The House of Favourite Newspapers

The Angel of darkness -15

0

Shambulizi kubwa la kigaidi linatokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall na kusababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Wakenya, Watanzania na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa wahanga wa tukio hilo la kikatili, wamo Watanzania, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam, mkewe, Asia Mustafa na watoto wao mapacha waliokuwa bado wachanga, Arianna na Brianna.

Kwa bahati mbaya, Ndaki na mkewe wanapoteza maisha katika tukio hilo, maiti zao na za Watanzania wengine zinasafirishwa mpaka nchini Tanzania ambako hatimaye wanazikwa.

Pacha wa kwanza, Arianna anapatikana na kurejeshwa nchini Tanzania ambako anakabidhiwa kwa ndugu zake. Bado haifahamiki pacha mwingine, Brianna yuko wapi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Upande wa pili, mwanamke mwenye upungufu wa akili, Mashango anamuokota mtoto mchanga kwenye shambulizi hilo la kigaidi na kutokomea naye kwenye dampo, mahali yalipo makazi yake.

Baadaye anahamia kwenye kitongoji cha watu maskini, Mathare, pembezoni kidogo mwa Jiji la Nairobi, mahali anakoweka makazi yake. Maisha yanazidi kusonga mbele huku mtoto huyo japokuwa alikuwa mdogo, akimpa changamoto kubwa za kimaisha Mashango.

Taratibu maisha ya Mashango yanaanza kubadilika kutokana na uwepo wa mtoto huyo, anaanza kufanya biashara ya mbogamboga na matunda na kuishi maisha ya kawaida kama binadamu wengine. Upande wa pili, Hans na mkewe wanatumia vibaya mali za marehemu na baadaye wanaamua kutoroka kuukwepa mkono wa sheria na kumtelekeza mtoto Arianna.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Taarifa za kutoroka kwa Hans na mkewe zilipokelewa kwa mshtuko mkubwa na ndugu wa ukoo wa Ndaki, hakuna aliyeamini kwamba Hans na mkewe wanaweza kufikia hatua ya kukosa utu ndani ya mioyo yao kiasi hicho.

Ilibidi waitane haraka kwa ajili ya kujadiliana nini cha kufanya kumsaidia mtoto Arianna ambaye hatima yake ilikuwa haijulikani.

Katika kikao hicho cha wanandugu, iliamriwa kwamba taarifa ziende kutolewa haraka mahakamani wakati wanandugu wengine wakiendelea kupiga mahesabu ya hasara iliyosababishwa na Hans tangu alipokabidhiwa kazi ya kusimamia mirathi kwa ajili ya mtoto Arianna.

Kilichozidi kuwachanganya wanandugu ni baada ya kugundua kuwa akaunti zote za benki zilizoachwa na wazazi wa Arianna zikiwa na kiwango kikubwa cha fedha, zilikuwa hazina kitu mpaka muda huo.

“Hans amepatwa na nini mpaka anakuwa mkatili kiasi hicho? Tena kwa mtoto wa kaka yake kabisa wa damu? Ama kweli ubinadamu kazi,” alisema ndugu mmoja katika kikao hicho, kila mtu akawa anamsikitikia Arianna.

Muafaka wa mwisho walioufikia, ilikuwa ni kwamba Arianna achukuliwe na kwenda kuishi kwa ndugu yao mwingine wakati wakiendelea kusubiri taratibu za kimahakama kutaka kujua itaamua nini kuhusu mtoto huyo.

Siku kadhaa baadaye, mahakama iliamua kubatilisha usimamizi wa mirathi uliokuwa chini ya Hans na hati ya kukamatwa kwake ikatolewa haraka. Akaanza kusakwa kila kona ili akajibu mashtaka yaliyokuwa yanamkabili. Hata hivyo haikuwa kazi nyepesi kumpata kwani tayari alishaondoka na kuelekea kusikojulikana na famili yake yote.
***
Siku ya kwanza kwa Brianna shuleni ilikuwa ngumu sana lakini alijitahidi kuendana na mazingira kwa kadiri ya uwezo wake. Wanafunzi wenzake walikuwa wakimtania na kumzodoa sana kwamba mama yake ni kichaa lakini mwenyewe hakuwa akijali, kilichompeleka shuleni ilikuwa ni kusoma na nguvu zake zote alizielekeza kwenye masomo.

