The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness – 36

1

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake na sasa maandalizi ya ndoa yao yamepamba moto. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba ni wapenzi.

Wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya na hatimaye, Arianna na Msuya wanafunga ndoa ya kifahari na kuacha gumzo kubwa jijini Arusha, wanasafiri mpaka kwenye Visiwa vya Hawaii kula fungate.

Wakiwa kwenye fungate, Arianna anaanza kusumbuliwa na arosto ya madawa ya kulevya na kufanya kila kinachowezekana kupata unga. Anapoupata anajifungia chumbani na kuanza kujidunga.Je, nini kitafuatia?

SONGA NAYO…

Baada ya kuhangaika kwa dakika kadhaa, hatimaye walifanikiwa kuufungua mlango huo na kumtaka Msuya ndiyo atangulie kuingia ili ajue Arianna yupo kwenye hali gani. Akiwa na wasiwasi mkubwa, Msuya alifungua mlango na kuingia, akawa anaangaza macho huku na kule, ghafla macho yake yakatua kwa Arianna.

“Mungu wangu! Arianna! Arianna!” alisema Msuya huku akionesha kuwa na mshtuko mkubwa.Arianna alikuwa amekaa kwenye sinki la kuogea na kuegamia huku shingo yake ikining’inia kwa nyuma, jambo lililomshtua mno Msuya. Harakaharaka akamsogelea pale alipokuwa ameuchapa usingizi baada ya kujidunga madawa ya kulevya na kuanza kumtingisha kwa nguvu.

“Arianna! Arianna! Umepatwa na nini mpenzi?”
Arianna akiwa kwenye ulimwengu tofauti kabisa, alianza kusikia sauti ya mtu akimuita kwa mbali huku akimtingisha, taratibu akili zake zikaanza kurudi na mwisho akazinduka na kujikuta amekaa kwenye sinki lenye maji, Msuya akiwa pembeni yake.
“Umepatwa na nini mke wangu?”

“Tumbo! Nimeharisha sana mpaka nimeishiwa nguvu,” Arianna alidanganya kwa sauti ya kichovu iliyomfanya Msuya aamini alichokuwa anaambiwa.
“Twende hospitali,” alisema Msuya huku akimbeba Arianna kutoka pale kwenye sinki lakini msichana huyo alitingisha kichwa kuashiria kwamba hakukuwa na haja ya kupelekwa hospitali.

“Nitafutie Glucose na maji mengi ya kunywa, huwa inanitokea hivi,” alisema Arianna, Msuya akatoka naye kule chooni, akawapita wale wahudumu ambao nao walikuwa wakishangaa kilichotokea huku wakiwa tayari kutoa msaada wowote uliokuwa ukihitajika.

“Kanitafutieni glucose na chupa tatu za maji ya kunywa haraka,” alisema Msuya akiwaambia wale wahudumu, akawapa fedha ambapo walitoka harakaharaka kwenda kutekeleza walichokuwa wanaambiwa na mteja wao. Msuya alichukua taulo na kuanza kumkausha Arianna kwani mwili wake wote ulikuwa umelowa kutokana na kukaa kwenye maji kwa muda mrefu, akambadilisha nguo na kumlaza kitandani.

Muda mfupi baadaye, Glucose na maji mengi ya kunywa vililetwa ambapo alifanya kama Arianna alivyokuwa anasema, ikachanganywa kwenye maji na kumpa anywe. Arianna alianza kuonesha kurejewa na nguvu zake, jambo lililomfurahisha sana Msuya.
“Basi inabidi twende hospitali kushughulikia tatizo lako la tumbo, unajua ukiharisha sana unaishiwa na maji mwilini, jambo ambalo ni hatari.”

“Wala usiwe na wasiwasi na mimi Msuya, tukikaa sana pamoja utanielewa, haya ni maradhi ya kawaida tu ambayo huwa yanapona yenyewe,” alisema Arianna kwa sauti ambayo ilikuwa tofauti na ambayo Msuya amezoea kumsikia.

Arianna aliendelea kumnywesha Glucose na baadaye nguvu zake zikawa zimerejea kabisa lakini bado alionekana kutokuwa sawa, hakuwa Arianna yule ambaye Msuya alikuwa akimfahamu lakini mwanaume huyo aliamua kunyamaza.

