The House of Favourite Newspapers

The Angel Of Darkness 31

0

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake.  Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anauza kinyemela nyumba aliyoachiwa na wazazi wake na kutorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba wawili hao ni wapenzi.

Hatimaye wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya. Mwanaume huyo anamwambia Arianna wakapime afya zao ili mipango ya ndoa ifuatie, lakini Arianna anatumia ujanja mkubwa na kusababisha wakutane kimwili bila tahadhari yoyote.

Huo unakuwa mwanzo wa safari nyingine kati yao lakini Diego anaanza kumlalamikia Arianna kutokana na wivu.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Sasa Diego, wewe unataka mimi nifanyeje? Ndiyo kwanza tumehamia hapa nyumbani kwa Msuya na tayari umeshaanza kuleta wivu, unafikiri akitushtukia kwamba tuna uhusiano wa kimapenzi itakuwaje?” Arianna aliongea huku akionesha kukasirishwa na kitendo cha Diego kumuonea wivu.

Kijana huyo akaondoka huku wakiwa hawajafikia muafaka wowote. Ilibidi Arianna awe na msimamo mkali kwa sababu kama angeruhusu wivu wa Diego uendelee, maana yake ni kwamba wangeyarudia maisha yao yaleyale ya taabu, jambo ambalo hakuwa tayari kuona linatokea.

Kwa hasira, baada ya kutoka kuzungumza na Arianna, Diego alienda kujifungia chumbani kwake, akiwa hataki kuongea na mtu yeyote, kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa cha Arianna kwani kwa jinsi alivyokuwa akimjua Diego, kwa hatua aliyofikia alikuwa tayari kufanya jambo lolote, hata ikibidi kuuharibu kabisa mpango walioupanga.

Ikabidi amfuate Diego chumbani kwake na kumuomba wakazungumze kwenye bustani za maua ndani ya eneo la nyumba hiyo ya kifahari, baada ya kumbembeleza sana hatimaye Diego alikubali. Arianna akawa anamtaka aachane na mambo ya wivu kwani kama angeendelea hivyo, uwezekano mkubwa ni kwamba Msuya angefahamu ukweli na kusababisha kila kitu kiharibike.

“Kama umenielewa twende tukale ‘mambo yetu’ halafu kila kitu kitakuwa sawa kama kawaida yetu,” alisema Arianna, Deigo akaachia tabasamu hafifu na kuinuka, akaelekea chumbani kwake kuchukua bomba la sindano na Cocaine, Arianna akatangulia chumbani kwake ambapo muda mfupi baadaye Diego alimfuata huku akiwa makini kuhakikisha haonekani na mtu yeyote.

Kama kawaida yao walijidunga madawa ya kulevya kisha wakafanya mapenzi mpaka kila mmoja aliporidhika. Arianna hakujali kwamba muda mfupi uliopita ametoka kukutana na Msuya, alichokuwa anakitaka kwa wakati huo ilikuwa ni kumtuliza Diego kwanza.

Baada ya kuridhika, kwa umakini mkubwa, Diego alitoka bila kuonekana na mtu yeyote na kwenda kujifungia chumbani kwake, akapitiwa na usingizi mzito kutokana na madawa aliyojidunga.

Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa Arianna ambaye uchovu ukichanganya na madawa hayo vilimmaliza kabisa, hakukumbuka hata kuficha bomba la sindano walilotumia kujidungia pamoja na mabaki ya madawa hayo yaliyokuwa mezani, akapitiwa na usingizi mzito.

“Ngo! Ngo! Ngo!” sauti ya mlango uliokuwa unagongwa ndiyo iliyomzindua Arianna kutoka kwenye lindi la usingizi mzito. Akakurupuka kitandani na kutazama saa ya ukutani, hakuyaamini macho yake kugundua kwamba tayari ilikuwa ni saa kumi na mbili za jioni.

Akiwa bado amepigwa na butwaa, macho yake yalitua kwenye bomba la sindano na mabaki ya Cocaine waliyojidunga asubuhi ya siku hiyo na Diego. Harakaharaka akaamka na kuokota lile bomba, akachukua kitambaa na kufuta meza kisha akakimbilia bafuni kwenda kulificha.

Mlango uliendelea kugongwa taratibu lakini kutokana na hali aliyokuwa nayo, Arianna hakutaka kabisa kufungua kwani alijua aliyekuwa anagonga lazima atakuwa ni Msuya na hakutaka amkute akiwa kwenye hali ile.

Harakaharaka akatandika vizuri kitanda ambacho kilikuwa kimevurugika kufuatia shughuli pevu iliyofanyika asubuhi ya siku hiyo kati yake na Diego kisha akakimbilia bafuni, akafungulia ‘bomba la mvua’ na kuanza kujimwagia maji kupunguza uchovu uliosababishwa na dozi ya madawa aliyojidunga asubuhi ya siku hiyo.

