TISHIO MAUAJI WALINZI DAR!

DAR ES SALAAM: SHABAHA ya jambazi kumvizia mlinzi na kumjeruhi au kumuua ni ili aweze kupora mali; inapotokea akafanya hivyo halafu asiibe chochote huacha maswali tata na tishio miongoni mwa jamii; Ijumaa Wikienda lina mkasa mzito.

 

Vyanzo vya habari kutoka Mtaa wa Yange Yange, Msongola, Ilala jijini hapa vinaeleza kuwa hivi karibuni katika maeneo hayo walinzi wawili wameuawa na muuaji kutokuiba kitu huku tukio jipya likitokea Mei 2, mwaka huu kwa mlinzi wa Kampuni ya Lina Millis, Michael Samweli kuuawa kinyama kwa kukatwa shingoni na kitu chenye ncha kali.

 

HUYU HAPA MWENYEKITI WA MTAA

Akizungumza na Ijumaa Wikienda mwenyekiti wa mtaa huo, George Ghati alisema:

“Kinachotia hofu ni huyu muuaji kutoiba kitu, tunajiuliza anataka nini kufanya mauaji hayo?

“Aprili 11, mwaka huu, kuna mlinzi aliuawa kwa bwana mmoja anaitwa Kyaro, staili ni hiihii ya kuchomwa visu na muuaji kutokomea bila kuiba chochote.

“Leo nazungumzia mauaji ya Samweli ambaye ameuawa na huyu mtu asiyejulikana, jambo hili linasikitisha sana,” alisema

mwenyekiti huyo wa mtaa.

SAMWELI ALIUAWAWAJE

Inaelezwa kuwa, siku ya tukio kama kawaida yake mlinzi huyo alifika eneo lake la kazi na kuanza kutekeleza majukumu yake lakini majira ya saa nane usiku alivamiwa na mtu asiyejulikana na kuuawa kikatili.

Akizungumza na Ijumaa Wikienda, Mkurugenzi wa Kampuni ya Lina Millis, Joyce Kimaro, ambaye ni mwajiri wa Samweli alisema:

“Siku hiyo kulikuwa na vijana wawili waliokuwepo usiku kwenye kiwanda changu cha kusaga nafaka ambapo walivamiwa na huyo muuaji.

 

“Alipoingia alimjeruhi kijana wa kwanza akamuacha anavuja damu, akamfuata mlinzi wangu mwingine na kuanza kumshambulia kwa kumchoma visu shingoni.

“Mimi sikuwepo lakini nilipigiwa simu na kuambiwa juu ya tukio hilo, nilipofika kwa kuwa tumefunga kamera za CCTV, ikabidi tuangalie video zilizochukuliwa, inaonyesha kwenye mida ya saa nane usiku, kijana wangu mmoja alitoka upande wa uzalishaji akielekea chooni.

 

“Wakati anaenda alikutana na huyo muuaji, alipambana naye kidogo lakini baadaye alichomwa kisu.

“Akawa anavuja damu, yule muuaji akajua ameshamuua akamchukua na kumficha chini ya gari kisha kumfunika kofia mdomoni halafu akamvua ovaroli akalivaa yeye.

“Baada ya hapo aliingia ndani, lakini kwa kuwa huko hakukuwa na kamera tukio alilofanya halikurekodiwa, alimvamia mlinzi na kumuua kisha baadaye kutoka.”

 

MASHUHUDA WASIMULIA

Shuhuda mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake aliliambia Ijumaa Wikienda kwamba majirani wakiambatana na polisi walifika eneo la tukio na kumkuta kijana mmoja akiwa amejeruhiwa vibaya huku Samweli akiwa ameuawa.

Alisema baada ya hapo polisi waliondoka na mwili wa marehemu huku majeruhi akipelekwa hospitali ya Zakhiem, Mbagala kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

 

KAMANDA WA POLISI AFUNGUKA

Naye Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Mussa Taibu alisema kuwa bado wanaendelea na uchunguzi kufuatia tukio hilo.

“Bado tunaendea na uchunguzi kwa kuwa muuaji anaonekana kwenye video zilizochukuliwa na kamera tunaimani kubwa kupitia kielelezo hicho tutafanikiwa kumnasa mtuhumiwa wa mauaji hayo na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria,” alisema kamanda Taibu.

 


Loading...

Toa comment