Siku hiyo ilipita, kesho yake asubuhi wakawahi kuamka kama kawaida yao na kutoka mpaka kwenye bustani nzuri za maua zilizokuwa hotelini hapo kwa ajili ya kupata kifungua kinywa. Muda mfupi baadaye, wahudumu wachangamfu wa hoteli hiyo, walikuwa tayari wameshawaandalia kila kitu kilichokuwa kinahitajika kwa kifungua kinywa.

Msuya na Arianna wakaanza kula taratibu huku wakiendelea kupiga stori za hapa na pale. Tofauti na jana yake, Arianna alionesha kurudi kwenye hali yake ya kawaida, jambo lililomfurahisha sana Msuya.

Wakiwa wanaendelea kula, mara Arianna alijiziba mkono wake mdomoni na kuinuka ghafla, akaanza kukimbilia chumbani kwao. Ilibidi Msuya naye aache kila alichokuwa anakifanya, akawa anamfuata Arianna alikoelekea. Katika hali iliyozidi kumchanganya, alimkuta msichana huyo akiwa amejiinamia kwenye sinki, akitapika mfululizo.
“Mungu wangu, umepatwa na nini tena?”

“Hata siju…i,” alisema Arianna kwa sauti ya kukatakata, Msuya akamsaidia mpaka alipomaliza kutapika, akamnawisha na kumrudisha chumbani walikoanza kuzungumza kuhusu afya ya Arianna.

“Usiwe mbishi Arianna, kwa nini hutaki twende hospitali?”
“Kuna kitu nakihisi, kama kitakuwa siyo chenyewe basi ndiyo tutaenda hospitali.”
“Kitu gani?”

“Naomba uwatume wale wahudumu wakaninunulie kipimo cha mimba.”
“Unasemaaaa? Unataka kuniambia umenasa ujauzito?” alisema Msuya, akiwa ni kama haamini alichokuwa anakisikia. Kutokana na jinsi alivyokuwa na shauku kubwa, harakaharaka alitoka na kwenda kuwafuata wahudumu, akawapa fedha na kuwaagiza kipimo hicho.

Mmoja wao akatoka na kwenda kwenye duka kubwa la madawa lililokuwa mita chache kutoka hotelini hapo, akanunua na kurejea hotelini ambapo alimkuta Msuya akiwa amesimama palepale akimsubiri. Akamkabidhi ambapo alitembea kwa kasi kurudi chumbani alikomkuta Arianna amelala kitandani akimsubiri.

Akakichukua kipimo hicho na kuingia nacho chooni, akatoa haja ndogo na kuiweka kwenye chombo maalum kisha akaingiza kipimo hicho na kusubiri kwa dakika kadhaa. Kama alivyokuwa amehisi, kipimo hicho kilibadilika na kuonesha mistari miwili ya rangi nyekundu kuonesha kwamba alikuwa amenasa ujauzito.

“Nina mimba,” alisema Arianna huku akimtazama Msuya usoni, kauli hiyo ikamfanya mwanaume huyo ainuke pale alipokuwa amekaa na kumnyanyua Arianna juujuu kwa furaha kubwa, akawa anazunguka naye ndani ya chumba hicho huku akiimba nyimbo za furaha.

Hakuna kitu ambacho Msuya alikuwa akikisubiri kwa hamu kama kusikia Arianna amenasa ujauzito, jambo ambalo hatimaye lilikuwa limetimia. Siku nzima, Msuya alishinda akiwa anachekacheka mwenyewe kama mwendawazimu, mapenzi kwa Arianna yakazidi kuongezeka maradufu huku akimuahidi mambo kedekede msichana huyo, ikiwa ni pamoja na kumrithisha vitega uchumi vingi.

“Nataka hata nikifa, wewe na mwanangu utakayemzaa msipate shida hata kidogo, nitakupa chochote unachokitaka,” alisema Msuya akiwa analichezea tumbo la Arianna kwa mahaba makubwa.

Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa Arianna. Ni kweli naye alikuwa anapenda kupata ujauzito wa Msuya lakini kila alipokuwa akijaribu kuvuta kumbukumbu na kuhesabu, alikuwa na wasiwasi mkubwa kwamba ujauzito huo ni wa Msuya au ni wa Diego.

kabaki njia panda huku akiendelea kuvuta kumbukumbu kujaribu kukumbuka alikutana kimwili na nani alipokuwa kwenye siku zake za hatari.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

1 Comment
  1. leonia says

    Duuh ni nzuri sana

Leave A Reply