The House of Favourite Newspapers

The Angels of Darkness – 60

1

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.

Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.

Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Baadaye Mashango anafariki dunia baada ya kugongwa na gari na Brianna anachukuliwa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge. Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa Arianna na kumchukua pia Diego kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.

Baadaye Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka. Wanatengeneza tukio feki la ujambazi ili ionekane wamevamiwa na Arianna kutekwa na majambazi. Licha ya misukosuko anayokutana nayo, msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya bila mtu yeyote kujua kwamba bado yupo hai.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Saa kumi na mbili kamili za asubuhi, safari ya kuelekea Mandera ilianza, Basi la Nyayo Express likatoka stendi na kuanza kuchanja mbuga kuelekea Kaskazini mwa Kenya.
Njia nzima Arianna alikuwa akimuomba Mungu wake afike salama kwani hali ilishachafuka na uwezekano wa kukamatwa tena na kujikuta akiishia kwenye mikono ya polisi wa Kenya ulikuwa mkubwa sana.

Basi likawa linachanja mbuga kwa kasi kubwa huku mara kwa mara Arianna akigeuka nyuma kutazama kama hakukuwa na gari la polisi lililokuwa likiwafuatilia.

“Thanks Almighty im going to be free again! Im going to start a new page of my life,” (Ahsante Mungu naenda kuwa huru tena. Naenda kufungua ukurasa mpya wa maisha yangu) alijisemea Arianna wakati gari likizidi kuchanja mbunga kuelekea Mandera.

***
Matangazo yenye sura ya Arianna yaliendelea kubandikwa kwa wingi kwenye mitaa ya miji mbalimbali nchini Kenya yakiwa na maelezo kwamba yeyote atakayefanikisha kupatikana kwa msichana huyo, atapewa zawadi nono ya shilingi za Kenya 50,000, sawa na karibu shilingi milioni kumi za Kitanzania.

“Ile advert kwa stima inaonesha ni deal ya chapaa mingi, lazima tuichangamkie,” mwanaume mmoja aliwaambia wenzake akiwahamasisha nao wakasome tangazo lililokuwa limebandikwa kwenye nguzo ya umeme kumhusu Arianna, wote wakaenda kuizunguka nguzo hiyo na kuanza kusoma kilichoandikwa.
Ndani ya muda mfupi tu, Arianna alikuwa gumzo kwenye mitaa yote ya Jiji la Nairobi na maeneo mengine ukiwemo Mji wa Mombasa. Vijana wengi wakaacha kila walichokuwa wanakifanya na kuingia mitaani kumsaka Arianna.
***
Mathare, Nairobi, Kenya
Maisha aliyokuwa anaishi msichana Brianna, pacha wa Arianna na familia ya mzee Njoroge, kwenye mtaa wa watu maskini wa Mathare, nje kidogo ya Jiji la Nairobi, yalimfanya aridhike kabisa. Japokuwa yalikuwa maisha ya hali ya chini, aliridhika kwa kila kitu kutokana na jinsi familia hiyo ilivyokuwa inamlea.

Walichokula watoto wa mzee Njoroge ndicho alichokula Brianna, walichovaa watoto wa familia hiyo ndicho alichovaa Brianna, kwa ufupi usingeweza kuamini kwamba binti huyo hakuwa mtoto wa Njoroge wa kumzaa. Alipewa huduma zote kwa usawa na wenzake.

Kilichomtofautisha na wenzake, ilikuwa ni uzuri wake wa asili ambao haukuweza kujificha. Kila aliyemuona msichana huyo, hakuacha kumsifia kutokana na jinsi alivyokuwa ameumbika.

Vijana wengi walikuwa wakishinda kutwa nzima wakirandaranda jirani na nyumba ya mzee Njoroge wakimvizia Brianna ili japo wapate nafasi ya kuwa naye karibu lakini haikuwa rahisi. Brianna hakuwa msichana wa kuzurura ovyo mitaani kama walivyokuwa wasichana wengi wa mtaa huo wa watu maskini.

Baada ya kuhitimu elimu ya msingi, alishindwa kuendelea na masomo ya sekondari kutokana na familia hiyo kukosa fedha za kumuendeleza. Muda mwingi akawa anashinda nyumbani. Mara chache alizokuwa anatoka, alikuwa akienda kusaidiana na mke wa Njoroge na wanaye kwenda kununua bidhaa za kuuza kwenye genge lao dogo lililokuwa jirani na nyumbani kwao.

Pia alikuwa akitoka kila Jumapili kwenda kanisani pamoja na wanafamilia wote kwa sababu mzee Njoroge alikuwa akiwalea kwa misingi ya kidini.

Asubuhi moja akiwa na mke wa Njoroge ambaye alikuwa akimuita mama, wakiwa na vikapu vilivyosheheni mbogamboga na matunda kwa ajili ya kuuza gengeni, walishangaa kundi la vijana kama saba hivi wakiwavamia na kuwazunguka, wakawa wanashangaa wakiwa hawaelewi kilichotokea.

