The House of Favourite Newspapers

Thomas Sankara, Rais Aliyekuwa Analipwa Mshahara Wa Dola 450 Kwa Mwezi

        sankara5Thomas Sankara (21 Desemba, 1949 – 15 Octoba, 1987).

Maisha ya siasa barani Afrika ni kama tanuru la moto, wengi wametumbukia na kuyeyuka na kuacha simanzi kubwa kwa wafuasi wao. Kwenye orodha hii tunao viongozi wengi waliouawa kikatili na wengine kudharirishwa.

Hii ndiyo Afrika iliyomeza wanasiasa wengi wazuri na mfano kwa kizazi na kizazi. Steve Biko aliuawa akiwa na miaka 30 tu, huyu alikuwa kiongozi wa kupinga suala la ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini kwa kushirikiana na akina Nelson Mandela.

Patrice Lumumba akiwa Waziri Mkuu wa Congo aliuawa na vibaraka wa magharibi wakiongozwa na Mobutu Seseseko wakati huo akiwa na miaka 35 tu. Thomas Sankara aliuawa akiwa na miaka 37 kwenye mapinduzi yaliyoratibiwa na rafiki yake wa karibu.

Thomas Sankara ni nani?

Thomas Sankara anafahamika kama “Che” Guevara wa Afrika’, alikuwa rais wa nchi ya Burkinafaso kuanzia mwaka 1983 hadi 1987.

sankaraThomas Sankara.

Aliingia madarakani na kuwa rais wa Burkina Faso baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa Rais Jean-Baptiste Ouédraogo, wakati huo akiwa na miaka 33.

Alizaliwa Desemba 21,1949 kwenye familia ya wacha mungu, baba yake Sambo Joseph Sangara na mama yake Marguerite Sankara walikuwa waumini wa dini ya wakatoliki (Catholic).

thomas-sankara…Kwenye shughuli za kiserikali wakati wa uhai wake.

Akiwa mdogo wazazi wake walitaka mtoto wao awe mhubiri wa dhehebu lao ndoto ambayo haikuweza kutimia.

Baada ya kumaliza elimu ya sekondari kwenye shule ya Gaoua iliyopo jijini Bobo-Dioulasso, mwaka 1966 alijiunga na jeshi akiwa na miaka 19 ambako alifuzu mafunzo ya urubani wa ndege za kijeshi.

sankaraaaThomas Sankara akiwa kwenye shughuli za kijeshi.

Baada ya mwaka mmoja alipelekwa nchini Madagascar kuongeza ujuzi wa kijeshi na akiwa huko alishuhudia maandamano makubwa dhidi ya serikali ya Philibert Tsiranana na kwa mara ya kwanza alijifunza nguvu ya falsafa za Karl Max na Vladimir Lenin.

Alirejea nchini kwake mwaka 1972 na miaka miwili baadaye alishiriki kwenye vita ya kugombea mpaka kati ya nchi yake na Mali. Walishinda vita hivyo.

Mbali na jeshi pia alikuwa mpiga gitaa mzuri akipigia bendi ya Tout-à-Coup Jazz  na mwendesha pikipiki mzuri hali iliyompa umaarufu mkubwa kwenye Jiji la Ouagadougou.

Mwaka 1976 alipanda cheo na mkuu wa kikosi cha makomando na mwaka huohuo alikutana na Blaise Compaore nchini Morocco na kuunda kikosi cha siri cha wanajeshi kwa jina la Kikosi cha makomandoo wenye mlengo wa kijamaa (Regroupement des officiers communistes, or ROC).

sankara1Thomas Sankara.

Viongozi wa kikundi hiki walikuwa Henri Zongo, Jean-Baptiste Boukary Lingani, Blaise Compaoré na Thomas Sankara. Hawa ndiyo walisababisha mapinduzi ya utawala wa Rais Jean-Baptiste Ouédraogo.

Juhudi zake za kujituma kwenye nafasi yake ilipelekea mwaka 1981 kuteuliwa kuwa katibu mkuu wa wizara ya mawasiliano na alivunja rekodi kwa kwenda na usafiri wa baiskeli kwenye kikao cha kwanza cha baraza la mawaziri kilichofanyika kwenye ikulu ya nchi hiyo, nafasi ambayo hakudumu nayo kwa muda mrefu.

Baada ya kupinduliwa kwa serikali ya Kanali Saye Zerbo Novemba 7, 1982 na kuingia kwa utawala wa Meja Jean-Baptiste Ouédraogo, Thomas Sankara aliteuliwa na kuwa waziri mkuu.

Alipewa nafasi hiyo baada ya kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa kijeshi waliofanikisha kuondolewa madarakani kwa Rais Saye Zerbo.

Alidumu kwenye nafasi hiyo kwa muda wa miezi minne tu kabla ya kuondolewa na kuwekwa chini ya ulinzi mkali nyumbani kwake baada ya kutembelewa na mtoto wa rais wa ufaransa wa wakati huo, François Mitterrand.

sankara2Thomas Sankara kwenye moja ya majukumu yake akiwa rais.

