The House of Favourite Newspapers

The World You Left Behind (Dunia Uliyoiacha Nyuma Yako)-22

0

Ajali mbaya na ya kutisha inatokea kwenye Makutano ya Barabara za Morogoro na Msimbazi, katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Gari la Mheshimiwa Abbas Magesa, Range Rover Evoque linagongwa na lori la mafuta na kuteketea kabisa.

Baadaye mwili wa Magesa unazikwa kwa heshima zote za kiserikali lakini utata mkubwa unaugubika msiba wake kwani mkewe haoneshi kuguswa hata kidogo na kilichotokea.

Upande wa pili, historia ya wanandoa hao inaelezewa ambapo mgogoro mzito unaibuka kati yao na kusababisha mpasuko mkubwa kwenye ndoa hiyo iliyodumu kwa miaka mingi.

Upande mwingine, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, CAG Daniel Mwampashi ambaye pia ni rafiki wa karibu wa Magesa, anakutwa amekufa nyumbani kwake ikiwa ni muda mfupi kabla hajawasilisha ripoti ya ukaguzi wake. Kibaya zaidi, usiku huohuo ofisi yake nayo inateketea kwa moto na nyaraka zote zinaungua.

Kabla hilo halijaisha, Magesa anajikuta akinasa kwenye mtego hatari na mwanamke aitwaye Grace ambapo wawili hao wanapigwa picha za utupu wakiwa hotelini na huo unakuwa mwanzo wa misukosuko mikubwa kwenye maisha ya waziri huyo.

Anatakiwa kutoa shilingi milioni hamsini ili picha zake za utupu zisivujishwe mtandaoni na kwa waandishi wa habari. Anahangaika na hatimaye anazipata fedha hizo, anafunga safari ya kuelekea Msitu wa Kazimzumbwi, Kisarawe mkoani Pwani alikoelekezwa kuzipeleka.

Hata hivyo, huko anakumbana na balaa jingine. Anaokolewa akikaribia kukata roho na kukimbizwa hospitalini. Akiwa hospitalini, Grace, mwanamke aliyemuingiza kwenye matatizo hayo anamfuata.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Baada ya kukamilisha taratibu zote muhimu hotelini hapo, Waziri Magesa alimpigia simu mlinzi wake na kumuelekeza kumpeleka mgeni huyo moja kwa moja mpaka hotelini. Dakika kadhaa baadaye, tayari Grace alikuwa ameshafikishwa hotelini hapo, akapelekwa moja kwa moja mpaka kwenye chumba alichokuwa amekodi Waziri Magesa.

“Umefanya vizuri sana kuvaa hiyo nikabu na baibui, mtu hawezi kukutambua kwa urahisi. Hata mimi tungekutana barabarani wala nisingekujua,” alisema Waziri Magesa mara baada ya mwanamke huyo kuingia, wakacheka na kugongesheana mikono.

Baada ya milango kufungwa, Grace alivua nikabu na baibui alivyokuwa amevaa, Magesa akashusha pumzi ndefu na kumtazama.

“Mbona unaniangalia sana?”

“Mh! Wewe ni mrembo sana ukichanganya na hayo mavazi uliyovaa ndiyo kabisa,” alisema Waziri Magesa, mwanamke huyo akaachia tabasamu pana lililozidi kumfanya aonekane mrembo zaidi.

“Pole sana kwa matatizo.”

“Usijali, nimeshapoa.”

“Enhee! Hebu nisimulie vizuri, nini kilitokea?” alisema mwanamke huyo huku akikaa kitandani, pembeni ya Waziri Magesa. Waziri Magesa alishusha pumzi ndefu kisha akaanza kumsimulia upya mwanamke huyo kila kitu alichokutana nacho.

“Nimekusababishia matatizo makubwa sana jamani, naomba unisamehe,” alisema mwanamke huyo na kumsogelea Magesa mwilini kiasi kwamba kila mmoja akawa anazisikia pumzi za mwenzake.

Kwa jinsi mwanamke huyo alivyokuwa mrembo, ukichanganya na nguo alizokuwa amebakiwa nazo baada ya kuvua baibui, Magesa alijikuta kwenye wakati mgumu mno, akashusha pumzi ndefu tena huku mapigo ya moyo wake yakianza kumwenda mbio kuliko kawaida.

Muda mfupi baadaye, wawili hao walikuwa wamekumbatiana kimahaba, wakiwa wamegusanisha ndimi zao mithili ya njiwa anayeyalisha makinda yake. Japokuwa Magesa hakuwa amepanga jambo hilo litokee, alijikuta akishindwa kabisa kumhimili shetani wa mahaba aliyekuwa amechachamaa ndani ya kichwa chake.