Ndani ya siku chache tu tangu aanze masomo, uwezo wake darasani ukaanza kuonekana na kuwashangaza wengi. Alikuwa na kichwa chepesi kiasi kwamba haikumuwia vigumu kujua kusoma na kuandika kama ilivyokuwa kwa wanafunzi wengine.

Taratibu akaanza kuwa kipenzi cha walimu na wanafunzi wenzake, hata wale waliokuwa wakimtania kuhusu mama yake, nao walianza kumheshimu kutokana na uwezo wake mkubwa darasani, ukichanganya na urembo wa asili ambao haukuweza kufichika mbele za macho ya watu.

Siku zilizidi kusonga mbele, hayo ndiyo yakawa maisha mapya ya Brianna, asubuhi akawa anawahi kwenda shule na akitoka tu, anaenda kuungana na mama yake kutembeza mbogamboga na matunda mitaani, biashara iliyozidi kuyabadilisha maisha yao.

Akili ya Mashango nayo ilizidi kuimarika kadiri siku zilivyokuwa zinasonga mbele, akazidi kustaarabika na kubadilika kwa kila kitu, usingeweza kuamini kwamba ni Mashango huyo ndiye siku za nyuma alikuwa mwendawazimu kabisa, akishinda kutwa nzima kwenye madampo.

“Brianna.”
“Abee mama.”
“Umekuwa dawa kubwa sana kwenye maisha yangu. Umeniponya mwanangu.”
“Kwa nini unasema hivyo mama?”

“Unajua kwa sababu gani siku ile nilipokupeleka shuleni kuanza masomo wenzako walikuwa wananiita kichaa?”

“Sijui mama,” alijibu mtoto Brianna huku akikaa vizuri ili kumsikiliza mama yake huyo, jioni moja wakiwa wamejipumzisha nje ya banda lao baada ya kumaliza biashara. Japokuwa kiumri Brianna alikuwa mdogo sana, Mashango alikuwa akizungumza naye kama anaongea na mkubwa mwenzake.

Akaanza kwa kumsimulia maisha yake ya zamani aliyowahi kupitia kabla hajachanganyikiwa akili na kila kitu kilichoendelea mpaka akajikuta anakuwa kichaa. Ilikuwa ni simulizi ambayo kama angepata nafasi ya kuielezea kwa watu, kila mmoja angemuonea huruma kwa jinsi alivyoteseka.

Alimueleza jinsi alivyoolewa na mwanaume mwenye uwezo mkubwa kifedha lakini tatizo kubwa likawa kwa Mashango kushindwa kubeba ujauzito. Alisimulia jinsi alivyoteswa na ndugu wa mwanaume waliokuwa wakimsimanga kila kukicha kwa sababu hazai na jinsi walivyoamua kwenda kumroga ili aachane na ndugu yao.

“Kama nisingeamua kuikimbia ndoa yangu huenda ningeshakuwa marehemu hivi sasa kwani walifikia hatua ya kunitegeshea uchawi mpaka ndani ya chumba nilichokuwa nalala, ikabidi nikimbie na kwenda mitaani ambako nilikuwa nalala kwenye stendi za mabasi, mvua, baridi, mbu na kila aina ya shida zote zikiniishia mimi, nikajikuta naanza kupoteza kumbukumbu na kujitambua na mwisho nikaishia kuwa kichaa,” alisema Mashango kwa uchungu, Brianna akajikuta akiangua kilio na kumkumbatia mama yake huyo huku akimbembeleza kwani Mashango naye alikuwa analia wakati anasimulia.

Hata hivyo, hakumfafanulia kila kitu Brianna kuhusu jinsi alivyompata na hata mtoto huyo alipojaribu kudadisi, Mashango aliishia kumwambia kuwa mambo mengine atayajua akishakuwa mkubwa.

“Wewe elewa kwamba mini ndiyo mama yako mzazi na nitakulea mwenyewe mpaka utakapokuja kuwa mkubwa,” alisema Mashango, wakakumbatiana tena na Brianna.

Siku zilizidi kusonga mbele, biashara yao ya mbogamboga na matunda ikazidi kushamiri hadi wakafikia hatua ya kubadilisha mfumo wa kufanya biashara, kwamba badala ya kuzungusha mitaani, waliamua kujenga genge dogo na kuongeza bidhaa mbalimbali, mtaji ukawa unazidi kuwa mkubwa.

Leave A Reply