The angel of darkness -46

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Mfanyabiashara huyo anamuoa Arianna na kumchukua na Diego pia kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.

Siku chache baada ya ndoa, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito lakini anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego, jambo linalomchanganya sana.

Anachokifanya ni kupanga mikakati na Diego ya kutoroka huku wakijifanya wamevamiwa na yeye kutekwa. Anachukua madini, fedha na bastola kisha kuondoka zake huku akipanga kukutana na Diego nchini Kenya. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Arianna hakujiamini, japokuwa alivuka salama katika mpaka wa Namanga na kuingia nchini Kenya lakini aliona kwamba muda wowote ule angeweza kukamatwa na polisi.

Huko hakukuwa na amani hata kidogo, kila kona kulikuwa na vitisho, Wasomali ambao bado waliendelea kuwang’ang’aniza wanajeshi wa Kenya kuondoka nchini mwao waliendelea kulisumbua taifa hilo kubwa Afrika Mashariki.

Watu wengi walitekwa, vyuo vilivamiwa na watu wengine kuuawa, serikali ya nchi hiyo ilichanganyikiwa, walijitahidi kuweka ulinzi kila kona lakini bado hali ya hatari iliendelea kuliandamana taifa hilo.
Mipakani ulinzi uliimarishwa kila kona, kitendo cha Arianna kufanikiwa kuvuka mpakani hapo huku akiwa na bunduki, kiasi kikubwa cha fedha pamoja na madini ya tanzanite, kwake ilionekana kuwa bahati kubwa mno.

Wakati huo safari yake ilikuwa ni kwenda jijini Nairobi ambapo huko angeishi na kufanya mambo yake na mwisho wa siku kupotea kabisa kwenye macho ya bwana Msuya, ila pamoja na hayo yote, mtu aliyekisumbua sana kichwa chake alikuwa Diego.

Walipanga vizuri kwamba mara baada ya yeye kufanikiwa kuondoka Tanzania basi wakutane Lianai, mji mmoja uliokuwa nchini Kenya. Kutoka hapo Namanga mpaka Lianai ilikuwa ni zaidi ya kilometa mia mbili ila kitu kilichomchosha ni kwamba hakujua kama Diego aliondoka nchini Tanzania au la.

“Cha kwanza nifike huko halafu nitajua nini cha kufanya,” alijisemea huku akiingia ndani ya basi.
Safari ya kuelekea Nairobi ikaanza. Ndani ya basi kulikuwa na abiria zaidi ya mia mbili huku idadi kubwa ya abiria waliokuwepo ndani humo wakiwa Watanzania ambao walikuwa wakielekea Nairobi kwa ajili ya biashara zao.

Katika kiti alichokuwepo, Arianna alikuwa kimya, hakutaka kuzungumza na mtu yeyote yule na muda mwingi alionekana kuwa na mawazo tele. Macho yake yalikuwa yakiangalia nje, moyoni mwake aliendelea kumuomba Mungu afike salama huko na kuanza kumsubiri Diego ambapo hakujua angetumia siku ngapi mpaka kufika.

Kutoka hapo Namanga mpaka Lianai basi lilichukua saa mbili, likafika na hivyo Arianna kuteremka. Kulikuwa na idadi kubwa mahali hapo, wengi wao walikuwa wabeba mizigo ambapo walimsogelea na kumuomba kulibeba lile begi lililokuwa na madini lakini Arianna hakutaka kumruhusu mtu yeyote yule, alilishikilia vizuri.

Alichokifanya ni kuulizia mahali kulipokuwa na hoteli ambapo angekaa hapo kwa kipindi fulani akimsubiri Diego kabla ya kuendelea na safari ya kuelekea Nairobi. Akaelekeza mahali hote ilipo na kuanza kwenda huko.

“Nikusaidieje?’ aliuliza dada wa hapo mapokezi kwa Kiswahili chake cha Kenya.
“Ninahitaji chumba,” alijibu Arianna.
“Shilingi elfu kumi kwa siku…”
“Hakuna tatizo!”