“Nipo kuoga nakuja!” Arianna alizungumza kwa sauti ya kichovu kutokea bafuni baada ya kuona mlango unaendelea kugongwa. Aliona hicho ndiyo kisingizio kizuri ambacho kitamfanya Msuya asiingie chumbani kwake kwa muda huo.

Lengo lake lilifanikiwa kwa sababu Msuya aliposikia sauti hiyo ya Arianna kwa mbali, naye alimjibu kwamba akimaliza anahitaji kuonana naye sebuleni. Arianna aliendelea kujimwagia maji ya baridi kwa muda mrefu huku akijisafisha vizuri mwili wake kuondoa dalili zozote zinazoweza kumfanya Msuya amhisi jambo lolote baya.

Baada ya kumaliza, alirudi chumbani kwake ambako alifanya tena usafi, akapulizia ‘air freshner’ chumba kizima na kuipoteza kabisa harufu ya madawa. Alipohakikisha kila kitu kipo katika hali nzuri, alivaa gauni jepesi na kujitanda khanga kwa juu, akatoka mpaka sebuleni ambako alimkuta Msuya akimsubiri kwa shauku.

“Ooh! Umeshindaje malkia wangu?” alisema huku akisimama pale alipokuwa amekaa, akamkumbatia Arianna na kumbusu kwenye paji lake la uso. Kwa kuwa bado uchovu uliosababishwa na madawa aliyotumia haukuwa umeisha, alidanganya kwamba hajashinda vizuri siku hiyo.

“Najisikia vibaya, naona homa bado haijaisha,” alidanganya Arianna.

“Pole sana, ndiyo maana nimeambiwa leo umeshinda kutwa nzima umelala mpaka nikawa na wasiwasi, pole sana mpenzi wangu,” alisema Msuya kwa sauti ya kubembeleza, akaanza kumhimiza kwamba waende hospitalini lakini alimdanganya kwamba amekunywa dawa kwa hiyo asiwe na wasiwasi.

“Kwa kuwa nimeambiwa mchana hujala nimeagiza wakuandalie supu kwanza kisha baadaye ndiyo tutakula chakula cha jioni,” alisema Msuya huku akikaa vizuri pembeni ya Arianna, wakawa wanatazama runinga huku wakipiga stori za hapa na pale.

Muda mfupi baadaye, supu ya kuku wa kienyeji ililetwa na mfanyakazi, ikaandaliwa mezani ambapo Arianna alianza kuifakamia. Moyoni alimshukuru Msuya kwani ni kama alikuwa amejua kinachomsumbua.

Arianna alikuwa na kawaida ya kupoteza hamu ya kula vyakula vigumu baada ya kutumia madawa ya kulevya hivyo supu kilikuwa chakula muafaka kwake kwa muda huo. Alipomaliza, tayari alikuwa amerejewa na nguvu, akashushia na juisi ya matunda iliyotengenezwa vizuri na wafanyakazi wa Msuya.

Waliendelea na mazungumzo ya hapa na pale, Msuya akamwambia anataka kumfanyia ‘sapraizi’ na kumtaka amsubiri hapohapo sebuleni, akapanda ngazi na kuelekea chumbani kwake, muda mfupi baadaye alirejea akiwa na kiboksi kidogo, akamkabidhi Arianna na kumtaka aende kukifungulia akiwa chumbani kwake.

Arianna alitii na kwa sababu tayari alikuwa ameshashiba, hata zile dalili za kulewa zilipungua kabisa, akaelekea chumbani kwake na kwenda kukifungua kiboksi hicho, akapigwa na butwaa kwa alichokiona.

Ndani yake kulikuwa na seti ya mkufu wa shingoni, hereni, pete na kidani, vyote vikiwa vimetengenezwa kwa dhahabu tupu. Arianna alishindwa kujizuia na kujikuta akipiga kelele kwa furaha. Kwa kipindi kirefu maishani mwake alitamani kuvaa dhahabu mwilini mwake lakini alikuwa akishindwa kutokana na gharama kubwa ya vito hivyo.

“Siamini! Siamini kama Msuya ananipenda kiasi hiki,” alisema Arianna huku machozi ya furaha yakimtoka. Akiwa katika hali hiyo, alisikia mlango ukifunguliwa, akageuka kutazama ni nani aliyekuwa akiingia, macho yake yakagongana na Msuya aliyekuwa amejawa na tabasamu pana.

“Ahsante bae (mpenzi)!” alisema Arianna na kumrukia Msuya mwilini, wakakumbatiana na kugandana kama ruba huku machozi ya furaha yakiendelea kumtoka Arianna. Ndani ya muda mfupi tu tangu afahamiane na Msuya, alijikuta akiishi kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Wakiwa wamekumbatiana kwa mahaba, wote walisikia mlango ukigongwa, bila hata kuuliza chochote Arianna akajua lazima atakuwa ni Diego.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye gazeti la Ijumaa Wikienda.

Leave A Reply