The House of Favourite Newspapers

The Angel of Darkness

0

Shambulizi kubwa la kigaidi linatokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall na kusababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Wakenya, Watanzania na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa wahanga wa tukio hilo la kikatili, wamo Watanzania, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam, mkewe, Asia Mustafa na watoto wao mapacha waliokuwa bado wachanga, Arianna na Brianna.

Kwa bahati mbaya, Ndaki na mkewe wanapoteza maisha katika tukio hilo, maiti zao na za Watanzania wengine zinasafirishwa mpaka nchini Tanzania ambako hatimaye wanazikwa.

Pacha wa kwanza, Arianna anapatikana na kurejeshwa nchini Tanzania ambako anakabidhiwa kwa ndugu zake. Bado haifahamiki pacha mwingine, Brianna yuko wapi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Upande wa pili, mwanamke mwenye upungufu wa akili, Mashango anamuokota Brianna kwenye shambulizi hilo na baadaye anahamia kwenye kitongoji cha watu maskini, Mathare, pembezoni kidogo mwa Jiji la Nairobi, mahali anakoweka makazi yake.

Maisha yanazidi kusonga mbele huku mtoto huyo japokuwa alikuwa mdogo, akimpa changamoto kubwa za kimaisha Mashango. Baadaye Brianna anaanza masomo na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo maisha ya Mashango yanavyoanza kubadilika.

Anaanza kufanya biashara ya mbogamboga na matunda na kuishi maisha ya kawaida kama binadamu wengine. Hata hivyo bado kuna watu ambao hawaamini kwamba mwanamke huyo amepona, wanamfanyia fitina za hapa na pale na kusababisha akamatwe na mgambo wa Jiji la Nairobi.

Hata hivyo anaonekana hana hatia. Wanamuachia lakini kwa bahati mbaya, wakati akirejea kwenye eneo lake la biashara anapata ajali mbaya ya kugongwa na gari na kupoteza maisha papo hapo. Hilo linakuwa pigo kubwa kwa maisha ya Brianna.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Baada ya kuthibitika kwamba tayari Mashango alishaaga dunia, ilibidi mtoto Brianna ambaye alikuwa akiendelea kulia kwa uchungu achukuliwe mpaka kwenye chumba maalum ambapo askari mmoja mwanamke alianza kumtuliza na kumuuliza maswali mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sehemu wanayoishi na kama walikuwa na ndugu yeyote.

Hata hivyo, Brianna alishindwa kujibu chochote zaidi ya kuendelea kulia tu, hali iliyowapa wakati mgumu askari pamoja na madaktari kujua namna ya kumsaidia mtoto huyo kutoa taarifa kwa ndugu na jamaa wa marehemu ili taratibu za mazishi zianze kufanywa.

“Nyamaza mtoto mzuri, haya niambie mnaishi wapi?”

“Mathare.”

“Ulikuwa unaishi na nani mwingine ukimtoa mama?”

“Hakuna mwingine.”

“Ndugu zenu wengine wako wapi?”

“Sijui.”

***

Taarifa za kifo cha Mashango zilisambaa kama moto wa nyika, watu wengi waliokuwa wakimfahamu walisikitishwa mno na kifo chake cha ghafla. Wengi kati yao walikuwa wakijiuliza kuhusu hatma ya mwanaye mdogo aliyemuacha, Brianna. Hakuna ambaye alijua mtoto huyo ataishije baada ya kuondokewa na mama yake.

Watoto ambao walizoea kumtania kipindi akiwa mwendawazimu, nao walionesha kuguswa sana na kifo cha Mashango, wengi wakawa wanashindwa kuyazuia machozi yasizilowanishe nyuso zao.

Kilichowaumiza wengi, ni kwamba Mashango alifariki dunia katika kipindi ambacho alikuwa ameshapona kabisa tatizo la kurukwa na akili lililomsumbua kwa miaka mingi.

“Mungu naye ako na majaribu yake. Yule Mashango kashindwa kugongwa na motokari akiwa mwehu leo kapona ndiyo kafa?” mwanaume mmoja alizungumza kwa Kiswahili cha Kikenya na kuungwa mkono na wenzake wengi aliokuwa akizungumza nao.

