The Angel of Darkness- 13

Shambulizi kubwa la kigaidi linatokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall na kusababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Wakenya, Watanzania na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa wahanga wa tukio hilo la kikatili, wamo Watanzania, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam, mkewe, Asia Mustafa na watoto wao mapacha waliokuwa bado wachanga, Arianna na Brianna.

Kwa bahati mbaya, Ndaki na mkewe wanapoteza maisha katika tukio hilo, maiti zao na za Watanzania wengine zinasafirishwa mpaka nchini Tanzania ambako hatimaye wanazikwa.

Pacha wa kwanza, Arianna anapatikana na kurejeshwa nchini Tanzania ambako anakabidhiwa kwa ndugu zake. Bado haifahamiki pacha mwingine, Brianna yuko wapi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Upande wa pili, mwanamke mwenye upungufu wa akili, Mashango anamuokota mtoto mchanga kwenye shambulizi hilo la kigaidi na kutokomea naye kwenye dampo, mahali yalipo makazi yake.

Baadaye anahamia kwenye kitongoji cha watu maskini, Mathare, pembezoni kidogo mwa Jiji la Nairobi, mahali anakoweka makazi yake. Maisha yanazidi kusonga mbele huku mtoto huyo japokuwa alikuwa mdogo, akimpa changamoto kubwa za kimaisha Mashango.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Hee! Jamani njooni muone maajabu, yule mwendawazimu Mashango eti anauza mbogamboga na matunda!”

“Haaa! Ukichaa umemuisha? Toka lini kichaa akafanya biashara?”

“Lakini jamani tuacheni masihara, unajua siku hizi Mashango amebadilika sana, ukimuona wala huwezi kudhani kwamba ni mwendawazimu, anaoga vizuri, anafua nguo zake na habebi tena uchafu kama kawaida yake, kila anakokwenda yuko na mwanaye.”

“Halafu kwa jinsi anavyomlea vizuri yule mtoto inaonesha kabisa kuwa amepona. Haiwezekani mwendawazimu akamlea mtoto vizuri. Si mnaona anavyokuwa?”

“Hamna acheni kumtetea, yule ni kichaa tu na uliwahi kuona wapi kichaa akapona bila kupelekwa hospitalini? Siwezi kununua chochote kutoka kwake,” akina mama kadhaa waliokuwa wamekaa nje ya nyumba kuukuu iliyoezekwa kwa makuti, katikati ya Mtaa wa Mathare, walikuwa wakibishana, muda mfupi baada ya Mashango kupita akiwa amejitwisha kapu la mbogamboga na matunda, akitafuta wateja huku akiwa ameongozana na mwanaye.

Japokuwa kulikuwepo na baadhi ya watu waliokuwa wakimpuuza kwa sababu tu ya historia yake, wengi walionesha kufurahishwa na maendeleo yake na kuamini kweli Mungu anaweza kutenda miujiza.

Bado kila mmoja aliendelea kuamini kwamba uwepo wa mtoto Brianna Mashanga kwenye maisha ya mwanamke huyo, ndiyo uliombadilisha kabisa. Hakuna aliyekuwa anajua nini kilisababisha awali Mashanga akachanganyikiwa na kuwa mwendawazimu wa kuokoka makopo.

Walichokuwa wanakijua ni kwamba tangu aanze kuonekana na mtoto huyo ambaye kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele alikuwa akizidi kuwa mkubwa na mrembo, maisha ya Mashango yalibadilika mno.

Siku ziliendelea kusonga mbele huku Mashango na mwanaye huyo wakiendelea kufanya biashara hiyo ya kuuza mbogamboga na matunda. Ratiba yao ya maisha ilibadilika kabisa, hawakuwa tena na muda wa kwenda dampo hasa baada ya mtaji wao kukua, wakawa hawana shida tena ya kwenda kuokota chupa tupu za maji wala makombo ya vyakula.

Mzunguko wa fedha uliotokana na biashara hiyo pekee, ulitosha kuwafanya wamudu maisha japo kwa kiwango cha chini. Wakawa wanaweza kujinunulia chakula ambacho walikuwa wakienda kujipikia wenyewe baada ya kumaliza biashara.

