The House of Favourite Newspapers

The Begining of My End (Mwanzo wa mwisho wangu)

3

Kijana mdogo, Benjamin Semzaba au maarufu zaidi kama Ben, anafikishwa mbele ya mkono wa sheria akikabiliwa na kesi nzito ya mauaji. Baada ya kunguruma kwa kipindi kirefu, hatimaye kesi iliyokuwa inamkabili inaelekea kufika mwisho na hukumu kutolewa.

Ushahidi wote umeshakamilika na hakuna shaka kwamba Ben ndiye aliyeua kwani ukiachilia mbali ushahidi huo, yeye mwenyewe mara kwa mara amekuwa akikiri kwa kinywa chake kufanya mauaji hayo na kilichokuwa kikisubiriwa ilikuwa ni hukumu tu.

Wakati kila mtu akiamini kwamba Ben ameua, Jordan Rwechungura, wakili aliyekuwa akimtetea katika kesi hiyo ambaye ukiachilia mbali kazi yake pia alikuwa rafiki mkubwa wa Ben, waliyecheza pamoja tangu wakiwa watoto wadogo, anakuwa mgumu kuamini kwamba ni kweli rafiki yake huyo ameua.

Historia ya makuzi ya Ben, inamfanya Jordan ahisi kwamba Ben hajaua ila ameamua kukubali kwa sababu ambazo yeye mwenyewe ndiye anayezijua. Jitihada zake za kutaka kuufahamu ukweli ili amnasue rafiki yake huyo kutoka kwenye kitanzi kilichokuwa kinamsubiri, zinagonga mwamba kutokana na Ben kukataa kutoa ushirikiano, muda wote aking’ang’ania kwamba ni yeye ndiye aliyeua.

Hatimaye siku ya hukumu inawadia, Ben akiwa amedhoofika sana na kubadilika kutokana na mateso ya gerezani, anaingizwa mahakamani huku mamia ya watu, wakiwemo waandishi wengi wa habari wakifuatilia kwa umakini kesi hiyo iliyogusa hisia za watu wengi.
Je, nini kitafuatia? Ben atapewa hukumu gani?
SONGA NAYO…

Baada ya kuingizwa kwenye jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Ben na wenzake walipelekwa kwenye vyumba maalum kusubiria muda wa kila mmoja kupandishwa kizimbani.
Muda wote Ben alikuwa kimya kabisa huku akililazimisha tabasamu hafifu kwenye uso wake, alitamani kila kitu kifanyike harakaharaka ili hatimaye asomewe hukumu yake. Alishasota sana mahabusu, safari za kwenda na kurudi mahakamani zilishamchosha na sasa alikuwa anatamani jambo moja tu litokee; asomewe hukumu yake, basi!

“Benjamin Semzaba!” sauti ya askari magereza ilisikika, Ben akaitikia na kusimama pale alipokuwa amekaa, mikononi akiwa amefungwa pingu kwa mbele, akatolewa mpaka kwenye korido huku askari wawili wakimlinda, wakaondoka naye mwenyewe akiamini kwamba muda wa kesi yake kusikilizwa ulikuwa umewadia lakini akashangaa kuona anaingizwa kwenye chumba cha mwendesha mashtaka.

“Ben! Nimeomba dakika chache tuzungumze kwa mara ya mwisho,” Jordan, aliyekuwa amevalia kiuanasheria, macho yake yakiwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu kuonesha kwamba alikuwa analia, alimwambia Ben kwa sauti ya chini na kumuomba askari magereza amfungue pingu.
“Ooh! Ahsante Jordan kwa namna unavyoonesha kunijali.”
“Usijali, wewe ni rafiki yangu Ben! Karibu ukae,” alisema Jordan huku akimuonesha sehemu ya kukaa, Ben akakaa na kushusha pumzi ndefu. Wakaanza kuzungumza ambapo kama ilivyokuwa muda mfupi uliopita, Jordan alirudia kumsihi amueleze ukweli kama ni yeye ndiye aliyeua.

Bado majibu ya Ben yalikuwa yaleyale, aliendelea kusisitiza kwamba ni yeye ndiye aliyeua. Wakaendelea kuzungumza mpaka muda aliopangiwa ulipoisha ambapo wale askari magereza waliingia na kumchukua Ben, wakamfunga tena pingu na kumrudisha kwenye chumba alichowepo awali.
Dakika chache baadaye, walianza kuitwa tena kwa ajili ya kwenda kwenye ukumbi wa kusikilizia kesi, Ben akawa wa kwanza kuitwa. Alitolewa chini ya ulinzi mkali na kupelekwa moja kwa moja kwenye ukumbi wa mahakama.

Mlango wa chumba cha mahakama ulifunguliwa, Ben alipoingia tu, mwanga wa kamera nyingi ulimmulika lakini mwenyewe hakujali, kama kawaida yake akawa analilazimisha tabasamu hafifu kwenye uso wake. Wale askari walimuongoza mpaka kizimbani, akafunguliwa pingu na kuoneshwa sehemu ya kusimama.

