The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness -48

1

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Mfanyabiashara huyo anamuoa Arianna na kumchukua na Diego pia kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.

Siku chache baada ya ndoa, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito lakini anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego, jambo linalomchanganya sana.

Anachokifanya ni kupanga mikakati na Diego ya kutoroka huku wakijifanya wamevamiwa na yeye kutekwa. Anachukua madini, fedha na bastola kisha kuondoka zake huku akipanga kukutana na Diego nchini Kenya. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Kituo cha polisi cha Lienai kilikuwa kikiteketezwa kwa moto, watu wote waliokuwa nje ya kituo kile, walijificha mbali kwa kuogopa kuonekana na magaidi hao.

Hakukuwa na mtu aliyetoka pale alipojificha kwani milio ya risasi iliyokuwa ikiendelea kusikika ilimtisha kila mmoja. Miili ya polisi ilitapakaa, kila mtu alionekana kujawa na hofu, hali iliyokuwa ikionekana mahali hapo, ilikuwa ni kama Baghdad au sehemu yoyote iliyokuwa na mapigano ya mara kwa mara.

Ndani ya kituo cha polisi kile, Arianna alibaki akitetemeka, magaidi wale ambao waliondoka dakika chache zilizopita, hawakujali, mtu ambaye hakuwa Msomali, hawakuhusika naye, hawakuja hapo kuwachukua watu ambao hawakuwa wao, walifika kwa ajili ya Wasomali ambao tayari waliwachukua na kuondoka nao.

Ndani ya selo ile, Arianna alibaki na wanaume wengine wa Kenya. Kila mmoja alionekana kujawa na hofu kutokana na moto ule ambao ulizidi kukiteketeza kituo kile, mbaya zaidi, hata milango ya ya chuma ya selo zote zilizokuwa ndani ya kituo hicho ilifungwa.

“Ni lazima tuondoke, ni lazima tuvunje geti,” alisema Arianna huku akiwaangalia wanaume waliokuwa ndani ya chumba kile.
“Tutaweza?”

“Yaani nyie wanaume wazima mnashindwa kufanya jambo? Sasa mlizaliwa na kuwa wanaume ili iweje? Si bora mngezaliwa na kuwa wanawake tu!” alisema Arianna huku akionekana kukerwa na wanaume hao ambao wala hawakuonekana kujishughulisha, wakati kituo hicho kilivyokuwa kikiteketea, hakukuwa na aliyekuwa na mpango wa kutoroka, ndiyo kwanza walikuwa wakisali sala zao za mwisho.

“Kubaki humu na kufa, ni upumbavu…” alisema Arianna.
Alichokifanya ni kuufuata mlango wa chuma na kuushika, ulifungwa kwa nje na hakukuwa na dalili zozote za kuupata ufunguo ambao ulikuwa huko kaunta, piga ua ilikuwa ni lazima mlango huo wauvunje, kama wasingefanya hivyo basi hiyo ilimaanisha kwamba walikuwa tayari kufa humo ndani.

Wanaume wale wa Kikenya hawakutaka kutulia, tayari mwanamke waliyekuwa naye humo alionekana kuwa na akili kuliko wao, kilichohitaji ni kuungana naye na kuuvunja mlango huo kisha kuondoka ndani ya kituo hicho.

Mlango ulikuwa imara na kama wasingetumia akili ya ziada basi wasingefanikiwa. Moto haukupungua, ulizidi kukiteketeza kituo kile, ulianzia kaunta na sasa ukaanza kwenda kwenye selo hizo, watuhumiwa wote waliokuwemo ndani ya selo hizo, wakaanza kupiga kelele.

“Tunapiga teke geti mpaka ling’oke…” alisema Arianna, alionekana kuchanganyikiwa.
“Tutaweza?” aliuliza mwanaume yuleyule wa mara ya kwanza.

“Hivi wewe mwanaume gani sasa? Mimi mwanamke nasema tunavunja, wewe mwanaume unasema hauwezi, kweli wewe ni mwanaume kweli au tomboy?” aliuliza Arianna huku akimaanisha kama alikuwa mwanaume au mwanaume mwenye mambo ya kike.