Fedha nyingine kidogo, Mashango akawa anampa Brianna na kumuelekeza sehemu za kuzihifadhi, kwenye kopo dogo lililokuwa limechimbiwa ardhini na kuachwa sehemu ndogo tu ya kuingizia sarafu.

“Hii ndiyo benki yetu, hatutakiwi kuchukua fedha zozote humu, kila siku inabidi tujitahidi tuwe tunaweka fedha kidogo, zitatusaidia baadaye,” alisema Mashango, wazo lililomfurahisha sana Brianna, huo ndiyo ukawa utaratibu wao.

Maisha yalizidi kusonga mbele, Mashango ambaye awali kila mtu alikuwa akimfahamu kama mwendawazimu anayeshinda dampo, sasa akawa anafahamika kama mfanyabiashara maarufu wa mbogamboga na matunda kwenye mitaa ya watu maskini ya Mathare jijini Nairobi.

Umaarufu wake ulienda sambamba na umaarufu wa Brianna ambaye kila mama yake alipokuwa anakwenda, naye alikuwa pembeni yake.

***

“Mbona Hans na mkewe wanataka kututia aibu jamani? Tutamjibu nini Arianna atakapokuja kuwa mkubwa kisha akagundua kwamba tulishindwa kusimamia vyema mali lukuki zilizoachwa na wazazi wake kwa ajili ya kumsaidia?”

“Hapa tulipofikia siyo mahali pa kuendelea kujadiliana tena, sote ni mashahidi wa jinsi Hans anavyotumia mali vibaya zilizoachwa na marehemu kaka yake. Halafu akiambiwa anajifanya kuleta ujeuri.”

“ Kinachotakiwa sasa hivi ni kwenda kufungua kesi mahakamani ya kubadilisha msimamizi wa mirathi kabla mambo hayajawa mabaya,” wanafamilia wa ukoo wa marehemu Joseph Ndaki, walikuwa kwenye kikao kizito.

Kitendo kilichokuwa kinafanywa na ndugu yao huyo, kiliwafanya washindwe kuendelea kuvumilia na kulifumbia macho suala hilo.

Mipango yote ikakamilishwa ambapo siku tatu baadaye, Hans Ndaki na mkewe wakiwa Kilwa wakiendelea kuponda raha, wanandugu hao walienda kufungua shauri mahakamani la kupinga Hans kuendelea kuwa msimamizi wa mirathi hiyo.

Taratibu za kimahakama zikafanyika ambapo Hans alitumiwa ujumbe hukohuko aliko wa kutakiwa kufika mahakamani haraka iwezekanavyo.

Kwa muda wote huo, Arianna ambaye kiumri bado alikuwa mdogo, akiwa haelewi chochote, alikuwa akiendelea vyema na masomo yake kwenye Shule ya Kimataifa ya East African, akiwa bado yupo kwenye hatua ya awali ya chekechekea (kindergaten).

Siku tatu baadaye, Hans na mkewe walirejea kutoka kuponda raha huku kila mmoja akionesha kuwa na wasiwasi mkubwa juu ya kilichosababisha waitwe mahakamani.

Hawakutaka kupoteza muda, wakaenda moja kwa moja mpaka mahakamani ambako walishtushwa mno na taarifa walizopewa kwamba wanandugu wameamua kusitisha uteuzi wa Hans kuwa msimamizi wa mirathi.

Mahakama ikawapa agizo kwamba wanatakiwa kukabidhi kila kitu walichokabidhiwa na familia hiyo walipoteuliwa kuwa wasimamizi wa mirathi.

“Mungu wangu,” alisema Hans huku akimkodolea macho mkewe kwani kiukweli japokuwa haukuwa umepita muda mrefu tangu walipokabidhiwa kazi hiyo, tayari walishatumia kiwango kikubwa cha fedha zilizokuwa benki pamoja na zilizokuwa zinaingia kupitia miradi yao mbalimbali, kwa matumizi yasiyohusiana kabisa na malezi ya mtoto.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

JIUNGE NA GLOBAL BREAKING NEWS!

globalbreakingnews.JPG

Loading...

Toa comment