The Angel of darkness 19
Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall jijini Nairobi wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.
Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna. Arianna anaokotwa na vikosi vya uokoaji na kurejeshwa Tanzania ambako awali anakabidhiwa kwa mdogo wa marehemu baba yake, Hans ambaye anapewa jukumu la kusimamia mirathi na kumlea mtoto huyo.
Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango na kwenda kuanza naye maisha kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Japokuwa mwanamke huyo alikuwa amechanganyikiwa akili, lakini anamlea vizuri mtoto huyo na kadiri muda unavyozidi kusonga mbele, ndivyo anavyozidi kuwa mkubwa huku mwanamke huyo naye akipona maradhi ya akili yaliyokuwa yanamsumbua.
Siku zinazidi kusonga mbele na kwa bahati mbaya zaidi, Mashango, mwanamke aliyekuwa akimlea Brianna kwa mapenzi makubwa, anagongwa na gari na kupoteza maisha, jambo linalomuathiri sana Brianna. Baadaye anajitokeza msamaria mwema, Wailima Njoroge ambaye anaamua kumchukua mtoto huyo na kuishi naye pamoja na familia yake.
Upande wa Arianna, maisha yanaanza kumuendea kombo ambapo Hans anatumia vibaya mali alizoachiwa Arianna na baadaye anatorokea kusikojulikana na familia yake. Arianna anaendelea kukua lakini kwa sababu ya kukosa uangalizi wa karibu, anajikuta akiingia kwenye vitendo viovu, ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…
Kitendo cha Arianna kuanza kutumia madawa ya kulevya kilimshtua mno kila aliyekuwa anamfahamu. Akawa na mabadiliko makubwa kimwili na kiakili, hakuwa Arianna yule aliyekuwa akisifiwa na kila mmoja kutokana na urembo wa asili aliojaliwa, ndani ya kipindi kifupi alidhoofika mno.
Mbaya zaidi, hata nyumbani kwao hakukanyaga tena, tangu alipoanza kujidunga madawa hayo, alijikuta akinogewa na mchezo huo kiasi cha kuhamishia makazi yake kwenye vijiwe vya wahuni, mahali kulipokuwa kunauzwa Cocaine.
Ndugu zake waliendelea kumtafuta kwa udi na uvumba na hatimaye wakafanikiwa kumpata akiwa hajitambui, baada ya kujidunga madawa hayo, wakambeba na kumrudisha nyumbani ambapo baadaye aliporejewa na fahamu zake baada ya unga kupungua kwenye damu yake, alijikuta akiwa amezungukwa na ndugu zake.
“Arianna!”
“Abee.”
“Unafanya nini binti yetu? Mbona unatusikitisha sana?”
“Mimi sijafanya kitu, kwanza hapa nimefikaje?”
“Tumekukuta kwenye vijiwe vya wahuni ukiwa hujitambui kutokana na kujidunga madawa ya kulevya. Umeanza lini mchezo huu?”
“Mimi situmii madawa ya kulevya, wananisingizia tu. Ila pombe nakunywa sikatai.”
“Usitufanye sisi sote hapa ni watoto wenzako. Hata unavyoongea inaonesha wazi kwamba unatumia madawa ya kulevya, tazama mdomo ulivyokuwa mzito,” alisema mzee Michael na kuungwa mkono na wanandugu wengine waliokuwa wamemzunguka Arianna lakini mwenyewe aliendelea kukataa.
Juhudi za kujaribu kumpa ushauri nasaha juu ya kuachana na matumizi ya madawa hayo hatari hazikuzaa matunda kwani Arianna hakuwa tayari kukiri kwamba anatumia madawa hayo na ndugu zake walipoendelea kumpa ushauri, alitishia kuondoka.
Ikabidi waitane pembeni na kushauriana juu ya nini cha kufanya, mmoja akatoa wazo kwamba inabidi apelekwe kwenye vituo maalum vya kuwasaidia waathirika wa madawa ya kulevya (rehab) ili aondokane na matumizi ya madawa hayo kabla mambo hayajawa mabaya zaidi.
