The House of Favourite Newspapers

Ticha Afa Ajalini Akifuatilia Kadi ya Bima Ya Afya

marehemu-4 marehemu-6

Wananchi wakimuaga marehemu, Janeth Francis Songo alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Maluga iliyopo Wilaya ya lramba mkoani Singida.

Stori: Dustan ShekideleRisasi Mchanganyiko, Jan 4-6, 2017, Toleo 1388

MOROGORO: Ni majonzi makubwa! Mwalimu wa Shule ya Msingi Maluga iliyopo Wilaya ya lramba mkoani Singida, Janeth Francis Songo, wiki iliyopita alileta simanzi kubwa kwa wakazi wa mjini Morogoro baada ya kufariki katika ajali ya gari iliyosababisha vifo vya watu wawili.

back-risasi-copy

Janeth, mama wa mtoto mmoja na mke wa Askari Polisi Joseph Kasala, alikutwa na mauti baada ya basi alilokuwa amepanda kupata ajali katika Kijiji cha Tumulo kilichopo mkoani Singida akiwa njiani kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya kusaidia matibabu ya mama yake mzazi, Mliguna Sunga aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

marehemu-1

Marehemu Janeth  Songo enzi za uhai wake.

Kwa mujibu wa mume wa marehemu, mkewe alilazimika kwenda Iramba, ambako ndiko kilipo kituo chake cha kazi kufuata kadi ya Bima ya Afya, ili aweze kumtibia mama yake mzazi, aliyehamishwa kutoka Morogoro kuelekea Muhimbili baada ya kupatwa na maradhi.

marehemu-3

Mume wa marehemu Janeth Songo akilia wakati akiaga mwili wa aliyekuwa mkewe.

“Mke wangu alikuwa amekuja likizo ya mwisho wa mwaka, yeye ni mkazi wa hapa Morogoro, sasa mama mkwe akapatwa ugonjwa akakumbuka kadi yake ya Bima ya Afya ameisahau Iramba, akataka kwenda nikamzuia, nikasema tutajichangachanga tumtibie, lakini bahati mbaya hali yake ikazidi kuwa mbaya akahamishiwa Muhimbili, sasa kule unajua gharama za vipimo na matibabu ziko juu, ndiyo akasema acha akimbie mara moja.

“Jumatano mke wangu aliamua kwenda lramba, Alhamisi alishinda kule na Ijumaa akapanda basi la moja kwa moja hadi Dar, bahati mbaya walipofika Kijiji cha Tumulo, gari likapata ajali na akafa yeye na dereva, tumeshindwa kumwambia mama mkwe juu ya kifo hicho cha mwanaye aliyekuwa akimtegemea kwa kila kitu,” alisema.

marehemu-2

Mtoto wa marehemu akiwa kabebwa.

Akisoma wasifu wa marehemu, mmoja wa wanafamilia alisema Janeth alizaliwa Morogoro Desemba 28, 1989 na alifunga ndoa ya bomani mwaka 2015 na mchumba wake Joseph Kasala na kujaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume, Eliud.

Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule hiyo, Manase Kipeta alisema taifa limepoteza nguvu kazi kubwa kwani Janeth alikuwa bado mdogo aliyekuwa akifundisha masomo mbalimbali katika madarasa ya juu ya 6 na 7, hivyo ameacha pengo kubwa katika shule yao.

Joseph Kasala ambaye ni askari polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi Morogoro, akimlilia mkewe alisema japokuwa kuna wanawake wengi, itakuwa vigumu mno kwake kuweza kumpata wa aina yake.

“Wanawake wako wengi lakini kwa sasa kumpata mwanamke wa aina ya mama Eliud ni ngumu sana, kama unavyojua mke wangu baada ya kumaliza chuo alipangiwa lramba na tulikuwa kwenye mchakato wa yeye kuhamia hapa Moro, siku zote za maisha yetu, mimi nikipata likizo ilikuwa naenda lramba na yeye akipata likizo anakuja, kama unavyojua mwisho wa mwaka shule zimefungwa yeye kaja,” alisema kwa majonzi huku akielezea familia inajipanga ili kuona namna ya kuufikisha msiba huo kwa mama yake mzazi.

Baadhi ya waombolezaji ambao ni marafiki na jamaa wa karibu wa wafiwa, walielezea masikitiko yao juu ya msiba huo uliotokea ghafla bila kutarajiwa na kuahidi kuwa bega kwa bega na familia hiyo katika kipindi hiki kigumu.

Janeth alizikwa Jumapili iliyopita katika Makaburi ya Kolla mjini hapa baada ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Iramba kwa kushirikiana na uongozi wa shule yake,  kuusafirisha mwili huo kutoka Singida hadi Morogoro.

Waone Wolper na Harmonize Wakidendeka Live Jukwaani


 

Comments are closed.