“Ni yeye! Ni yeye! Mimi ndiyo wa kwanza kumuona,” alisema kijana mmoja kati ya wale saba huku akiwa ameshika tangazo lililokuwa likionesha kwamba msichana huyo anatafutwa.

Wakiwa bado wamepigwa na butwaa, Brianna na mama yake waliweka mizigo yao chini, wakawa wanataka kueleweshwa nini kilichotokea. Ilibidi mmoja kati ya wale vijana aanze kuwafafanulia kwamba msichana huyo alikuwa anatafutwa na dau nono lilitangazwa kwa yeyote atakayefanikisha kupatikana kwake.

“Kwani amefanya nini mwanangu mpaka atafutwe kiasi hiki?” alisema mama yake Brianna huku naye akilitazama kwa umakini lile tangazo.

“Hee! Mbona sijawahi kupiga picha kama hii?” Brianna alisema huku naye akionesha kupatwa na mshtuko mkubwa. Sura ya mtu aliyekuwa kwenye tangazo hilo, ilikuwa ikifanana na yake kwa asilimia kubwa ingawa mwenyewe alitambua kwamba hakuwa yeye.

“Kwanza huyu siyo mimi, isitoshe mimi siitwi Arianna,” alisema Brianna na kusababisha kila mtu amshangae. Hata mama yake naye alionesha kumshangaa, akahisi labda alikuwa na hofu kubwa moyoni ndiyo maana alizungumza hivyo. Umati mkubwa watu uliendelea kufurika eneo hilo huku kila mtu aking’ang’ania kwamba aliyekuwa akitafutwa ni yeye, mwenyewe akawa anatumia nguvu kubwa kukanusha.

Harakaharaka simu zilipigwa kupitia kwenye namba iliyokuwa kwenye tangazo hilo ambayo ilikuwa ni ya Diego. Kwa kuwa kijana huyo alikuwa jijini Nairobi akiendelea na kazi ya kumtafuta Arianna, alipopigiwa simu tu, haraka sana alifika eneo la tukio akiwa ameongozana na polisi watatu wa Kenya. Wakapenya kwenye umati mkubwa wa watu waliokuwa wamefurika eneo hilo na kwenda mpaka pale Brianna na mama yake walipokuwa wamesimama, wakiwa wamezungukwa na watu wengi.

“Arianna! Ni wewe? Ooh! Ahsante Mungu uko salama,” alisema Diego kwa sauti ya juu huku akiinua mikono kama ishara ya kumshukuru Mungu wake, akamsogelea na kumkumbatia Brianna akiamini kwa asilimia mia moja kwamba aliyekuwa mbele yake ni Arianna.

Msichana huyo alibaki amepigwa na butwaa, akiwa haelewi kinachoendelea. Sura ya Diego ilikuwa ngeni kabisa kwake, hakuwahi kumuona hata mara moja na alibaki anashangaa kwa nini amuite kwa jina la Arianna wakati yeye jina lake ni Brianna.

“Mbona unashangaa Arianna?” Diego alisema baada ya kuona hali isiyo ya kawaida ikimtokea msichana huyo, huku akitetemeka kwa hofu.
“Mimi siyo Arianna.”

“Inawezekana matukio yaliyomtokea yamemfanya awe kwenye hali hii, tuondoke naye mpaka sehemu tulivu,” alisema Diego, wazo lililoungwa mkono na wale askari, wakawatawanya watu waliokuwa wanazidi kufurika eneo hilo na kusogea na msichana huyo mpaka kwenye gari walilokuja nalo, lililokuwa mita kadhaa kutoka pale walipokuwa.

Yule mwanaume aliyekuwa wa kwanza kutoa taarifa juu ya kuonekana kwa msichana huyo, naye alichukuliwa kwa ajili ya taratibu za kumkabidhi zawadi yake, wakapanda kwenye gari la polisi na kutaka kuondoka lakini mke wa Njoroge hakukubali kabisa msichana huyo aondoke peke yake, akashinikiza na yeye achukuliwe kwa sababu hakuwa anaelewa kilichotokea.

Dakika kadhaa baadaye, gari walilopanda lilipaki kwenye hoteli kubwa ya Moven Pick Nairobi, wakateremka na Diego akawaongoza mpaka kwenye bustani nzuri zilizokuwa nje ya hoteli hiyo, wakakaa huku akiwa makini kumtazama yule msichana ambaye muda wote alikuwa akishangaashangaa kila kitu.

“Nataka mniambie binti yangu amefanya nini mpaka mumtafute kwa nguvu namna hii kama mkora!” alisema mke wa Njoroge, Diego akawa anamshangaa kwa nini amuite yule msichana binti yake wakati aliamini hamfahamu.

Mazungumzo yaliendelea lakini yalitawaliwa na hali ya kutoelewana, huyu anazungumza hivi huyu anazungumza kile, ikawa vurumai. Ilibidi Diego aombe kuzungumza na msichana huyo pembeni wakiwa wawili tu.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

1 Comment
  1. Otto Kabagala says

    briana binti mstaarabu, bahati yake ndiyo sasa.

Leave A Reply