Pia viongozi wawili wa ROC Henri Zongo na  Jean-Baptiste Boukary Lingani nao waliwekwa chini ya ulinzi mkali hali iliyopelekea wananchi wengi kuandamana wakiishinikiza serikali kuwaachia huru.

Wakiwa chini ya ulinzi mkali, kiongozi mwingine wa ROC, Blaise Compaore aliongoza mapinduzi ya kuwakomboa wanachama wenzake.

Hapa yakupasa uelewe jambo moja muhimu kwamba ROC walikuwa ni makomando walioiva kijeshi na wenye uwezo wa hali ya juu, kwa kusaidiana na serikali ya Libya chini ya Muammar Gaddafi haikuwa ngumu kwao kuusambaratisha utawala wa Rais Jean-Baptiste Ouédraogo na kumkomboa Waziri Mkuu na siku hiyo alitangazwa kuwa Rais wa Burkina Faso.

thomas-sankara2Thomas Sankara akiwa na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Akiwa rais aliiongoza nchi hiyo kutoka taifa maskini hadi taifa lenye uwezo mkubwa wa kiuchumi na kijeshi kwa muda wa miaka minne tu.

Ndiye aliyebadili jina la nchi yake kutoka Upper Volta na kuwa Burkina Faso likiwa na maana ya ‘Ardhi ya Watu Wenye Akili.

SIKU YA KIFO CHAKE

Oktoba 15, 1987 akiwa ikulu alipinduliwa na kuuawa na mwili wake kufukiwa mahali pasipojulikana.

Mauaji hayo yaliratibiwa na rafiki na mwanachuo mwenzake ambaye ndiye alifanikisha yeye kuwa rais, Blaise Compaore ambaye ndiye alirithi kiti chake.

compaore-and-sankaraCompaore (kushoto) akiwa na Sankara (kulia).

Kwa madai kwamba Sankara alikuwa na uhusiano na watu wabaya akina Prince Johnson ‘bwana vita’ aliyehusika na mauaji ya Rais Samuel Doe wa Liberia, Charles Taylor na Ufaransa.

Mauaji ya hayo yaliambatana na vifo vya wasaidizi wake wa karibu 12 wakiwemo mawaziri na walinzi wake. Baada ya mauaji hayo mwili wake ulizikwa kwa siri hadi mwaka 2015 karibu lake lililoponekana na kupewa heshima.

sankara42Kaburi la Thomas Sankara.

Aliuawa wakati akihutubia baraza la mawaziri wa serikali yake. Kikosi kilichoingia ikulu na kutekeleza mauaji hayo kiliongozwa na Mkuu wa Walinzi wa Usalama wa Rais, bwana Yacinthe Kafando ambaye baada ya kutekeleza mauaji hayo naye alikamatwa na kunyongwa lengo kuu likiwa kuficha siri.

guineas-junta-leader-dadis-camara1-mtuhumiwaYacinthe Kafando.

Compaore hakutaka ijulikane kama yeye ndiye kahusika na mauaji ya rafiki yake na hakutaka kaburi la wapi kazikwa Sankara lionekane, bahati mbaya hakuna siri ya watu wawili duniani yote yalijulikana baadaye.

 compaoreAliyekuwa rais wa Burkina Faso, Blaise Compaore.

Mtu mwingine aliyehusika kwenye mauaji ya Sankara, bwana Arzouma Ouedraogo naye alifariki kwenye ajali ya gari siku chache baada ya kuachiwa kutoka kwenye kifungo cha siri. Wengi wanaamini aliuawa ili kuficha siri ya nani alihusika na mipango ya kuuawa kwa Rais Sankara, kipenzi cha wananchi maskini wa Burkinafaso.

Mke wake Marium na watoto wake wawili, Philipe na August walifanikiwa kutoroka na kukimbilia nchini Ufaransa alikoishi miaka 20 baada ya Compaore kutangaza kuwaua lengo likiwa kupoteza kabisa kizazi cha Sankara.

mariam-sankara-2Mke wa Thomas Sankara, Mirium.

Thomas Sankara atakumbukwa kwa kupiga vita rushwa ikiwemo kujilipa mshahara wa shilingi za kitanzania shilingi laki tisa kwa mwezi (thamani ya sasa), wakati huo alikuwa analipwa dola 450 tu.

Alipiga marufuku matumizi ya anasa kwa viongozi wa serikali ikiwa ni pamoja na kuzuia matumizi ya magari ya thamani aina ya Mercedes Benz. Alizuia maafisa wa serikali kusafiri kwa ndege daraja la kwanza.

Jambo lililowashangaza wengi alizuia picha zake kuwekwa kwenye majengo au ofisi za serikali. Na aligoma misaada ya kutoka nje kwa kusema,” Yeyote anayekupa lishe lazima akutawale, utakuwa chini yake.”

sankaraThomas Sankara.

Wiki moja kabla ya mauti yake alisema;

 “Wanaharakati ni kama binadamu wengine na wanaweza kuuawa, lakini huwezi kuua mawazo yao.”

Na Leonard Msigwa/GPL/MTANDAO.

 

 

 

 

 

 

Comments are closed.