The Angel Of Darkness

Shambulizi kubwa la kigaidi linatokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall na kusababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Wakenya, Watanzania na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa wahanga wa tukio hilo la kikatili, wamo Watanzania, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam, mkewe, Asia Mustafa na watoto wao mapacha waliokuwa bado wachanga, Arianna na Brianna.

Kwa bahati mbaya, Ndaki na mkewe wanapoteza maisha katika tukio hilo, maiti zao na za Watanzania wengine zinasafirishwa mpaka nchini Tanzania ambako hatimaye wanazikwa.

Pacha wa kwanza, Arianna anapatikana na kurejeshwa nchini Tanzania ambako anakabidhiwa kwa ndugu zake. Bado haifahamiki pacha mwingine, Brianna yuko wapi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Upande wa pili, mwanamke mwenye upungufu wa akili, Mashango anamuokota mtoto mchanga kwenye shambulizi hilo la kigaidi na kutokomea naye kwenye dampo, mahali yalipo makazi yake.

Baadaye anahamia kwenye kitongoji cha watu maskini, Mathare, pembezoni kidogo mwa Jiji la Nairobi, mahali anakoweka makazi yake. Maisha yanazidi kusonga mbele.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Kitu pekee ambacho Mashango hakuweza kukiacha, ilikuwa ni kwenda kwenye madampo kuokoteza mabaki ya vyakula na nguo. Ilikuwa ni lazima afanye hivyo kwani hakutaka kuona mwanaye huyo wa hiyari analala na njaa hata siku moja.

Mtoto huyo alipofikia hatua ya kuanza kutembea mwenyewe, Mashango alikuwa anapenda kutembea naye akiwa amemshika mkono, akimuonesha njia zote alizokuwa anapita kwenda kwenye madampo kujitafutia riziki. Siku zikawa zinaendelea kusonga mbele na hatimaye mtoto huyo akatimiza umri wa miaka mitatu.

Tofauti na watoto wengi waliokuwa na umri sawa na mtoto huyo ambao walikuwa wakienda kuandikishwa kwenye shule za awali, Brianna Mashango, jina alilobatizwa na mama yake huyo wa hiyari, likiwa ni mchanganyiko wa jina alilolikuta kwenye kidani alichokuwa amevalishwa mtoto huyo shingoni (Brianna) na jina lake (Mashango), hakupata fursa hiyo.

Muda wote alikuwa akishinda na mama yake kwenye madampo au kwenye kibanda chao, kamwe Mashango hakuruhusu mtoto huyo awe mbali naye hata kwa dakika chache.

Watu waliomfuata Mashango na kumshauri kuhusu kumpeleka mtoto huyo shuleni, aliwakatalia katakata, akilini mwake akihisi huenda bado ni mpango wa kutaka kumuiba mtoto wake huyo ambaye sasa aligeuka na kuwa furaha pekee maishani mwa mwanamke huyo.

Hata walimu wa shule za jirani walipomfuata na kumpa ofa ya kumfundisha bure mtoto huyo, bado Mashango hakutaka kabisa kusikia suala hilo, akatishia kuhama mtaa huo endapo mwanaye ataendelea kufuatwafuatwa.

Japokuwa alikuwa anapenda mtoto huyo aende shule na kupata elimu sawa na watoto wengine, hofu ya kuibiwa au kutekwa na watu wasiokuwa na nia njema naye, ilimfanya akatae katakata kumpeleka shuleni.

Siku zilizidi kusonga mbele, Brianna akawa anazidi kuwa mkubwa huku urembo wake ukiendelea kujidhihirisha waziwazi licha ya kwamba alikuwa akishinda dampo na mama yake huyo na kuishi maisha ya kifukara mno.

Kutokana na jinsi Mashango alivyokuwa maarufu kwenye kitongoji cha watu maskini cha Mathare, mtoto huyo naye alikuwa maarufu ndani ya muda mfupi mno, ikawa kila anakopita na mama yake, watu wanawaita wote wawili kwa majina yao.

Maisha aliyokuwa anayapitia mtoto huyo, yalimfanya akili zake zianze kufanya kazi kwa kiwango kikubwa akiwa bado na umri mdogo sana. Mashango alifurahishwa sana na maendeleo ya mtoto huyo, ikafika wakati wakawa wanazungumza pamoja utafikiri Mashango anazungumza na mkubwa mwenzake.

