The House of Favourite Newspapers

TIMU YA TANZANIA YAANZA VIBAYA AFCON

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imeanza vibaya michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon 21019) inayoendelea nchini Misri baada ya jana Jumapili kufungwa mabao 2-0 na Senegal.

Katika mchezo huo wa Kundi C uliochezwa kwenye Uwanja wa June 30 uliopo Cairo, Misri na kuchezeshwa na Mtunisia, Sadok Selmi, Taifa Stars ilicheza kwa nidhamu kubwa licha ya kuzidiwa uzoefu na wapinzani wao.

 

Senegal ilijipatia bao la kwanza dakika ya 28 kupitia kwa Keita Baldé Diao wa Inter Milan ambaye alitumia uzembe wa walinzi wa Taifa Stars, huku Krépin Diatta wa Club Brugge KV akifunga bao la pili dakika ya 65 kwa shuti kali nje ya eneo la hatari baada ya kuuwahi mpira wa kona uliookolewa na John Bocco.

 

Licha ya Taifa Stars kupoteza mchezo huo, lakini kazi kubwa ilifanywa na kipa Aishi Manula ambaye aliokoa michomo mingi iliyooelekezwa langoni mwake.

Taifa Stars ilionekana kutokuwa na utulivu mkubwa hasa kwenye safu ya kiungo ambapo mapema Kocha Emmanuel Amunike alimtoa Feisal Salum na nafasi yake kuchukuliwa na Farid Mussa ingawa mabadiliko hayo hayakusaidia kitu. Baada ya mchezo huo, Alhamisi ya wiki hii Taifa Stars itapambana na Kenya, kisha Julai Mosi itamaliza hatua ya makundi kwa kucheza dhidi ya Algeria.

Kikosi cha Taifa Stars: Aishi Manula, Gadiel Michael, Hassan Kessy, Kelvin Yondani, David Mwantika, Feisal Salum/ Farid Mussa, Himid Mao, Mudathir Yahya/ Frank Domayo, Mbwana Samatta, Simon Msuva/ Thomas Ulimwengu na John Bocco.

 

Kikosi cha Senegal: Edouard Mendy, Moussa Wagué, Youssouf Sabaly, Kalidou Koulibaly, Salif Sané/ Cheikhou Kouyate, Badou Ndiaye, Ismaïla Sarr, Idrissa Gueye, M’Baye Niang/ Moussa Konate, Krépin Diatta, Keita Baldé Diao/ Sada Thioub.

Comments are closed.