The World You Left Behind-21

Ajali mbaya na ya kutisha inatokea kwenye Makutano ya Barabara za Morogoro na Msimbazi, katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Gari la Mheshimiwa Abbas Magesa, Range Rover Evoque linagongwa na lori la mafuta na kuteketea kabisa.

Baadaye mwili wa Magesa unazikwa kwa heshima zote za kiserikali lakini utata mkubwa unaugubika msiba wake kwani mkewe haoneshi kuguswa hata kidogo na kilichotokea.

Upande wa pili, historia ya wanandoa hao inaelezewa ambapo mgogoro mzito unaibuka kati yao na kusababisha mpasuko mkubwa kwenye ndoa hiyo iliyodumu kwa miaka mingi.

Upande mwingine, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Daniel Mwampashi ambaye pia ni rafiki wa karibu wa Magesa, anakutwa amekufa nyumbani kwake ikiwa ni muda mfupi kabla hajawasilisha ripoti ya ukaguzi wake. Kibaya zaidi, usiku huohuo ofisi yake nayo inateketea kwa moto na nyaraka zote zinaungua.

Kabla hilo halijaisha, Magesa anajikuta akinasa kwenye mtego hatari na mwanamke aitwaye Grace ambapo wawili hao wanapigwa picha za utupu wakiwa hotelini na huo unakuwa mwanzo wa misukosuko mikubwa kwenye maisha ya waziri huyo.

Anatakiwa kutoa shilingi milioni hamsini ili picha zake za utupu zisivujishwe mtandaoni na kwa waandishi wa habari. Anahangaika na hatimaye anazipata fedha hizo, anafunga safari ya kuelekea Msitu wa Kazimzumbwi, Kisarawe mkoani Pwani alikoelekezwa kuzipeleka ambako ananusurika kuuawa.

Baadaye Grace, mwanamke aliyemwambia kwamba anazo taarifa juu ya wauaji wa Mwampashi anakutana na Magesa hotelini ambapo mbali na mambo mengine wawili hao wanajikuta wakiangukia dhambini.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Japokuwa Magesa alikuwa amepewa taarifa mbaya na za kushtua mno muda mfupi uliopita, Grace aliweza kumsahaulisha kila kitu, kwa mara nyingine shetani wake wa mahaba akapanda kichwani na kuchachamaa. Kilichofuatia kikawa ni mpambano mwingine wa kukata na shoka, usio na refa wala jezi.

Kwa zaidi ya muda wa saa mbili na dakika kadhaa, Waziri Magesa bado alikuwa amejifungia ndani ya chumba cha hoteli akiwa na Grace. Walifanya yao mpaka kila mmoja aliporidhika ambapo Waziri Magesa ndiye aliyekuwa wa kwanza kutoka hotelini baada ya kuwekeana ahadi na Grace juu ya siku na mahali pa kukutana wakati mwingine.

Magesa alipotoka aliwakuta walinzi wake wakiwa bado wako nje ya hoteli ile, wakiwa makini kuhakikisha ulinzi unadumishwa. Wakamsindikiza Magesa mpaka ndani ya gari lake na kuondoka mahali hapo bil amtu yeyote kujua kilichokuwa kinaendelea.

Muda mfupi baadaye, mwanamke aliyekuwa amevaa hijabu ndefu na kujifunga nikabu usoni iliyoziba uso wake wote na kuacha wazi macho tu, alionekana akitoka ndani ya hoteli hiyo. Akatembea harakaharaka mpaka kwenye kituo cha teksi na kuingia kwenye moja aliyoichagua.

Kwa kuwa muda ulikuwa umeenda sana, Waziri Magesa alipotoka hotelini hapo, alipitia ofisini kwake kama ushahidi tu, akaweka kila kitu vizuri kisha akaondoka na walinzi wake na safari ya kurejea nyumbani kwake ikaanza.

Dakika kadhaa baadaye, tayari alikuwa nyumbani kwake, kama kawaida yake akapokelewa na familia yake, wakiwemo watoto wake ambao muda huo tayari walikuwa wameshatoka shuleni. Wakaenda kukaa sebuleni na kuanza kuzungumza kama familia, wakipiga stori za hapa na pale.

“Umeshindaje mke wangu,” Magesa alimsalimu mkewe ambaye alionesha kutochangamka kama kawaida yake.

“Nzuri tu, za kazi.”

“Salama, hebu nakuomba ndani tuzungumze mara moja,” alisema Magesa kwa lengo la kutaka kujua nini kinamsumbua mkewe kwani huo ndiyo ulikuwa utaratibu wao wa siku zote katika ndoa yao. Kila mmoja alikuwa na jukumu la kujua nini kimesababisha mwenzake akawa katika hali isiyo ya kawaida inapotokea hivyo.

“Mbona nakuona hauna furaha mke wangu, nini tatizo?”

