The House of Favourite Newspapers
gunners X

The angel of Darkness-20

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna. Arianna anaokotwa na vikosi vya uokoaji na kurejeshwa Tanzania ambako awali anakabidhiwa kwa mdogo wa marehemu baba yake, Hans ambaye anapewa jukumu la kusimamia mirathi na kumlea mtoto huyo.

Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango na kwenda kuanza naye maisha kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Japokuwa mwanamke huyo alikuwa amechanganyikiwa akili, lakini anamlea vizuri mtoto huyo na kadiri muda unavyozidi kusonga mbele, ndivyo anavyozidi kuwa mkubwa huku mwanamke huyo naye akipona maradhi ya akili yaliyokuwa yanamsumbua.

Siku zinazidi kusonga mbele na kwa bahatri mbaya zaidi, Mashango, mwanamke aliyekuwa akimlea Brianna kwa mapenzi makubwa, anagongwa na gari na kupoteza maisha, jambo linalomuathiri sana Brianna. Baadaye anajitokeza msamaria mwema, Wailima Njoroge ambaye anaamua kumchukua mtoto huyo na kuishi naye pamoja na familia yake.

Upande wa Arianna, maisha yanaanza kumuendea kombo ambapo Hans anatumia vibaya mali alizoachiwa Arianna na baadaye anatorokea kusikojulikana na familia yake. Arianna anaendelea kukua lakini kwa sababu ya kukosa uangalizi wa karibu, anajikuta akiingia kwenye vitendo viovu, ikiwemo matumizi ya madawa ya kulevya.

Baadaye Arianna anaamua kuuza nyumba aliyoachiwa na wazazi wake kinyemela na kutorokea Arusha akiwa na Diego. Kijana huyo anaendelea na biashara ya madawa ya kulevya na kwa bahati mbaya, polisi wanafanikiwa kupajua mahali alipokuwa akiishi na Arianna.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Diego yuko wapi?” alihoji askari mmoja aliyeonesha kuwa na mamlaka kuliko wenzake huku askari wengine wakianza kupekua ndani ya chumba hicho.

“Diego hakai hapa,” alisema Arianna kwa sauti iliyoonesha dhahiri kwamba ametopea kwenye matumizi ya madawa ya kulevya. Kauli hiyo ilionesha kuwaudhi wale askari, mmoja wao akamnasa Arianna kibao kwa nguvu na kusababisha adondoke chini, damu zikaanza kumtoka mdomoni.

Bila kupoteza muda, kiongozi wao waliamuru Arianna afungwe pingu, jambo ambalo lilitekelezwa, ndani ya sekunde chache baadaye, Arianna alitolewa nje na kwenda kupakizwa kwenye gari la polisi lililokuwa nje ya nyumba hiyo, akiwa amefungwa pingu mikononi kwa nyuma.

“Diego! Umeniponzaa…” alisema Arianna kwa sauti iliyoonesha alikuwa akiugulia maumivu makali. Katika hali ambayo hakuitegemea, alisikia muungurumo wa pikipiki ikija kwa kasi, akajua moja kwa moja kwamba lazima alikuwa ni Diego kwani huo ndiyo usafiri aliokuwa anapenda kuutumia.

Alitamani angekuwa na uwezo wa ziada wa kumpa taarifa mpenzi wake huyo ili kama inawezekana ageuze haraka na kupotea eneo hilo lakini haikuwezekana. Wale askari waliokuwa wamejigawa, wengine wakiendelea kukusanya ushahidi ndani ya chumba hicho na wengine wakiwa wametanda nje, walisikia muungurumo huo wa pikipiki, wakaziweka silaha zao tayaritayari.

Kufumba na kufumbua, Diego alitokezea akiwa amepakizwa kwenye bodaboda, akiwa hajui hili wala lile lakini akashtuka kukuta nyumba yote ikiwa imezingirwa na polisi.
“Diego kimbia, polisi wanakutafuta,” Arianna alipiga kelele kwa sauti ya juu akiwa ndani ya gari la polisi, akatulizwa kwa rungu la polisi lililotua kwenye miguu yake na kusababisha alie kwa maumivu makali.

“Geuza! Geuza, kimbia tuondoke haraka,” alisema Diego akimhimiza dereva wa bodaboda aliyopanda lakini tayari alishachelewa, askari wenye silaha walishawazingira na kutoa amri ya kuwataka kujisalimisha vinginevyo wangewafyatulia risasi.

Diego na dereva wake wa bodaboda wakanyakuliwa kama vifaranga vya kuku vinavyozolewa na mwewe, wakawekwa chini ya ulinzi na kufungwa pingu.

Baada ya kupekuliwa sana, dereva wa bodaboda aliachiwa baada ya kubainika kwamba hakuwa akihusika na chochote, Diego akaunganishwa na Arianna kwenye gari, wakachukuliwa na kupelekwa kituo kikuu cha polisi jijini Arusha wakiwa na vithibitisho vyote vilivyokutwa ndani ya chumba changu.

Walipofikishwa, waliteremshwa chini ya ulinzi mkali na kuingizwa mahabusu, kila mmoja upande wake. “Chalii angu huu msala umewakalia vibaya kinoma, lazima mgongwe nyundo kibao nyuma ya nondo arifu,” askari mmoja alikuwa akizungumza na Diego kwa Kiswahili chenye lafudhi ya Arusha, wakiwa ndani ya kituo kikuu cha polisi.

“Afande, tusaidie tutoke, tupo tayari kukupa kiasi chochote cha fedha unachotaka,” Diego alimnong’oneza askari huyo kwa sauti ya chini, akatingisha kichwa kuonesha kwamba amemuelewa.

Kutokana na kiwango kikubwa cha madawa waliyokamatwa nayo Diego na Arianna, faili la kesi yao liliandaliwa haraka na ndani ya saa chache tu, tayari mchakato wa kuwapeleka mahakamani ulishaanza kufanyika.

“Afande, fanya mpango basi, ujue tutafungwa ukizidi kuchelewa?”
“Kama nilivyokwambia chalii yangu, kesi yako imekaa vibaya, wakuu kibao wote wanaitolea macho, yaani hata kama ni mkwanja inabidi ukate wa kuelewa maana kila mtu anataka kuona mnapigwa mvua nyingi fasta,” yule askari aliyeahidi kuwasaidia Diego na Arianna, alimwambia Diego, hali iliyozidi kumchanganya.

Baada ya taratibu zote kukamilika, hatimaye siku iliyofuatia, Arianna na Diego walipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka yaliyokuwa yanawakabili, Arianna akiwa mtuhumiwa namba mbili katika kesi hiyo.

Hata hivyo, kwa kuwa tayari Diego alishaandaa mazingira ya kutoa ‘kitu kidogo’, baada ya kusomewa mashtaka hayo, hakimu alitangaza kuwa dhamana yao ipo wazi. Kwa kuwa Diego alikuwa akishirikiana na mtandao mpana wa wauza madawa ya kulevya jijini Arusha, wote wawili waliwekewa dhamana siku hiyohiyo.

Hata hivyo, kutokana na jinsi kesi ilivyokuwa imewakalia vibaya, walilazimika kuhonga fedha nyingi kwa maafisa wa polisi, waendesha mashtaka na hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, kitendo kilichosababisha waishiwe fedha zote walizokuwa nazo, kuanzia zile Arianna alizouza nyumba yao mpaka mtaji wa madawa ya kulevya.

Leave A Reply