The World You Left Behind 30
Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, unasababisha waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa kuwa mkali kama pilipili na anaahidi kuwachukulia hatua kali wote waliotajwa kwenye ripoti ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali.
Hata hivyo, kazi haiwi nyepesi kwake, muda mfupi baada ya kuvujishiwa ripoti ya ukaguzi wa hesabu za serikali na rafiki yake kipenzi, CAG Mwampashi, tukio baya linamtokea rafiki yake huyo zikiwa ni saa chache kabla ya kusoma ripoti hiyo hadharani.
CAG Mwampashi anauawa kikatili akiwa nyumbani kwake na ofisi yake inateketezwa na kubaki kuwa majivu. Kama hiyo haitoshi, Magesa ananusurika kwenye majaribio kadhaa ya kutaka kuukatisha uhai wake, hali inayolazimu awe anatembea na walinzi kila anakokwenda.
Upande wa pili, ndoa ya waziri huyo inakumbwa na migogoro ya hapa na pale. Baadaye Magesa anapenyezewa taarifa za kushtua mno juu ya mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake kwenye ajali ya kupangwa.
Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kuinusuru nafsi yake. Akiwa anahangaika kutafuta namna ya kujinusuru, matatizo mengine yanaibuka nyumbani kwake na kusababisha mkewe, Vivian aondoke kwa hasira.
Hatimaye siku ya tukio inawadia na tayari gari la Magesa, ambalo kila mmoja anaamini kwamba mwenyewe ndiye anayeliendesha, linaelekea eneo la tukio kulikopangwa ajali mbaya itokee.
Je, nini kitafuatia?
SONGA NAYO…
Kifaa maalum kilichofungwa ndani ya gari la Magesa lenye teknolojia ya hali ya juu, kilikuwa na uwezo wa kuonesha kila kitu kilichokuwa kinatokea barabarani, kama ambavyo dereva akikaa kwenye usukani anaona. Kilikuwa kinaonesha barabara yote kuanzia mbele gari linakoelekea, kushoto, kulia na upande wa nyuma.
Ilikuwa ni teknolojia kubwa mno ambayo watu wengi hawakuwa wanaijua, hasa ukizingatia ukweli kwamba hata bei ya gari hilo na vifaa vyake ilikuwa kubwa sana na kuwezesha watu wachache wamudu kununua.
“Kwa hiyo itakuwaje?”
“Mimi na wewe hatujui, tuendelee kufuatilia tutaona nini kitakachotokea,” alisema Grace, Magesa akawa anatetemeka mno, wote waliendelea kufuatilia kilichokuwa kinaendelea, gari likaendelea na safari bila mtu yeyote kujua kilichokuwa kinaendelea. Hata walinzi wa Magesa walikuwa na uhakika wa asilimia 100 kwamba bosi wao ndiye aliyekuwa ndani ya gari hilo.
Safari ikaendelea mpaka gari hilo lilipofika kwenye makutano ya Barabara za Msimbazi na Morogoro. Lilipofika kwenye taa za kuongozea magari, kwa kuwa taa nyekundu ilikuwa imewaka, gari lilijiseti lenyewe, likapunguza mwendo na hatimaye kusimama, magari mengine yaliyokuwa nyuma nayo yakafanya hivyohivyo.
Grace na Magesa walikuwa kimya kabisa wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea kwa kutumia laptop ndogo, wakawa wanasubiri kuona nini kitatokea kwani hilo ndiyo eneo lililopangwa kuyakatisha maisha ya Magesa.
“Tazama kwa makini kitakachotokea halafu utaniambia kama nilichokwambia awali ni kweli au la,” alisema Grace, Magesa akazidi kuiinamia ile laptop huku mapigo ya moyo wake yakimuenda mbio kuliko kawaida.
Gari la kifahari aina ya Range Rover Evoque (New Model) liliendelea kusimama kwenye taa za kuongozea magari huku magari mengine nayo yakiwa yamesimama isipokuwa yale tu yaliyoruhusiwa na taa hizo za barabarani.
