The House of Favourite Newspapers

TISHIO LA AL -SHABAAB, HARMONIZE ULINZI MKALI SUDAN

DAR ES SALAAM: Achana na ule ulinzi wa kawaida wa mabaunsa wanne ambao amekuwa akiutumia nchini Tanzania, mkali wa Bongo Fleva, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ amejikuta akiwekewa ulinzi wa kufa mtu huko Juba, Sudan Kusini, Gazeti la Ijumaa limenyetishiwa.

Kwa mujibu wa timu aliyoambatana nayo, ulinzi huo ni kufuatia kuwepo kwa tishio la kiusalama hususan kutoka kwa kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab.

Mkali huyo anayesumbua na Wimbo wa Saula alioshirikiana na Lava Lava, alitinga nchini humo hivi karibuni kwa ajili ya kufanya bonge moja la shoo katika Viwanja vya Nyakuruon Cultural Center vilivyopo Juba nchini Sudan Kusini na ndipo waandaaji walipomuandalia ulinzi huo mzito wa jeshi la polisi.

FULL SILAHA ZA KIVITA

Mitandao ya nchini humo imetupia picha mbalimbali za ulinzi huo wa Harmonize ambapo zilionesha askari polisi wakiwa na silaha nzito za moto wakihakikisha hakuna mtu anayeweza kumsogelea na kumdhuru huku wengine wakiwa wamejichanganya na raia wakati walipompokea uwanja wa ndege.

FULL ‘ESKOTI’ YA WAJEDA

Kama hiyo haitoshi, siku ya shoo ilipowadia alipokuwa akielekea uwanjani, mbali na polisi wa kawaida kuwepo kwenye msafara, alisindikizwa na wanajeshi wa nchi hiyo ambao walionekana kushikilia mitutu mizito zaidi kuhakikisha anafika salama viwanjani.

AL SHABAAB NDIYO CHANZO

Mitandao mbalimbali nchini imeeleza kuwa, waandaaji wa shoo hiyo, M-Mgurush Mobile Money, walimuwekea ulinzi huo Harmonize kufuatia kuwepo kwa mashambulio ya mara kwa mara YA Al Shabaab nchini humo.

“Ilikuwa ni lazima awekewe ulinzi mzito kama huu maana inakumbukwa ni mapema tu mwaka huu kulitokea shambulio baya la Al-Shabaab hivyo hatukuwa na uhakika wa asilimia mia moja kuwepo kwa usalama,” ilieleza taarifa ya waandaji wa shoo hiyo.

SHOO YAANZA MAPEMA

Kutokana na sababu hizo za kiusalama, Serikali ya nchi hiyo iliamuru shoo hiyo ianze mapema ili iwahi kuisha ambapo ilianza majira ya saa 12:00 jioni na kumalizika majira ya saa 3:00 usiku.

SHOO SI YA NCHI HII

Kuonesha kwamba kila kunapokuwepo na mwakilishi wa Kundi la Wasafi Classic Baby (WCB) huwa kunakuwa na balaa si la kitoto, bwa’mdogo huyo kutoka umakondeni mkoani Mtwara, Tanzania, aliangusha bonge moja la shoo jukwaani.

Aliimba nyimbo zake zote kali ikiwemo Kwangwaru alioimba na bosi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ambao uliibua shangwe la hatari ambapo mamia ya watu waliokusanyika kwenye viwanja hivyo waliimba naye mwanzo hadi mwisho.

FULL KUWARUSHA STIMU

Akiwa jukwaani, mkali huyo kutoka WCB alitumia staili ya kuimba kisha kukata muziki na kujifanya kama anataka kuondoka hivi, jambo ambalo lilisababisha mashabiki wapige kelele za kumzuia asiweze kuondoka uwanjani hapo.

Hata hivyo, mkali huyo alizidi kuwapagawisha kwa kurudi fasta na kupiga ngoma mpya jambo ambalo liliwafanya mashabiki wazidi kuchanganyikiwa kwa furaha isiyokuwa na mfano.

POLISI WAPATA KAZI YA ZIADA

Video mbalimbali zilizorushwa kwenye mitandao hiyo zilionesha jinsi ambavyo polisi walifanya kazi ya ziada kuwazuia mashabiki waliokuwa na mzuka wa kutaka kusogelea jukwaa, jambo ambalo lilimfanya Harmonize kuwakemea polisi mara kwa mara.

“Msiwabugudhi mashabiki wangu tafadhali, waacheni wajiachie,” alisikika Harmonize kwa lugha ya Kimombo a.k.a yai.

AWASHUKURU WASUDANI

Baada ya kumaliza shoo hiyo, Harmonize aliwashukuru mashabiki wa nchi hiyo na kuahidi kurejea tena nchini humo kufanya balaa lingine kwani ameamini ni nchi salama na hakuna tishio lolote la kigaidi kama ambavyo ilikuwa ikielezwa.

NI HISTORIA NYINGINE…

Kwa siku za hivi karibuni, vijana wa WCB; Harmonize, Lava Lava, Rayvany na wengineo wamekuwa wakifanya maajabu katika shoo za uwanjani kwa kujaza watu na kuporomosha shoo zinazoweka historia katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Comments are closed.