Tigo Yatoa Kompyuta 20 Chuo Kikuu cha Sayansi Mbeya

Mkurugenzi wa Tigo Nyanda za juu Kusini, Henry Kinabo (katikati) akimkabidhi Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), Profesa Aloys Mvuma, moja ya kompyuta 20 zilizotolewa kama msaada kwa chuo hicho.

KATIKA juhudi za kuchangia malengo ya serikali ya kuboresha na kuinua viwango vya elimu katika taasisi za elimu ya juu, kampuni inayoongoza katika maisha ya kidigitali nchini Tanzania, Tigo, imekabidhi kompyuta za mezani 20, zitakazowanufaisha wanafunzi 4,630 katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).
Akibidhi kompyuta hizo katika chuo hicho, Mkurugenzi wa Tigo, Nyanda za juu Kusini, Henry Kinabo, alisema: “Tunaamini ya kwamba kompyuta tunazozitoa hapa leo, zitachangia sehemu kubwa katika kubadilisha jinsi wanafunzi wanavyosoma na pia zitaleta nafasi kwao kubuni teknolojia mpya na kuchangia katika ukuaji wa uchumi nchini Tanzania.
“Tigo ipo mstari wa mbele kwa ajili ya kuboresha viwango vya elimu katika vyuo vikuu kwa kuleta nyenzo za kusomea na kuwasaidia wanafunzi na walimu kukuza vipengere muhimu vinavyohitajika katika karne hii ya 21.”
Aliendelea kuelezea zaidi kwamba kupitia mchango huo, Tigo imeunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania katika mtazamo wake wa kubadilisha nchi kuwa ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ambapo teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ndio chachu ya maendeleo hayo.
Mnamo mwaka 2017, Tigo ilichangia kompyuta 47 katika Chuo Kikuu cha Dodoma, zilizowanufaisha wanafunzi takriban 36,150. Mpaka leo jumla ya wanafunzi 40,780 katika vyuo vikuu nchini wamenufaika na msaada wa kompyuta kutoka Tigo kwa kipindi cha miaka miwili sasa.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST), Profesa Aloys Mvuma, aliipongeza kwa mchango wao kwa kusema: “Ni kupitia ushirikiano huu ndio tutaweza kutoa stadi za kisasa za TEHAMA na maarifa kwa kizazi kijacho cha wataalam ili nchi iweze kukidhi mahitaji ya taarifa zinazobadilika mara kwa mara na mitindo ya kidigitali katika jamii na uchumi wa dunia.”
Aidha,  mkuu wa idara ya Sayansi na Elimu za Ufundi, Dkt. John. P. John, aliwashukuru Tigo kwa msaada huo na alisema kompyuta hizo zitasaidia kuboresha kiwango cha elimu mkoani Mbeya.
“Tunawashukuru Tigo kwa kusaidia juhudi za serikali kwa kutoa mchango wa vifaa vya kufundishia masomo ya TEHAMA katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST). Tunaamini kwamba hizi kompyuta zitaboresha jinsi wanafunzi wanavyosoma na pia zitaongeza ueledi katika elimu ya kidigitali hapa Chuoni.”

Loading...

Toa comment