Tigo yakera wateja wake

tigo
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya simu ya mkononi ya Tigo wikiendi iliyopita iliwakera wateja wake baada ya huduma zao kutoweka ghafla hewani bila taarifa na kusababisha usumbufu mkubwa, uliowafanya waiombe serikali kuiwajibisha.

Huduma zote zinazotolewa kupitia mtandao wa kampuni hiyo zilisitishwa kuanzia majira ya saa nne asubuhi Jumapili iliyopita na hazikurejea hadi alfajiri ya Jumatatu.

Wateja mbalimbali waliopiga simu chumba cha habari cha gazeti hili, walilalamikia hali hiyo, wakisema lilikuwa ni hujuma, kwani hawakuelewa kitu gani kilisababisha huduma za Tigo pekee kutopatikana, wakati mitandao mingine ilikuwa ikipatikana.

“Hii ni hujuma, watu tulikuwa na shughuli nyingi tulizokuwa tukitegemea huduma ya simu, lakini hatukuweza kuwasiliana. Mimi nilipotezana na mgeni wangu ambaye alikuwa hajawahi kufika Dar es Salaam, sasa hata sielewi nitampata wapi,” alisema Jovin Paul, aliyepiga simu akitokea Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Wateja hao waliitaka Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kuiwajibisha kampuni hiyo ya simu ili iwe fundisho kwa mitandao mingine ambayo hujiamulia mambo yake bila taarifa kwa watumiaji wa bidhaa zao.

Gazeti hili lilimtafuta Ofisa habari wa Tigo, John Manyancha ili kutoa ufafanuzi wa nini kilitokea, lakini badala ya kujibu aliomba apatiwe anuani ya baruapepe apate kujibu kupitia huko. Alipopewa, baadaye alituma taarifa iliyoonekana kutoka kwa Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Diego Gutierrez.

Katika taarifa hiyo kwa vyombo vya habari, meneja huyo aliomba radhi kwa wateja wake kutokana na tukio hilo, akidai lilisababishwa na sababu zilizo nje ya uwezo wa kampuni, kwani mkongo wa taifa ulikatika sehemu tofautitofauti.

Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Mkurugenzi wa TCRA, Ali Yahya Simba na ofisa habari wake, Innocent Mungi, lakini wote hawakupatikana kwa maelezo kuwa walikuwa nje ya nchi katika mkutano muhimu barani Ulaya.

Msaidizi wa Mungi, aliyetajwa kwa jina moja la Mwakianjala, alisema asingeweza kuzungumzia hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya kampuni hiyo ya simu, kwani jukumu hilo ni la mkurugenzi pekee.


Loading...

Toa comment