“Unanitia unyonge sana mume wangu, siku hizi umebadilika sana, angalia kama leo umechelewa sana kurudi nyumbani. Najua kazini umetoka tangu saa kumi jioni lakini sasa hivi saa moja ndiyo unaingia nyumbani. Halafu kwa nini ulikuwa umezima simu?” mke wa Magesa, Vivian alisema huku uso wake ukionesha kuwa na huzuni.

Kama kawaida yake, Magesa alianza kumbembeleza mkewe na kumtaka asimhisi vibaya kwani bado alikuwa akishughulikia matatizo yake ya kikazi, akamvuta mkewe kifuani kwake na kumkumbatia.

“Mh! Mbona kama unanukia pafyumu ngeni?” alihoji Vivian huku akijitoa mwilini mwa mumewe. Kauli hiyo iliufanya moyo wa Magesa ulipuke pyaaa! Akajua lazima mkewe atajua ukweli kwamba muda mfupi uliopita, alikuwa na mwanamke mwingine gesti.

Tangu waoane, Magesa hakuwahi kumsaliti mkewe hata mara moja mpaka alipokutana na Grace kwa hiyo hakuwa akizijua mbinu wanazozitumia wasaliti ili kuficha ushahidi wanapotoka kufanya yao. Magesa akawa anababaika.

“Aaah! Eeeh! Unajua leo tumebadilisha pafyumu kwenye gari, walinzi wangu walisema tuitoe iliyokuwepo kwa sababu inaweza kuwa imechanganywa na sumu kwa lengo la kuniua, unajua sasa hivi hatutakiwi kumuamini mtu,” alidanganya Magesa huku akikwepesha macho yake, mkewe akashusha pumzi ndefu na kurudi kumkumbatia tena mumewe.

Kwa kuwa mumewe hakuwahi kumsaliti au kumuoneshea vitendo vyenye ishara ya usaliti hata mara moja, hakuwa na cha kufanya zaidi ya kuamini kile alichoambiwa na mumewe, wakaendelea kukumbatiana huku Magesa akiendelea kuzungumza na mkewe na kumtaka atulie na yote wanayopitia yatafika mwisho.

“Napatwa na wasiwasi mkubwa mume wangu, ikitokea umekufa unafikiri nitafanya nini na hawa watoto na kama unavyojua umeshanizoesha kukaa nyumbani tu kila kitu unaniletea?”

“Mungu atanilinda mke wangu, wala usiwe na wasiwasi,” alisema Magesa huku akiendelea kutafakari kwa kina alichoambiwa na Grace.

“Mpaka sasa hivi hujajua nani anaweza kuwa adui yako na kwa nini anataka kukuua?”

“Mh! Hali ni tete mke wangu, hata wewe nikikwambia huwezi kuamini lakini siwezi kumhukumu mtu yeyote kwa sababu bado sina uhakika, nahitaji kufanya uchunguzi wa chini kwa chini kwanza,” alisema Magesa na kushusha pumzi ndefu. Baada ya mkewe kuendelea kumdadisi, ilibidi amueleze ukweli kwamba Innocent Kasaka, waziri mkuu na rafiki mkubwa wa familia hiyo ndiye aliyekuwa nyuma ya mpango wa kutaka kumuua Magesa.

“Hapana! Haiwezekani mume wangu! Haiwezekani,” alisema Vivian huku akiinuka pale kitandani alipokuwa amekaa na mumewe, akiwa haamini kabisa alichoambiwa.

“Hata mimi nilipoambiwa nilishtuka hivyohivyo.”

“Inawezekana aliyekwambia anataka kuzigombanisha familia zetu, hata jioni ya leo mke wake mbona alikuwa hapa nyumbani na tumezungumza mambo mengi sana ikiwemo matatizo yanayokukabili?” alisema Vivian.

“Inawezekana mkewe akawa hajui chochote, si unajua wanaume wengi huwa hawawashirikishi wake zao kwenye masuala kama hayo?”

“Kwani umemkosea nini mpaka afikie uamuzi huo? Kwanza yeye ni bosi wako na isitoshe ni rafiki yako mkubwa mpaka sasa familia zetu zimekuwa kama ndugu. Nini kimetokea?”

“Hata sielewi mke wangu, ndiyo maana nimesema ngoja niendelee kufanya utafiti kwanza kabla sijaamua chochote lakini kwa sasa hatutakiwi kumuamini mtu yeyote,” alisema Magesa, kwa pamoja wakainuka na kwenda sebuleni kuungana na watoto wao waliokuwa wakitazama runinga.

Mazungumzo ya hapa na pale yakaendelea lakini safari hii mke wa Magesa alionesha kuwa kwenye mawazo pengine kuliko hata ilivyokuwa mara ya kwaza. Taarifa alizopewa na mumewe zilimshtua mno na kumfanya ajiulize maswali mengi yaliyokosa majibu.

Wakiwa wanaendelea kutazama runinga, mara lilitokea tangazo la ‘breaking news’ runingani, wote wakaacha kila walichokuwa wanakifanya na kutegea macho na masikio kutaka kusikia ni habari gani iliyokuwa ikielekea kutangazwa.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Uwazi Mizengwe.


Loading...

Toa comment