The House of Favourite Newspapers

The World You Left Behind 42

0

Matumizi mabaya ya fedha za serikali na ubadhirifu mkubwa unaotokea kwenye Wizara ya Fedha, vinamsababishia waziri mwenye dhamana katika wizara hiyo, Abbas Magesa matatizo makubwa na kufanya roho yake iwindwe kwa udi na uvumba.

Mpango wa hatari wa kuyakatisha maisha yake unaandaliwa na kwa bahati nzuri, Grace, mwanamke aliyekutana naye kwenye mazingira ya kutatanisha, anamueleza kuhusu mpango huo na kumpa mbinu za nini cha kufanya ili kunusuru maisha yake.

Hatimaye siku ya tukio inawadia na kwa utaalamu wa hali ya juu, Grace anamuokoa Magesa huku watu wengine wote wakiamini kwamba waziri huyo amekufa kwenye ajali hiyo. Wawili hao wanatorokea mafichoni Mombasa, Kenya ambako Magesa analazimika kuanza maisha mapya kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Grace anasafiri kuelekea Israel kikazi na Magesa anaitumia nafasi hiyo kumpekua mwanamke huyo akitaka kuujua ukweli wa maisha yake. Anachokutana nacho kinamshangaza sana. Hatimaye Grace anarejea na Magesa anambana kwa maswali magumu, hali inayosababisha mwanamke huyo apasue jipu na kueleza ukweli.

Upande wa pili, uchunguzi wa kina juu ya kifo cha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Mwampashi ambaye alikuwa na urafiki wa karibu na Magesa unazidi kushika kasi na viongozi wa juu wa usalama, wamepeana saa 72 kuhakikisha ukweli unafahamika kuhusu kilichojificha nyuma ya mauaji hayo na tayari kuna kila dalili ya siri kufichuka.Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Inspekta Jordan Ngai, Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi aliendelea kumhoji maswali magumu Dokta Mathias Msalala, daktari uliyeufanyia vipimo mwili wa marehemu Daniel Mwampashi, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Daktari huyo akawa anapekua kwenye kabati lake akitafuta kitabu maalum (disptach) ambacho ndicho kilichokuwa na jina la askari aliyemkabidhi risasi alizozitoa kwenye mwili wa marehemu Mwampashi siku alipoufanyia uchunguzi mwili huo.

Baada ya muda, Dokta Msalala alifanikiwa kukipata kitabu hicho lakini katika hali iliyomshangaza kila mmoja, ukurasa ambao ndiyo daktari huyo aliodai kwamba alijaza taarifa hizo, ulikuwa umechanwa.

“Kwani ofisi hii mnatumia watu wangapi?”
“Tunatumia wengi mkuu lakini hakuna mwenye tabia ya kupekua vitu visivyomhusu.”
“Unataka kunihakikishia kwamba siyo wewe uliyechana hiyo katarasi kwa lengo la kuficha ushahidi?”

“Nakuapia mkuu, tena nimekumbuka kitu. Siku ile wakati namkabidhi yule askari hizo risasi, kuna moja ilidondokea chini ya kabati lakini mwenyewe hakuiona, hebu tusaidiane kulisogeza hili kabati pembeni tunaweza kuiona,” alisema daktari huyo huku hofu ikizidi kuongezeka ndani ya moyo wake.

Tangu aanze kazi yake hiyo, hakuwahi kukutana na tukio la ajabu kama hilo, akasaidiana na Inspekta Ngai na kwa bahati nzuri, walifanikiwa kuiona risasi moja ikiwa sakafuni. Kwa umakini wa hali ya juu, Inspekta Ngai aliiokota na kuiweka kwenye kifuko maalum kisha akaandika maelezo juu yake na kuiweka kwenye begi lake.

Akaendelea kumhoji daktari huyo kisha akamuaga na kuahidi kurudi muda wowote atakapohitaji ushirikiano wake. Akatoka huku na yeye akiwa na maswali mengi ndani ya kichwa chake. Dokta Msalala ni kama alikuwa amepigwa na bumbuwazi kubwa, akiwa haelewi ni mchezo gani uliokuwa ukiendelea.

Baada ya Inspekta Ngai kuondoka, alibaki ametulia ofisini kwake, akiendelea kujiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.

* * *
Ephraim Mandiba, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, akishirikiana na vijana wake, aliendelea na kazi ya kuhakikisha wanafahamu kila kitu kilichokuwa kimejificha nyuma ya tukio la kifo cha Mwampashi.

Vijana wake waliotumwa nyumbani kwa marehemu Magesa, hawakupata shida ya kupata walichokifuata kwani mtoto mkubwa wa marehemu, Ivan Magesa aliwapa ushirikiano wote uliokuwa ukihitajika. Wakafanikiwa kupata laptop ya marehemu Magesa ambapo bila kupoteza muda walimpigia simu bosi wao aliyewapa maelekezo ya sehemu ya kukutania.

Wale vijana waliotumwa wizarani, nao walifanikiwa kupata namba za laptop iliyokuwa ikitumiwa na marehemu Mwampashi ambayo iliibwa siku aliyouliwa akiwa nyumbani kwake.