“Basi sawa dada…” alisema mwanaume huyo.
Hakukuwa na kilichoendelea zaidi ya kuanza kuuvunja mlango huo. Wanaume saba wenye nguvu wakaanza kuupiga mlango ule mateke. Ilikuwa ni lazima kufanya hivyo kwani kama wasingefanya hivyo ilikuwa ni lazima kuteketezwa na moto ndani ya chumba hicho na kufa.

Kwa Arianna alionekana kuwa na nguvu zaidi, kilichofikirika moyoni mwake ni utajiri ambao aliuacha hotelini. Ilikuwa ni lazima atoke ndani ya chumba hicho kwani vinginevyo, ule utajiri aliuoacha kule hotelini ungepotelea mikononi mwa mtu mwingine.

“Unavujika….tuendeleeni,” alisema Arianna na hivyo kuendelea kuupiga zaidi.
Baada ya dakika tano, wakaona vyuma vilivyoshikilia ukuta vikianza kung’oka. Hawakutaka kuacha, walipiga zaidi na hatimaye mlango ule kung’oka kabisa. Hakukuwa na cha kufanya zaidi ya kugombania kutoka.

Wote wakatoka ndani, hakukuwa na mtu aliyepitia kaunta kutokana na moto uliokuwa ukiendelea kuwaka, walichokifanya ni kupitia mlango wa nyuma. Arianna hakutaka kubaki, kama walivyofanya wale wanaume, naye akatoka kupitia mlango wa nyuma.

Bado nje hakukuwa na amani hata kidogo, kila mtu alikuwa akikimbia huku na kule, japokuwa hakukuwa na magaidi wale lakini wote waliona kuwa bado magaidi walikuwa mahali hapo, hivyo wakaendelea kujificha zaidi.

Arianna akaelekea barabarani, akaunganisha na kuelekea katika hoteli ile aliyofikia. Njiani, alikuwa akihema kama mbwa kwani hakutembea zaidi ya kukimbia tu, alichoka lakini hakutaka kusimama hata kidogo.

Hakuchukua muda mrefu, akafika hapo hotelini. Mlinzi alivyomuona, jinsi alivyokuwa mchafumchafu, akamzuia.“Kuna nini?” aliuliza Arianna huku akionekana kukasirika kuzuiwa hapo getini.

“Unaendaga wapi?” aliuliza mlinzi yule.
“Nakwenda ndani….mimi ni mteja, nilichukua chumba…”
“Haupo serious, hakuna mteja aliyeingia kwa hoteli akiwa kama wewe, wewe ni chokoraa…” alisema mlinzi huyo huku akimwangalia Arianna, kwa jinsi moshi ulivyomchakaza, mlinzi hakutaka kuamini kama kulikuwa na mtu kama huyo ambaye angekuwa na uwezo wa kupanga ndani ya hoteli hiyo ya gharama.
****
“Nisikilizenii kwanza, mke wangu yupo wapi?” aliuliza mzee Msuya.
“Mzee, subiri kwanza…”
Japokuwa polisi walijitahidi kumtuliza mzee huyo lakini hakutaka kutulia. Alichanganyikiwa mno, kitendo cha kuambiwa kwamba mkewe alitekwa, tena akiwa na mimba yake kilimchanganya mno.

Polisi walijitahidii kumpoza, hakupozeka, hakutaka kubaki mahali hapo, akaondoka na kuelekea nyumbani kwake. Kichwani mwake lilimjia wazo moja tu kwamba ni lazima achapishe picha nyingi za Arianna na kuzibandika mitaani, mbali na kuzibandika, pia aweke zawadi ya shilingi milioni nne kwa mtu yeyote atakayefanikisha kupatikana kwake.

Hiyo ilikuwa nafasi pekee, baada ya picha hizo kubandikwa, watu hawakutaka kutulia, wakaanza kumtafuta msichana huyo.
Wanawake waliovaa nikabu, wakatakiwa kuvua kwa muda kwani kulikuwa na mtu muhimu aliyekuwa akitafutwa. Kila mmoja alizitaka fedha hizo na ndiyo maana walikuwa na juhudi kubwa kumtafuta.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Ijumaa.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO, BOFYA HAPA ===>https://www.facebook.com/shigongotz/

1 Comment
  1. Prince'kabagala says

    ariana rudi kwa mmeo, unaoufanya ni ujinga huo.

Leave A Reply