Tinampay Atua Dar, Amuhofia  Pialali

Arnel Tinampay alivyotua Dar.

Arnel Tinampay raia wa Ufilipino tayari ametua nchini kwa ajili ya pambano lake na Mtanzania, Idd Pialali huku akitamka wazi mpinzani wake ana uwezo mkubwa wa kutembea ndani ya ulingo lakini haiwezi kumtisha.

Bondia huyo amewasili nchini jana Jumamosi kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya pambano hilo litakalopigwa Novemba 28, mwaka huu kwenye Ukumbi wa Next Door Arena uliopo Masaki jijini Dar.

Pambano hilo ambalo linadhaminiwa na Gazeti la Spoti Xtra, +255 Global Radio, DSTV, Plus TV, Uhuru Fm, Clouds Media, Precision Air, Smart Gin na Kebby Hotel.

 Tinampay alisema kuwa amekuja nchini kwa kazi moja ya kuhakikisha anampiga Pialali mbele ya Watanzania huku akiri mpinzani wake ana uwezo mkubwa wa kutembea ndani ya ulingo jambo ambalo anapaswa kuwa nalo makini.

“Hii ni mara pili kuja hapa, nimecheza na Mwakinyo (Hassan) yeye alikuwa bora kwa sababu ya ngumi zake zina nguvu lakini sasa nataka kumpiga Pialali mbele ya mashabiki wake wa hapa.

Arnel Tinampay akiwa na Mhariri wa Gazeti la Championi Jumamosi, Lucy Mgina.

“Pialali ni bondia mzuri, nimeangalia baadhi ya mapambano yake nimeona kwamba anajua sana na mzuri wa kutembea ulingoni akiwa ana pambana lakini hilo haliwezi kunitisha kabisa kwa sababu nimejiandaa vizuri,”alisema Tinampay.

Kwa upande wa tiketi za pambano hilo zinauzwa kwa Sh 20000 mzunguko, Sh 5000 kawaida na Sh 100,000 kwa VIP huku zikipatikana kupitia Nilipe App, maduka ya Vunja Bei Store na Vunja Bei Toto Sinza, Shishi Food  (Kinondoni), pia Cake City  ya Salasala.

 Sehemu nyengine ambazo  tiketi zitakuwa  ni Kaites Lounge ambayo inapatikana Tabata na Dickson Sound ya Magomeni.

Arnel Tinampay akiwa na mwandishi wa Championi, Ibrahim Mussa.

Mbali ya  pambano hilo  mapambano mengine ya utangulizi ambapo Adam Chiga anatarajia kucheza dhidi ya Adam Kipenga wakati Ramadhan Shauri akitarajia kucheza dhidi ya Salehe Mkalekwa.

 Lakini mkongwe Japhet Kaseba yeye atakata ubishi na mkali mwingine Iman Mapambano, Seleman Kidunda kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ‘JWTZ’  yeye ataonyesha ubavu na mkongwe Said Mbelwa wakati Ismail Galiatano kutoka pia JWTZ atazichapa na Mustafa Doto.  Kwa upande wa kinadada bondia Stumai Muki atamaliza ubishi dhidi ya mkali Lulu Kayage.

Toa comment