Mwanga wa kamera nyingi uliendelea kummulika, akabaki amepigwa na butwaa kwa jinsi mahakama ilivyokuwa imefurika siku hiyo. Minong’ono iliendelea kutawala mahakamani hapo, kila mtu akizungumza lake lakini mwenyewe hakujali chochote.
Kwa macho yaliyokosa matumaini, alianza kuwatazama watu waliokuwa wamefurika mahakamani hapo. Macho yake yalitua kwa rafiki yake wa siku nyingi na wakili aliyekuwa anamtetea kwenye kesi hiyo, Jordan Rwechungura. Macho yao yakagongana na kwa sekunde kadhaa walibaki wakitazamana.
Baadaye Jordan alimpa ishara Ben, harakaharaka akageukia kule alikomwelekeza kwa ishara, macho yake yakatua kwa mkewe aliyekuwa amekaa siti ya mbele kabisa, mkononi akiwa amembeba mtoto mdogo ambaye hakuwa akielewa chochote kilichokuwa kinaendelea.

Macho ya Ben na mkewe, Gladness yaligongana, wakatazamana huku uso wa mwanamke huyo ukiwa umelowa kwa machozi. Kutokana na jinsi alivyokuwa anajisikia ndani ya moyo wake, Gladness alishindwa kuendelea kutazamana na mumewe, akajiinamia chini huku kilio cha kwikwi kikisikika.
Machozi mengi yaliyokuwa yakimtoka, yalikuwa yakichuruzika na kumlowanisha mwanaye lakini mwenyewe hakujali. Akawa anaendelea kulia kwa uchungu huku akitamka maneno ambayo hakuna aliyekuwa anayaelewa.

Japokuwa Ben alijiapiza kwamba kamwe hatalia kwa kilichotokea, uzalendo ulimshinda na kujikuta akianza kulengwalengwa na machozi huku donge kubwa likiwa limemkaba shingoni, muda mfupi baadaye michirizi ya machozi ikaanza kuonekana kwenye uso wake.
“Kooooorti!” sauti nzito ya askari aliyekuwa anamaanisha hakimu anakaribia kuingia, ndiyo iliyomzindua Ben kutoka kwenye dimbwi la mawazo machungu alilokuwa amezama ndani yake. Watu wote wakatulia na waandishi wa habari waliokuwa wakiendelea kumpiga picha Ben sambamba na mkewe pamoja na mwanaye, nao walitulia.

Sheria za mahakama zilikuwa zikizuia kufanyika kwa shughuli zozote baada ya hakimu kuingia mahakamani na yeyote ambaye angebainika kuvunja sheria hizo, angeweza kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Ukumbi mzima wa mahakama ulikuwa kimya kabisa, watu wote walitulia, hakukuwa na kelele zozote zilisosikika zaidi ya vishindo vya jaji na jopo lake ambao waliingia na kwenda kuketi sehemu yao.

Muda mfupi baadaye, taratibu za kesi zilianza kufuatwa kama kawaida. Mwendesha mashtaka wa serikali, Bonaventure Kilasi, alisimama na kuanza kumsomea mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Ben. Watu wote walikuwa kimya kabisa wakifuatilia kwa makini kila kilichokuwa kinaendelea.
Waandishi wa habari nao walikuwa bize kuandika kwenye ‘notebook’ zao kila kilichokuwa kinaelezwa. Baada ya mwendesha mashtaka wa serikali kumaliza kusoma mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Ben, jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Eustas Twalipo alianza kusoma mwenendo wa kesi hiyo, ukiwemo utetezi wa mshtakiwa.

Baada ya kuzungumza kwa dakika kadhaa mfululizo, uliwadia muda ambao watu wote walikuwa wakisubiri kwa shauku kubwa. Hakimu akakohoa kidogo ili kuweka sawa koo lake, akavua miwani yake na kuifuta vumbi kisha akaivaa tena na kumtazama Ben aliyekuwa ametulia kizimbani.
Akaendelea: “Baada ya kusikiliza mwenendo mzima wa kesi inayokukabili, mahakama imekukuta na hatia ya kuua kwa kukusudia, kinyume na sheria ya makosa ya jinai ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1977. Kabla sijasoma hukumu, je, ndugu mshtakiwa una chochote cha kujitetea?”

Watu wote waliokuwa mahakamani, walimgeukia Ben pale kizimbani alipokuwa amesimama, kila mtu akiwa na shauku kubwa ya kumsikia atasema nini.
Je, nini kitafuatia? Ben atasema nini? Usikose Jumamosi kwenye Gazeti la Risasi Jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

3 Comments
  1. Erick Abdallah says

    Nzuri Sana

  2. Aman Norbety says

    Sina hakimu

  3. habibu mshauri says

    naomba sehemu ya kwanza mpk ilipoishia th begnning of my end kwny email address yng

Leave A Reply