“Mama kwa nini sisi tunaenda kuokota vyakula kwenye dampo wakati wengine wanaenda kununua sokoni?” Brianna alimuuliza mama yake kwa lafudhi ya kitoto, Mashango akamtazama mtoto huyo akiwa ni kama haamini kusikia swali kama hilo kutoka kwa mtoto mwenye umri mdogo kiasi hicho.

“Sisi ni maskini mwanangu, hatuna fedha za kwenda kununua sokoni,” alisema Mashango huku naye akijihisi aibu kutokana na swali hilo.

“Kwa nini usitafute hela na sisi tuanze kufanya biashara, mbona mama Njoroge yeye anauza mchicha halafu anapata hela?”

Japokuwa Mashango alikuwa na akili za kiutu uzima, hakuwahi kuwaza jambo hilo hata siku moja. Kwake alisharidhika na aina ya maisha aliyokuwa anaishi. Wazo alilolitoa mtoto mdogo Brianna likazifanya akili zake zifunguke.

Kushinda kwake dampo kulimuwezesha kuwa karibu na fursa nyingi lakini kamwe hakuwahi kuwaza hata mara moja kwamba anaweza kuwa anajipatia fedha kwa kushinda kwake dampo.

Baada ya kauli hiyo ya mwanaye, alitafakari kwa muda, akashusha pumzi ndefu kisha akamgeukia Brianna ambaye kwa kipindi hicho alikuwa na umri wa miaka minne tu.

“Nimepata wazo, unaonaje tukiwa tunaenda kuokota chupa tupu za maji na kuzikusanya kisha tunaenda kuziuza kama wanavyofanya watu wengi kule dampo?”

“Sawa mama, nitakuwa nakusaidia,” alisema mtoto huyo na kuinuka, akamkumbatia mama yake kwa nguvu. Aliamini sasa hatakuwa anachekwa na watoto wenzake waliokuwa wanamwambia yeye na mama yake wanakula uchafu kwa kuokota makombo jalalani, kauli ambazo japokuwa alikuwa na umri mdogo zilikuwa zikimuumiza sana.

Kesho yake, Mashango aliwahi kuamka kama kawaida yake, akamchukua mwanaye ambaye sasa alikuwa anaweza kutembea mwenyewe bila tatizo, akamvalisha nguo kuukuu na safari ya kuelekea dampo ikaanza lakini tofauti na siku zote, siku hiyo hawakuwa wanaenda kuokota makombo ya vyakula bali kukusanya tupu za maji kwa lengo la kwenda kuziuza.

Waliifanya kazi hiyo kwa ushirikiano wa hali ya juu, mama na mwana wakawa wanakusanya chupa nyingi za plastiki na kuziweka sehemu moja, ilipofika saa nane za mchana, tayari walikuwa wamekusanya furushi kubwa, wakatafuta mifuko mikubwa na kuzijaza, Brianna akabeba mfuko mdogo wakati mama yake alijitwisha mzigo mkubwa.

Wakaenda mpaka kwenye kituo cha wafanyabiashara waliokuwa wananunua chupa hizo. Kila mtu alikuwa anamshangaa Mashango kwani hakuwa yule mwanamke mwendawazimu waliyekuwa wanamfahamu.

Walishangaa amepata wapi wazo la kukusanya chupa wakati kwa miaka nenda rudi alikuwa akiishi kwenye dampo na hakuwahi kuwa na wazo kama hilo hata mara moja.

Kila mmoja akawa anazungumza lake. Baada ya chupa hizo kupimwa kwenye mizani, walilipwa fedha kulingana na ukubwa wa mzigo, mtu na mama yake wakaondoka na kuelekea kwenye genge lililokuwa jirani.

Wakanunua mahitaji muhimu kwa ajili ya chakula kisha wakarejea kwenye banda lao na kuanza kupika, kila mtu akawa anaendelea kumshangaa Mashango kwani hata kujipikia chakula chake mwenyewe halikuwa jambo la kawaida kwake.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS
GLOBALBREAKINGNEWS.JPG

Loading...

Toa comment