The House of Favourite Newspapers

The Angel of darkness – 29

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba wawili hao ni wapenzi.

Hatimaye wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya. Mapenzi kati ya Arianna na Msuya yanaanza kukolea, jambo linalosababisha Diego awe kwenye wakati mgumu sana kihisia kutokana na wivu uliokuwa ukimsumbua kila kukicha.

Asubuhi moja, Msuya anaondoka kuelekea kazini lakini huku nyuma, Arianna na Diego wanakutana kama kawaida yao. Baadaye Msuya anagundua kwamba amesahau kitu nyumbani kwake ambapo anarudi ghafla bila taarifa. Inabakia kidogo awafume Arianna na Diego wakiwa bafuni wanaogeshana.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Ni mpaka gari la Msuya lilipoondoka ndipo Arianna aliporudi kwenye hali yake, akashusha pumzi ndefu na kuinua mikono juu kama ishara ya kumshukuru Mungu wake kwani hakuelewa nini kingetokea kama angewakuta. Diego aliendelea kutulia chumbani kwake kwa muda mrefu mpaka baadaye sana ndiyo akatoka na kumfuata Arianna chumbani kwake.

Kama kawaida yao, walijidunga madawa ya kulevya, wakafanya mapenzi kisha Diego akatoka na kumuacha Arianna akiwa amelala fofofo.

Arianna hakuamka mapema, hata wafanyakazi wa nyumba hiyo walipojaribu kwenda kumuamsha kwa ajili ya kutekeleza maagizo waliyoachiwa na bosi wao, Arianna hakuamka mpaka jioni Msuya aliporudi. Akaenda kumuamsha Arianna ambaye alijifanya anaumwa ndiyo maana amelala muda wote huo.

“Kwa nini mchana hukula chakula kama tulivyokubaliana?”
“Sijisikii hamu ya kula.”
“Inabidi ujilazimishe Arianna, unafikiri kama huli utapata wapi nguvu na siku ndiyo zimekaribia kuelekea kwenye ndoa yetu?”

“Naumwa mpenzi wangu, hata sijisikii kula chochote.”
“Lakini mbona vipimo vinaonesha huna ugonjwa wowote? Au tuende kwenye hospitali nyingine kupima?”

“Usijali, huna haja ya kuhangaika naamini nitapona tu wala usiwe na wasiwasi.”
“Lakini ndoa yetu imekaribia Arianna, utaweza kweli kurudi kwenye hali yako ya kawaida?”

“Nitaweza Msuya wala usiwe na wasiwasi,” Arianna alisema huku akionesha kuwa mchovu sana. Msuya alimuacha aendelee kupumzika, akaendelea kulala mpaka muda wa chakula cha jioni ambapo Msuya alimfuata tena chumbani kwake na kuanza kumbembeleza waende kula pamoja.

Ili kumfurahisha Msuya, ilibidi Arianna aamke na kwenda kula japokuwa hakuwa na hamu ya kula hata kidogo kutokana na madawa aliyojidunga. Akajikongoja mpaka sebuleni ambapo muda mfupi baadaye, Diego naye alijumuika nao ambapo tofauti na siku iliyopita, alionekana kurudi kwenye hali yake ya kawaida.

Kilichomfurahisha zaidi ilikuwa ni kumuona Arianna akiwa kwenye hali ya kupoteza mwelekeo. Hakuna jambo ambalo Diego alikuwa halipendi kama kumuona Arianna akifunga ndoa na Msuya na kuwa mume na mke halali.

“Dada yako anaumwa sana hata sielewi ni nini kwa sababu vipimo vinaonesha kuwa hana tatizo lolote.”

“Wala usihangaike shemeji, dada ndivyo alivyo kuna wakati anaweza kuumwa na hospitali vipimo vikaonesha haumwi chochote. Atapona tu.”
“Lakini ndoa yetu iko karibu, akiendelea kuwa kwenye hali hii unafikiri itakuwaje shemeji?”

“Atapona tu hata kabla ya hiyo ndoa yenyewe, wala usiwe na wasiwasi,” Diego alikuwa akizungumza na Msuya wakati wakiendelea kupata chakula cha jioni. Kwa muda wote huo, Arianna alikuwa kimya kabisa, akisikiliza mazungumzo yote.

Ndani ya moyo wake alijisikia vibaya sana kutokana na kilichokuwa kinaendelea. Kutokana na mapenzi ya dhati aliyokuwa akimuonesha, nafsi yake ilikuwa ikiendelea kumsuta na kukiri ndani ya nafsi yake kwamba Msuya hakustahili kulipwa mabaya.