Hakuna mtu ambaye angeweza kugundua kwamba gari hilo lilikuwa likijiendesha lenyewe, vioo vya ‘tinted’ vilizidi kulifanya suala hilo kuwa fumbo gumu. Hatimaye taa za kijani ziliwaka, magari yote yakaendelea na safari likiwemo gari la Magesa lakini ghafla, wakati gari hilo likiwa limefika katikati ya makutano hayo, lori kubwa la mafuta lilionekana likija kwa kasi kubwa utafikiri magari ya mashindano, kutokea upande wa Barabara ya Msimbazi.
Japokuwa taa nyekundu ziliwaka kuashiria magari yanayotoka upande huo hayaruhusiwi, dereva hakuonesha kupunguza mwendo, likawa linatoa muungurumo mkubwa kama ndege inayotaka kupaa.
Kila mtu aliyekuwa eneo hilo alibaki amepigwa na bumbuwazi, wengine wakajishika vichwa wakiwa hawaamini kama kile kilichokuwa kinaelekea kutokea ni kweli. Ungeweza kufananisha na filamu za kusisimua za Hollywood lakini haikuwa hivyo.
Kufumba na kufumbua, kilisikika kishindo kikubwa cha kutisha, gari la Magesa likaburuzwa mita kadhaa kabla ya kishindo kingine kikubwa zaidi kusikika wakati magari hayo yakilipuka.
Moshi mkubwa ukatanda angani, ungeweza kudhani kwamba tayari giza limeshaingia kutokana na jinsi moshi huo ulivyosababisha giza nene eneo hilo. Watu wakawa wanakimbia huku na kule, wengine wakiokoa nafsi zao na wengine wakijaribu kwenda kutoa msaada.
***
“Mungu wangu!” Magesa alisema kwa sauti ya mshtuko wa hali ya juu, akamgeukia Grace aliyekuwa ametulia pembeni yake, akaitazama tena ile laptop, hakuweza kuona chochote zaidi ya moto na moshi mzito na baadaye ikawa haioneshi kitu chochote.
“Nataka kuendelea kuona mpaka mwisho.”
“Haiwezekani Magesa, vifaa vyote vilivyofungwa kwenye gari vimeshateketea.”
“Kwa hiyo itakuwaje sasa,” alisema Magesa huku akijifuta jasho jingi lililokuwa linamlowanisha karibu kila sehemu ya mwili wake.
“You are dead!” (Umekufa!) alijibu Grace huku akiizima laptop hiyo na kuiweka kwenye begi lake.
Magesa alishindwa kujizuia, akakaa chini na kuanza kuangua kilio mithili ya mtu aliyepokea taarifa za msiba. Machozi na kamasi vikawa vinamtoka kwa wingi.
“Nimewakosea nini mpaka wafikie hatua ya kuandaa mipango hatari kama hii ya kuniua? Nimewakosea niniiii?”
“Magesa, hatuna muda wa kupoteza, inuka nifuate haraka,” alisema Grace kwa sauti yenye mamlaka, harakaharaka Magesa alimfuata, wakaingia vyumba vya ndani vya jengo hilo.
“Lete hiyo simu yako. Itabidi uvae hizi nguo.”
“Mh! Nitavaaje nguo za kike?” alisema Magesa wakati akimkabidhi Grace simu, akaifungua na kutoa laini, akaivunja mbele ya macho ya Magesa.
“Inabidi uvae tu Magesa, umeshaingia kwenye ulimwengu mwingine kabisa. Ule ulimwengu uliouzoea umeshauacha nyuma yako, vaa twende,” alisema Grace. Naye akabadilisha nguo na kuvaa baibui na nikabu. Akamsaidia Magesa naye kuvaa baibui na nikabu, mkononi akamshikisha mkoba wa kike, akawa na mwonekano wa kike kabisa.
“Tunaelekea wapi?”
“Utajua mbele ya safari,” alisema Grace.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Uwazi Mizengwe.