The House of Favourite Newspapers

TIMBWILI LAIBUKA KANISA KATOLIKI

0

HALI ya utulivu bado ni tete kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Mikaeli, Kawe, jijini Dar es Salaam, baada ya hivi karibuni waumini kuzua timbwili zito, Risasi linakuhabarisha.  Chanzo kiliwaambia waandishi wetu kuwa vurugu za waumini hao ni mwendelezo wa kupinga uongozi na uamuzi wa Padri Nicholas Bahati Kundy wa parokia hiyo. Inaelezwa kuwa, hivi karibuni padri huyo ambaye pia ni Paroko wa kanisa hilo aliamua kuifuta Jumuiya ya Mtakatifu Stephano iliyo chini ya parokia hiyo kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi.

Sambamba na Jumuiya hiyo kufutwa, padri Kundy pia alimvua uongozi wa Jumuiya ya Mtakatifu Stephano, Samweli Mgila kwa madai ya kushiriki tafrani na matukio yaliyotokea parokiani hapo siku za nyuma. Uamuzi huo wa paroko Kundy uliamsha upya mvutano kati yake na baadhi ya waumini wa parokia hiyo ambayo kwa muda mrefu wamekuwa wakimtuhumu padri huyo kwa mambo mengi kama ufisadi.

“Kanisa Katoliki limekuwa kama siasa na sisi tumefanywa kama maiti. “Padri (Kundy) alisema mtu aliyekufa hawezi kufufuka, ila sisi Jumuiya ya Stephano bado tupo hai, pamoja na kwamba tumetengwa na padri,” alisema Samweli Mgila, mwenyekiti aliyeondolewa uongozini kupitia barua ya Desemba 19, mwaka jana.

Muumini mwingine wa Jumuiya hiyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alipinga jumuiya yao kufutwa na kuongeza kuwa: “Namsifu Padri Mtura (aliwahi kutumikia parokia ya Kawe) ambaye alijenga Kanisa hili na ukuta, lakini alishtumiwa kuzaa, akasemwa, akaonywa yakaisha. “Lakini huyu (Kundy) hataki kuonywa, anafikia hatua ya kufuta jumuiya yetu, sisi twende wapi?

“Mimi nimekaa hapa toka mwaka 79 (1979) na kanisa hili limezaa makanisa mengi, leo kanisa linavurugika kirahisi tu.” Naye Mwenyekiti Msaidizi wa Kanda ya Mtakatifu Petro ambayo ndiyo mlezi wa Jumuiya ya Mtakatifu Stephano iliyofutwa aliyejitambulisha kwa jina moja la Ester, alipoulizwa na waandishi wetu kuhusu mgogoro huo na sababu za kufutwa Jumuiya alisema:

“Mimi siyo mhusika mkuu wa uamuzi huu, aliyefuta Jumuiya siyo mimi, sisi kama Kanda tulienda kwa Padri (Kundy) kuuliza tukaambiwa Jumuiya ya Stephano haipo tena. “Padri alisema kama kuna mtu haelewi aende ataeleweshwa.” Hata hivyo sintofahamu kubwa ilitokea kati ya wanajumuiya iliyofutwa na uongozi wa Kanda hadi kusababisha kutokea kwa zogo na kurushiana maneno makali miongoni mwa waumini.

Kwa upande wake padri Kundy alieleza katika barua yake kuwa anatekeleza sehemu ya maelekezo yaliyotolewa na Askofu Mkuu Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Thaddeus Ruwa’ichi.

“Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam ameagiza kuwa yeyote anayejijua alishiriki katika tafrani/ matukio yaliyotokea hapa parokiani Kawe, ajue kwamba kutokea siku ya leo siyo kiongozi tena wala hawezi kuchaguliwa kuwa kiongozi katika ngazi yoyote ya jumuiya, kanda, parokia hata vyama vya kitume, endapo yeyote atakuwa amesahau tutamkumbusha,” ilisema sehemu ya barua ya kumvua uongozi mwenyekiti Samweli ambayo waandishi wetu waliiona.

Oktoba 6, mwaka jana Paroko Kundy alizuiliwa na baadhi ya waumini wake kuendesha ibada kwa tuhuma za kukosa weledi kwenye kazi yake jambo ambalo mwenyewe amelipinga.

Novemba 4, mwaka huu, waumini wa parokia waliodai kupinga uongozi wa Paroko Kundy kupitia kwa Samweli Mgila Mwenyekiti wa Kamati ya Ufuatiliaji na David Kulwa aliyejitambulisha kwa cheo cha Katibu wa Kamati ya Ufuatiliaji, walitoa waraka kwa waandishi wa habari uliokuwa na tuhuma sita dhidi ya Paroko Kundy.

Tuhuma hizo ni; Mosi, Padri Kundy amekuwa na tabia ya kufichua hadharani siri za sakramenti ya kitubio. Pili, Padri Kundy amekuwa na tabia ya kufuta chaguzi za Jumuiya ndogo ndogo pale wanapochaguliwa waumini ambao yeye hawapendi.

Tatu, padri huyo amekuwa na tabia ya kuendesha shughuli za Parokia bila kushirikisha vyombo vya ushauri vilivyo chini ya Halmashauri ya Walei. Nne, Padri amekuwa na tabia ya kutumia sadaka ya Parokia kinyume cha bajeti ya Parokia iliyopitishwa na Kamati ya Uchumi na Fedha ya Parokia.

Tano, Padri Kundy amekuwa na tabia ya kutoa huduma ya sakramenti ya ndoa kwa kutoza gharama kubwa zaidi kuliko viwango vilivyopitishwa na Sita, padri huyo amekuwa na tabia ya kushindwa kutoa huduma ya misa ya mazishi kwa waumini wake pasipo sababu za msingi.

Mgogoro huu wa Parokia ya Kawe unafahamika kwenye ngazi za jimbo na kwamba mara kadhaa umekuwa ukisuluhishwa bila mafanikio. Waandishi wetu walipomtafuta Askofu Ruwa’ichi, hakuweza kupatikana mara moja kufafanua nini suluhisho la mgogoro huo wa parokia ya Kawe.

 

MEMORISE RICHARD NA KHADIJA BAKARI

.

Leave A Reply