Wengi waliamini kwamba katika kipindi ambacho Mashango alitakiwa kufa hata kama ni kwa ajali, ni kipindi alichokuwa mwendawazimu kwani kuna wakati alikuwa akifikia hatua ya kutembea katikati ya barabara au wakati mwingine kulala kabisa barabarani lakini wala hakuwahi kugongwa hata siku moja.

Gumzo la kifo cha Mashango liliendelea kusambaa kwa kasi lakini swali ambalo hakuna ambaye aliweza kulijibu, ni mahali walipokuwepo ndugu wa Mashango. Wakazi wengi wa Nairobi walizoea kumuona Mashango akiwa peke yake kwa kipindi kirefu kabla ya baadaye kuanza kumuona akiwa na mtoto Brianna tangu alipokuwa mchanga kabisa.

Hakuna aliyekuwa anajua historia yake wala mahali alikotokea, jambo lililowapa kazi kubwa madaktari wa hospitali aliyopelekwa pamoja na askari wa kikosi cha usalama barabarani. Ilibidi wakubaliane kutoa taarifa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kama kuna mtu yeyote aliyekuwa akimfahamu mwanamke huyo.

Baada ya saa 72 kupita bila kuwa na taarifa za mtu yeyote aliyekuwa anamfahamu Mashango, ilibidi Manispaa ya Jiji la Nairobi ichukue jukumu la kwenda kuuzika mwili wa mwanamke huyo. Hatimaye mwili wa Mashango ukazikwa na manispaa kwenye Makaburi ya Mathare na kuhudhuriwa na watu wachache, akiwemo mtoto Brianna.

“Mimi naomba nimchukue huyu mtoto nikaishi naye nyumbani kwangu.”

“Unaitwa nani?”

“Wailima Njoroge.”

“Unaishi wapi?”

“Mathare, ni jirani na alipokuwa akiishi marehemu.”

“Ok, sawa. Sasa kwa sheria za hapa Kenya ni lazima kwanza upitie Wizara ya Jinsia na Watoto, kisha baada ya hapo utaenda kula kiapo mahakamani ndiyo utaruhusiwa kumchukua,” alisema daktari maalum aliyeongozana na maafisa wa Manispaa ya Jiji la Nairobi, muda mfupi baada ya mazishi ya Mashango.

Baada ya maelezo hayo, daktari huyo mwanamke ambaye ndiye aliyepewa jukumu la kumsimamia mtoto Brianna wakati wa mazishi ya mama yake, alimfuata mtoto huyo aliyekuwa amelilalia kaburi akiendelea kulia kwa uchungu na kumuinua, akambeba bila kujali kwamba atachafua koti lake jeupe la kidaktari, akawa anaendelea kumbembeleza.

Baada ya shughuli hiyo kukamilika, watu wote walitawanyika na Wailima Njoroge, jirani wa marehemu Mashango aliyekuwa akimpenda sana mtoto huyo na kutamani awe wake, aliondoka na kuelekea moja kwa moja kwenye Wizara ya Jinsia na Watoto ya Kenya kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kumchukua mtoto huyo.

Kutokana na ukweli kwamba mtoto huyo hakuwa na mahali pa kwenda baada ya kifo cha mama yake, maombi ya Njoroge yalishughulikiwa haraka na baada ya siku moja tu, akawa tayari ameshakamilisha kila kitu, akaenda mahakamani kuapa akiwa na mtoto huyo na kukabidhiwa rasmi kuwa mlezi wake, huku akipewa pia jukumu la kuhakikisha anaendelea na masomo.

Japokuwa haikuwa rahisi kwa Brianna kuyazoea mazingira mapya, kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele ndivyo alivyokuwa akianza kuzoeana na watoto watatu wa Njoroge na kuwaona kama sehemu ya familia yake, roho nzuri ya mama wa familia hiyo pamoja na Njoroge mwenyewe, vikamfanya aendelee kusahau taratibu pengo la kuondokewa na mama yake.

Siku kadhaa baadaye aliendelea na masomo, taratibu akaanza kurudi kwenye hali yake ya kawaida. Pale alipokuwa akimkumbuka sana mama yake, marehemu Mashango, alikuwa akitoka na kwenda kwenye kaburi lake ambapo alikuwa akitumia saa kadhaa kukaa juu ya kaburi, akilia na kumuombea kwa Mungu apumzike kwa amani.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Leave A Reply