Dakika kadhaa baadaye, sauti za miguno ya kimahaba zilikuwa zikisikika kutokea ndani ya chumba hicho cha hoteli, Waziri Magesa na Grace wakielea kwenye dimbwi la mapenzi.

“Leo nimeamini kama kweli unanipenda, ahsante sana ila naomba tutunze siri, asijue mke wangu au mtu mwingine yeyote, si unajua mimi ni kiongozi wa serikali?”

“Wala usijali Magesa, hakuna mtu yeyote atakayejua, nataka tudumu pamoja kwa kipindi kirefu,” alisema Grace, akiwa amejilaza juu ya kifua cha Magesa, wakiendelea kufanyiana vituko vya kimahaba vya hapa na pale.

“Haya niambie ukweli sasa, nani alihusika na kifo cha rafiki yangu Mwampashi? Nataka pia uniambie wanaoniwinda ni akina nani.”

“Mh! Mbona una haraka hivyo? Nitakwambia kila kitu lakini nataka uniahidi kitu kimoja.”

“Kitu gani unataka nikuahidi?”

“Nataka uniahidi kwamba hutamwambia yeyote kwamba mimi ndiyo nimekwambia.”

“Kuhusu hilo wala usiwe na wasiwasi.”

“Unakumbuka kabla marehemu Mwampashi hajavamiwa nyumbani kwake na kuuawa wewe na yeye mlikutana pale City Garden Hotel?”

“Ndiyo! Tena tulizungumza kwa kirefu sana. Kwani wewe ulikuwa wapi mpaka ukatuona?”

“Wewe nijibu kwanza. Mlikuwa mnazungumzia nini?”

“Tulikuwa tunazungumzia ishu za kazi na mambo yetu mengine, si unajua jamaa alikuwa rafiki yangu sana.”

“Pale wakati mnazungumza ni nani mwingine alikuwepo?”

“Tulikuwa wenyewe tu, wengine walikuwa na wateja wa kawaida ambao hatuwafahamu.”

“Hebu jaribu kukumbuka vizuri, hakuna mtu unayemfahamu aliyekuja?”

“Hakuna, tulikuwa wenyewe tu.”

“Basi hukuwa makini, hukumuona dereva wa mheshimiwa waziri mkuu?”

“Nani, Twalipo?”

“Huyohuyo, mbona mimi nilimuona, tena alikuwa amekaa jirani kabisa na wewe,” alisema Grace na kumfanya Waziri Magesa ajaribu kuvuta kumbukumbu zake nyuma. Licha ya kujaribu kukumbuka vizuri, bado hakupata picha juu ya kile kilichokuwa kinazungumzwa na mwanamke huyo.

Alishindwa kuelewa kuna uhusiano gani kati ya kilichotokea mpaka rafiki yake akapoteza maisha na yeye kunusurika kuuawa mara kadhaa.

“Sijakuelewa.”

“Najua huwezi kunielewa kirahisi lakini kwa kifupi tu, adui yako mkubwa ni mheshimiwa waziri mkuu, misimamo yako katika kazi ndiyo inayokuponza. Mimi nimeamua kukusaidia kwa sababu nakupenda lakini vinginevyo nisingeweza kuhatarisha maisha yangu kwa namna yoyote ile.

“Bado sijakuelewa, hebu nifafanulie,” alisema Waziri Magesa huku akionesha kuwa na hofu kubwa mno ndani ya moyo wake. Hakutaka kuamini kwamba mheshimiwa Innocent Kasaka anaweza kuwa anahusika kama mwanamke huyo alivyokuwa anamwambia.

“Unakumbuka ripoti aliyokupa mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali, rafiki yako Mwampashi kabla hajafikwa na mauti?”

“Ndiyo, tena nakala yake nyingine ninayo.”

“Si unakumbuka kwamba ilionesha kwenye wizara yako kuna ubadhirifu mkubwa sana?”

“Ndiyo, tena nikalazimika kuitisha mkutano wa dharura na wenzangu na kuwataka kila mmoja ajipime na kuona anahusikaje katika kashfa iliyoibuliwa na Mwampashi.”

“Basi kwa taarifa yako, mheshimiwa Kasaka anashirikiana na wasaidizi wako na kama huamini, anza kufuatilia najua utagundua mambo mengine makubwa zaidi,” alisema mwanamke huyo.

Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Uwazi Mizengwe.

Leave A Reply