The House of Favourite Newspapers

Tigo yatoa ofa simu za kisasa zenye vifurushi vya intaneti maonyesho ya sabasaba

Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael (kushoto) akiuzungumza na waandishi wa habari juu ya udhamini wao katika maonyesho hayo.
Meneja wa Ukuzaji wa Biashara wa Tantrade, Stephen Koberou (kushoto) akizungumza jambo.

 

KAMPUNI inayoongoza kwa mageuzi ya kidigitali ya Tigo ambayo ndiyo mdhamini mkuu wa mawasiliano katika Maonyesho  ya Kimataifa ya Biashara (DITF) yanayofanyika jijini Dar es Salaam ambayo niya 42  yanayoandaliwa na Mamlaka ya Ukuzaji wa Biashara Tanzania (Tantrade) imewataka Watanzania kujiandaa kupokea ofa kabambe za simu za kisasa zenye ofa murua za
vifurushi vya intaneti kwa kipindi hiki cha msimu wa sabasaba.

 

 

Akitambulisha udhamini huo jijini Dar es Salaam leo, Meneja Mawasiliano wa Tigo, Woinde Shisael alisema kuwa hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Tigo kudhamini maonesho hayo. Ushirikiano huu ni sehemu mojawapo ya azma ya Tigo kuchangia juhudi za serikali kukuza biashara kama njia mojawapoya kukuza uchumi wa viwanda nchini.

 

 

Kila mwaka kwa kipindi cha miaka 42 sasa, Maonyesho ya Kimataifa ya Dar es Salaam ya Biashara (DITF) yamekuwa chachu kubwa ya kukuza uchumi wa viwanda kwani yanatoa fursa kubwa kwa wafanyabiashara wakubwa, wadogo na wa kati kuonyesha ubunifu katika bidhaa na huduma, pamoja na teknologia mpya kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi. Vilevile, Sabasaba ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwani inatoa fursa za ajira na mapato kwa sekta tofauti,’ Woinde alisema.

 

 

Amewataka  Watanzania kujiandaa kupokea ofa kabambe za simu za kisasa zenye ofa murua za
vifurushi vya intaneti kwa kipindi cha hadi miezi sita kutoka Tigo.

 

 

‘Tumeingia ubia na watengenezaji wakubwa wa simu duniani kama vile Tecno, Samsung na Nokia kuhakikisha kuwa wateja na wananchi
watakaofika katika viwanja vya Sabasaba, Dar es Salaam au katika maduka yote ya Tigo nchi nzima wanafaidika na simu janja kwa bei nafuu kuanzia Shilingi elfu 69,000 pekee katika msimu huu wa Sabasaba.’

 

 

Meneja wa Ukuzaji wa Biashara wa Tantrade, Stephen Koberou akizungumzia udhamini huo ameishukuru Tigo kwa kuchukua jukumu la kuthamini maonyesho ya mwaka huu ya Sabasaba ili kukuza biashara huku akihamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kujionea ubunifu na teknologia mpya, kujifunza, kujenga mahusiano mapya ya kibiashara pamoja na kuwa sehemu ya fursa kubwa zaidi ya kufanya manunuzi na kupata huduma muhimu kwa bei nafuu.

 

Kauli mbiu ya maonyesho hayo maarufu kama Sabasaba ni ‘Ukuzaji wa Biashara kwa Maendeleo ya Viwanda’ na yalianza Juni 28 ambapo yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi Jumatatu ya Julai pili na yatahitimishwa Julai 13, mwaka huu.

 

 

Comments are closed.