Baada ya kukabidhiwa ufunguo, akaanza kuelekea katika chumba hicho. Bado mawazo hayakumtoka, alipiga hatua kuelekea chumbani huko ambapo baada ya kufika, akajitupa kitandani nha kupumzika.
Kwa kuwa ilikuwa ni asubuhi tayari, hakulala sana, saa sita mchana akaamka na kutoka nje huku lengo lake likiwa ni kutafuta chakula kwani kile kilichokuwa kikipikwa hotelini hapo, hakukipenda kutokana na hali ya ujauzito aliokuwa nao.

Kutokana na hali aliyokuwa nayo, hakutaka kutoka na yale madini, alihakikisha anayaficha chumbani humo, yeye akatoka na bastola ndogo ambayo aliiweka kiunoni kisiri kwa ajili ya ulinzi wake binafsi kutokana na matukio mengi ya mauaji na wanawake kubakwa yaliyokuwa yakitokea huko.

“Wewe dada uje usogee kwa hapa,” alisikika mwanaume mmoja aliyevalia sare za kipolisi, alikuwa na mwenzake, chini alivalia bukta na soksi ndefu kana kwamba alikuwa akienda kucheza mpira.

Arianna akashtuka, moyo wake ulijawa hofu kubwa, alipowaangalia polisi wale, sura zao tu zilionyesha ni watu wenye roho mbaya ambao hawakuwa na utani hata kidogo. Hapo alikuwa amebakiza kama hatua kumi na tano kabla ya kukifikia kibanda kilichokuwa kikipigwa wali. Akawafuata.
“Wewe ni Mtanzania?” aliuliza polisi mmoja.
“Ndiyo!”

“Iko wapi kibali yako?”
“Kibali gani?”
“Karatasi yako ya kuishi huku kwa Kenya?” alijibu polisi mwingine huku wakimwangalia msichana huyo usoni.

“Kibali?” aliuliza huku akijifanya hajasikia.
Polisi wale hawakuonekana kuwa na utani hata kidogo, kitendo cha Arianna kujifanya hajasikia chochote na kuuliza kwao kilionekana kuwa kama dharau, hapohapo wakamsogelea na kuanza kumpekua bila hata ridhaa yake.

“Kuna nini?” aliuliza huku akiwa na wasiwasi.
Hakutaka kupekuliwa, alijua fika kwamba alibeba bunduki hivyo kitendo cha polisi wale kuanza kumpekua kikamfanya kuwa na hofu ya kukutwa na bastola ile.

Akajitahidi kukataa kupekuliwa lakini akawa amekwishachelewa kwani sehemu ya kwanza kabisa polisi kumpekua ilikuwa ni kiunoni.

“Hii bunduki ya nani?” aliuliza polisi mmoja.
“Wewe ni shabaab? Umetumwa na shabaab?” alihoji polisi mwingine, hata kabla Arianna hajajibu maswali hayo, akabebwa mzobemzobe na kuanza kupelekwa katika kituo cha polisi.

Watu wote waliokuwa pembeni wakabaki wakimwangalia, walimuonea huruma ila kitendo kile kilichokuwa kikiendelea kililifanya tukio hilo kuwa kama filamu fulani ya mapigano.

Japokuwa Arianna alikuwa akipiga kelele aachwe lakini hakukuwa na aliyemuelewa, hivyohivyo tena huku wakiwa wamembeba, akapelekwa katika kituo cha polisi ambapo humo ndani kulikuwa na kundi la Wasomali, kwa kuwa hesabu za harakaharaka walikuwa kama ishirini, wanaume kwa wanawake, hofu ikamjaa, akajikuta akiwa njiani kupewa kesi ya ugaidi.

Kijasho kilimtoka, hakuwa na tumaini la kutoka salama, kilichomuuma zaidi ni yale madini na fedha alizoziacha kule hotelini.

Je, nini kitaendelea? Usikose kusoma siku ya Ijumaa katika Gazeti la Ijumaa

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

 

Loading...

Toa comment