“Lazima nijitoe kwenye hali hii,” aliwaza Arianna wakati akiendelea kusikiliza mazungumzo kati ya Msuya na Diego huku mwanaume huyo akionesha kuchanganyikiwa mno na hali aliyokuwa nayo mkewe mtarajiwa.

Baaada ya kumaliza chakula, Arianna alikuwa wa kwanza kuinuka na kuelekea chumbani kwake, akajifungia mlango kwa ndani na kuendelea kuuchapa usingizi.
Huku nyuma, Msuya aliendelea kuzungumza na Diego mambo mbalimbali, baadaye wakaagana na kila mmoja akaelekea chumbani kwake kulala huku Diego akijipongeza ndani ya nafsi yake kwa mafanikio yaliyokuwa yakiendelea kuonekana.

Siku hiyo ilipita, kesho yake asubuhi, kama kawaida Msuya alienda chumbani kwa Arianna kumjulia hali. Tofauti na siku iliyopita, Arianna alionekana kuwa kwenye hali nzuri kwa sababu madawa ya kulevya yalikuwa yamepungua sana mwilini mwake.

“Nimeongea sana jana na kaka yako na amenihakikishi kwamba utakuwa sawa bila hata kwenda hospitalini.”

“Ni kweli, ni kawaida yangu kuna kipindi huwa nakuwa hivi lakini usijali nitapona.”
“Lakini nina wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wangu kwa sababu siku zimeisha kabla ya harusi yetu, au tuisogeze mbele?”

“Huna haja ya kufanya hivyo mpenzi wangu, niamini ninachokwambia, nitakuwa sawa tu wala usijali,” Arianna aliendelea kusisitiza, Msuya akambusu kwenye paji la uso wake na kumuaga kwa sababu muda wa kwenda kazini ulikuwa umefika.

Akatoka na kuelekea kwenye maegesho ya magari ambapo aliingia ndani ya gari jingine, Nissan Murano ambalo hakuwa akilitumia mara kwa mara na safari ya kuelekea kazini kwake ikaanza.

Alipoondoka tu, kama kawaida yake, Diego alitoka chumbani kwake harakaharaka na kuelekea chumbani kwa Arianna.

“Vipi mpenzi wangu,” alisema Diego huku akitaka kumbusu Arianna mdomoni lakini alimtoa na kusimama pembeni.
“Nisikilize Diego, haya maisha mimi siyawezi.”

“Vipi kwani mpenzi wangu? Nini kimetokea?”
“Msuya hastahili kulipwa mabaya kiasi hiki. Wewe mwenyewe unajua tulikuwa tunaishi maisha gani kabla ya kukutana na huyu baba wa watu. Anajitahidi kunitunza mimi na wewe mpaka amefikia hatua anafikiria kukupeleka hata chuo cha ufundi ili kesho na keshokutwa na wewe uajiriwe au ujiajiri lakini kwa nini tunamlipa mabaya?”
“Sikuelewi mpenzi wangu.”

“Unanielewa sana, namaanisha kwamba kuanzia sasa mimi sitaki tena kuendelea kutumia madawa mpaka nakuwa hoi. Nitakapokuwa nazidiwa na ‘arosto’ nitakuwa najidunga lakini kidogo siyo kama wewe unavyotaka.”
“Kwa hiyo unampenda Msuya si ndiyo?”

“Hata kama ungekuwa wewe Diego, mtu anajitahidi kwa hali na mali kutusaidia, kwa nini usimpende,” alisema Arianna, kauli iliyoonesha kumkasirisha mno Diego kwa sababu hakuna jambo ambalo alikuwa hataki kuona linatokea kama Arianna kumpenda Msuya kwani aliamini hatakuwa na chake tena.

Mzozo mkubwa uliendelea kati yao, wakawa wanajibizana huku Diego akitumia maneno ya kuudhi na kumtishia Arianna.

“Usitake kunipangia maisha ya kuishi Diego, naweza kuamua chochote na hakuna mtu wa kunihoji chochote,” alisema Arianna kwa kujiamini, majibizano yakaendelea kiasi cha kumfanya Diego apandwe na jazba kali.

“Nitakubonda sasa hivi, usitake kuniletea mambo ya kishenzi,” alisema Diego lakini Arianna hakutishika chochote, akaendelea kujibizana naye. Kwa hasira Diego akamvaa Arianna mwilini na kuanza kumrushia makonde kama anapigana na mwanaume mwenzake.

Kutokana na kipigo hicho, Arianna alidondoka chini huku damu nyingi zikimtoka puani na mdomoni, Diego akatoka na kurudi chumbani kwake, akamuacha Arianna akiugulia maumivu makali.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Leave A Reply