweli kwani nahisi mwisho wa siku maisha ya Arianna yatakuwa kwenye wakati mgumu,” alisema mjomba wake Hans.

Hivyo ndivyo walivyopanga, kesho yake ndugu wanne wakajipanga na kwenda nyumbani kwa Hans, lengo la kwenda huko lilikuwa ni kumwambia kuhusu matumizi makubwa ya fedha ambazo ziliwekwa kwa ajili ya Arianna huku yeye na mkewe wakiwa kama wasimamizi.
“Tumekuja kumuona Hans! Tumemkuta?” waliuliza mara baada ya kufika nyumbani hapo.
“Hayupo.”

“Amekwenda wapi?”
“Zanzibar na dada, wamesema watakuja mwezi ujao,” alijibu mfanyakazi, jibu lile likawaacha hoi kwani hata walipowapigia simu, hawakupatikana.

Hicho ndicho kilichotokea, bado Hans na mkewe Sophia waliendelea kuyafurahia maisha, fedha walizokuwa nazo katika kipindi hicho ziliwapagawisha kiasi kwamba hawakutaka kusikia la mtu yeyote yule.
Katika safari zao zote, hawakutaka kuambatana na Arianna, yeye alibaki nyumbani na mfanyakazi wa ndani.

Ndugu waliwasubiri, siku zikakatika, wiki zikazidi kusogea, baada ya kubaki siku kadhaa kabla ya mwezi kuisha, taarifa zikaletwa kwamba wangerudi bali wangekwenda Kilwa kuponda raha.

Leave A Reply