Hakuna aliyekuwa na taarifa kwamba wakati wakijadiliana hayo, Arianna alikuwa akiwasikiliza, naye akawa anajipanga namna ya kuwatoroka. Mpaka ndugu hao wanafikia muafaka wa nini cha kufanya, tayari Arianna alikuwa ameshatoka ndani ya nyumba hiyo kwa kupitia mlango wa nyuma na kutokomea kusikojulikana.
Baada ya kutoroka nyumbani, Arianna aliamua kubadilisha kijiwe, akaenda kwenye maskani nyingine ya wahuni kulipokuwa kunauzwa madawa ya kulevya. Hayo ndiyo yakawa maisha yake mapya, akawa anashinda vijiweni na kurudi nyumbani kwao kulala nyakati za usiku. Siku nyingine alikuwa akilala hukohuko.
Tabia ya matumizi ya madawa ya kulevya, ilimfanya kuingia kwenye tabia nyingine hatarishi ya kufanya ngono hovyo, hasa akishajidunga madawa hayo. Kutokana na jinsi alivyokuwa na mvuto wa kipekee, wanaume wengi walikuwa wakitamani kufanya naye mapenzi, wakawa wanampa ofa ya kumnunulia unga kisha akishalewa wanamuingilia kimwili kwa urahisi.
Siku zilizidi kuyoyoma, ikafika mahali, dozi aliyokuwa anatumia ikawa imeongezeka kiasi cha kushindwa kumudu kununua, akaanza tabia nyingine ya kwenda kuchukua vitu vya thamani nyumbani kwao au kwa ndugu zake na kwenda kuviuza bila ruhusa ili apate fedha za kwenda kununulia unga.
“Sikia mrembo, mi naona kama unahangaika sana kupata fedha za kununulia ‘ngada’ wakati una vitega uchumi kibao, kwa nini usiuze ule mjengo wenu?”
“Tatizo hati mshkaji wangu, ningeshausukuma kitambo.”
“Kwani hati ipo kwa nani?”
“Anayo dingi mkubwa, lakini mtu mwenyewe mnoko kama nini.”
“Sasa mbona kazi rahisi hiyo, inabidi tusuke mpango wa kwenda kumuibia, au we unaonaje?” Diego, kijana mhuni aliyekuwa akimuuzia madawa ya kulevya Arianna alimpa ushauri ambao msichana huyo mdogo alikubaliana nao.
Wakapanga njama ambapo Arianna alimchorea ramani Diego kisha wakaanza kuvizia siku ambayo hakutakuwa na mtu nyumbani kwa mzee huyo ili wakatimize azma yao.
Baada ya kuvizia kwa zaidi ya wiki mbili, hatimaye walipata upenyo Jumapili moja wakati ndugu wote wakiwa wameenda kanisani ambapo Diego aliingia mpaka chumbani kwa mzee huyo na kwenda kupekua kwenye sanduku, akafanikiwa kupata hati ya nyumba hiyo.
Kwa kuwa tayari walishatafuta madalali, baada ya kuipata hati hiyo, zoezi la kuiuza nyumba hiyo lilifanyika harakaharaka, mteja akapatikana siku hiyohiyo na kesho yake, Arianna akakabidhiwa kiwango cha shilingi milioni sabini.
“Inabidi tutorokee Arusha, mimi nitakuwa nakulinda au unasemaje?” Diego alimwambia Arianna baada ya kupata fedha hizo, wazo ambalo msichana huyo alilikubali. Siku hiyohiyo wakapanda basi na kukimbilia Arusha ambako walienda kutafuta nyumba ya kupanga na kuyaanza maisha mapya.
Wakawa wanashinda ndani wakijidunga madawa ya kulevya kisha baada ya hapo wanafanya ngono na kulala fofofo. Huku nyuma, ndugu wa Arianna walipokea kwa mshtuko taarifa za kuibwa kwa hati ya nyumba kisha kuuzwa kwa nyumba aliyoachiwa Arianna na wazazi wake.
Ikabidi waanze kumtafuta Arianna kwani kila mmoja alijua lazima yeye ndiye mhusika wa tukio hilo lakini jitihada zao za kumtafuta hazikuzaa matunda kwani tayari alishatorokea Arusha akiwa na Diego.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.