Muda mfupi baadaye, Mandiba alikuwa ofisini kwake na vijana wake ambapo kwa pamoja walianza kushughulikia taarifa zote walizozipata.

Cha kwanza ilikuwa ni kuanza kuitafuta laptop iliyokuwa inatumiwa na Mwampashi ambapo kwa kutumia teknolojia ya anuani ya vifaa vilivyounganishwa na intaneti iitwayo Media Access Control Address (MAC address) pamoja na namba ya utambulisho wa kifaa chochote cha mawasiliano ya kielektroniki, International Mobile Station Equipment Identity (IMEI) kazi hiyo ilianza mara moja.

Ukimya ulitawala ndani ya ofisi hiyo, kelele pekee zilizokuwa zinasikika zilikuwa ni za kugongwagongwa kwa ‘keyboard’ za laptop wakati timu nzima ikiwa bize kuitafuta laptop hiyo.

Kutokana na ubora wa teknolojia iliyokuwa inatumika, muda mfupi tu baadaye, kitufe chekundu kwenye moja ya laptop zilizokuwa zinatumika kwa kazi hiyo, kilianza kuwaka na muda mfupi baadaye, ramani ya satelaiti ilifunguka kwenye kompyuta kubwa iliyokuwa ndani ya ofisi hiyo, ikionesha mahali laptop hiyo ilipokuwa.

“Tumeipata! Kwisha kazi,” alisema mmoja wa wataalamu hao huku akionesha kuwa na furaha, wote wakaacha kila walichokuwa wanakifanya na kusogea kwenye kompyuta hiyo kubwa, wakawa wanafuatilia kwa makini ili kuweza kusoma ramani ya mahali laptop hiyo ilipokuwa.

“Tumieni hii ramani ya GPS (Global Positioning System) kufuatilia mahali ilipo, nataka mrudi nayo, hata ikibidi kutumia nguvu mnajua nini cha kufanya,” alisema Mandiba kwa sauti yenye mamlaka.

Bila kupoteza muda, vijana watatu walitoka mpaka kwenye maegesho ya magari nje ya ofisi hiyo, wakaingia kwenye gari lililokuwa na vioo vyeusi (tinted) na safari ya kuelekea Mwenge ikaanza kwa kasi kubwa mithili ya magari ya mashindano.

Baada ya vijana hao kuondoka, Mandiba na vijana wengine waliobakia ofisini hapo, walianza kushughulika na laptop iliyokutwa nyumbani kwa Magesa ambapo waliichomeka kwenye umeme kwa kuwa haikuwa na chaji kabisa kisha muda mfupi baadaye wakaiwasha.

“Inaonekana imefungwa kwa password,” alisema kijana mmoja, Mandiba akamtazama kwa jazba.

“Kwa hiyo kama imefungwa kwa password mimi nifanyeje? Unakuwa utafikiri ndiyo umeanza kazi leo? Hebu tumia Power ISO na Password Cracker kuingia ndani,” alisema Mandiba, kijana huyo akahisi kufedheheka kwa sababu alikuwa anajua nini cha kufanya unapokutana na laptop, kompyuta au simu iliyofungwa kwa password.

Harakaharaka akasaidiana na mwenzake chini ya usimamizi wa Mandiba mwenyewe na muda mfupi baadaye walifanikiwa kutoa password iliyowekwa kwa kutumia teknolojia za kitaalamu za Power ISO na Password Cracker.

Kwa umakini wa hali ya juu wakaanza kufuatilia mawasiliano ya barua pepe kati ya Magesa na Mwampashi enzi za uhai wao.
* * *
“Magesa!”
“Naam mpenzi wangu.”
“Kuna jambo nahisi halipo sawa hapa. Laptop yako ulikuwa nayo ndani ya gari siku ile ya ajali?”
“Hapana, niliiacha nyumbani.”

“Kuna mtu huwa anaitumia tofauti na wewe?”
“Hapana, kwanza ina password ambayo hakuna mtu yeyote anayeijua. Hata mwanangu Ivan na utundu wake wote hajui chochote.”

“Sasa mbona inaonesha imewashwa muda mfupi uliopita?”
“Imewashwa? Nani kaiwasha na wewe umejuaje wakati tuko wote hapa ndani?”
“Kuna mitambo yangu nilishakuwa nimeiunganisha kipindi kirefu tu kufuatilia kila ulichokuwa unafanya kwenye laptop yako, niamini ninachokwambia kwamba imewashwa, njoo ujionee mwenyewe,” alisema Grace na kuongozana na Magesa mpaka kwenye chumba kidogo kilichokuwa na vifaa vingi vya mawasiliano.

Akamuonesha laptop ndogo ambayo juu yake kulikuwa na ramani ya mtandaoni ikionesha kilichokuwa kinafanyika ndani ya laptop hiyo. Magesa akabaki amepigwa na butwaa, kwanza alishangaa iweje Grace awe na uwezo wa kujua kitu kama hicho na pili ni akina nani waliokuwa wakishughulika na laptop yake.

“Ina siri nyingi sana ndani yake, hata sijui itakuwaje,” alisema Magesa lakini Grace akamwambia asiwe na wasiwasi kila kitu kitakuwa sawa.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumanne ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply