The House of Favourite Newspapers

Simulizi ya Filamu ya Titanic 01

0

Hii ni kazi mpya kabisa ambayo itakuwa ikikueletea simulizi za filamu mbalimbali jinsi zilivyo kwa mtindo wa kuhadithia kila kitu mpaka mwisho. Kwa kuanza, tunaanza na filamu ya Titanic iliyoigizwa mwa 1997 na waigizaji kama Leonardo DiCaprio ‘Jack’ Kate Winslet ‘Rose’ na wengine wengi.

Rose akichorwa.

Filamu inaanza kwa kuonyesha vyombo maalumu vikiwa vimekwenda chini ya maji kutafuta mabaki ya meli kubwa ya Titanic iliyozama mwaka 1912 katika Bahari ya Atlantiki iliyokuwa ikitokea katika Jiji la Southampton na kwenda New York nchini Marekani.
Vyombo vile vimezama mita nyingi chini, vikakutana na meli hiyo na kuanza kuitazama. Walitaka kujua vitu vingi kuhusu meli hiyo ambayo historia yake iliandikwa miaka ya nyuma. Vyombo vile vimeikuta meli hiyo ikiwa chini kabisa na kuanza kuizunguka huku ikiipiga tochi.
Hali ya chini ya maji inatisha, milio ya ajabu inasikika kwa mbali, maji yanaonekana kutulia japokuwa kwa kina kirefu kama hicho amani inaonekana kuwa ndogo.
Japokuwa ulikuwa ni mchana lakini chini ya maji kulikuwa na giza kana kwamba ilikuwa usiku. Vyombo vile viliendelea kuzunguka kila kona katika meli ile kabla ya kuzama ndani kabisa. Wataalamu wale walikuwa wakiiangalia kupitia katika vidirisha vidogo vya vyombo walivyokuwa ndani yake.
“Nyamazeni, bado tunataka kusikia pia,” alisikika bosi wa watu hao aliyeitwa Brock akiwaambia wenzake waliokuwa wakifuatilia kwenye kidirisha ndogo katika chombo maalumu walichokuwamo.
“Naiona inatokea kutoka gizani kama meli ya kishetani,” alisema Lewis kwa sauti ya chini kabisa huku mwenzake akiwa ameshika kamera iliyokuwa ikipiga kwa nje kulipokuwa na meli hiyo.
“Hii meli ilizama saa 8:30, usiku wa tarehe 15/4/1912 baada ya kuelea kwa muda mrefu kutoka juu ya maji,” alisema Brock huku akiangalia nje.
“Hahah! Unajua bosi wewe ni kama mjinga sana,” alisema Lewis kiutani huku akicheka. Wote wakaanza kucheka akiwepo bosi huyo.
Kumbuka kwamba hao ni wanasayansi lakini pia ni watu waliokuwa wakifuatilia mambo mengi yaliyokuwa yamepita. Kwa kipindi hicho walihitaji kujua kuhusu meli hiyo, nini kilitokea mpaka kuzama yote na kuua watu wengi kiasi hicho?
Vyombo vile viliendelea kuizunguka meli ile na wakati mwingine kuingia ndani. Walitaka kuona kila kitu kilichokuwa ndani ya meli hiyo. Hawakutaka kuondoka, kitendo cha kuiona meli hiyo kilimaanisha kwamba ni mwanzo wa mafanikio waliyokuwa wakiyahitaji kipindi hicho.
“Tumekwishafika katika meli ya Titanic. Maili mbili na nusu chini ya bahari, mita 3821, presha ya huku chini ni kubwa mno,” alisema Brock.
Kwa kuwa vyombo walivyokuwa navyo vilikuwa vikubwa na visingeweza kufika ndani kabisa, walichokifanya ni kuagiza chombo kingine na kwenda kuzunguka ndani ya vyumba vya meli hiyo ili kuona kile kilichokuwa humo ndani.
Walivyovikuta humo chini viliwashtua. Walikuta miguu ya watu, miili ya watoto ilikuwa imeliwa sana na samaki, picha ya humo baharini iliwatisha sana. Walikwenda mpaka walipokuta sehemu iliyokuwa na mlango
“Huo ni mlango, pitisha chombo kwenye huohuo mlango,” alisema Brock.
“Haina shida. Wewe tulia tu wala usijali bosi,” alisema Lewis.
Chombo kile kikaingia ndani kabisa ya chumba hicho na kuendelea kupiga picha kila kitu kilichokuwa humo ndani. Wakaingia katika chumba kimoja kilichoonekana kuwa cha ndani kabisa.
“Tumeingia ndani kabisa,” alisema Lewis mmoja kibonge huku akitabasamu.
“Hicho ni kitanda cha Hockleys. Hapo ndipo yule mwanaharamu alipokuwa akilala,” alisema Brock.
“Ooh! Kuna mtu hakufunga maji…”
“Subiri kwanza. Hebu rudi nyuma kulia.”
Hapohapo kile chombo kikaanza kupelekwa upande wa kushoto ambapo Brock aliuzungumzia.
“Ule pale ni mlango wa kabati, hebu sogea karibu zaidi.”
“Bosi! Unasikia harufu ya kitu chochote?” aliuliza Lewis.
“Nataka nijue kilichokuwa chini ya huo mlango!” alijibu bosi kwa sauti iliyoonyesha umakini mkubwa wa kufuatilia kilichokuwa kikiendelea.
“Naombeni mikono yangu!” alisema Lewis.
Hapohapo akapewa mikono ya chombo kile ambayo iliunganishwa na kile chombo kilichokuwa kimekwenda kule na kuanza kuuinua mlango uliokuwa ukionekana kama umefunika kitu fulani. Mlango ulipotolewa, macho yao yakatua katika sanduku moja kubwa. Kila mtu akabaki akiliangalia kwa mshangao kana kwamba walikuwa wakiangalia kitu fulani cha ajabu sana.
Hawakutaka kuchelewa, huko wakiwa kwenye sura za kutabasamu wakakichukua kisanduku hicho na kwenda nacho kwenye meli yao kwa kuhisi kwamba ndani yake kulikuwa na mali nyingi kama dhahabu, almasi au lulu.
Baada ya kukichukua kisanduku kile, wafanyakazi wote wanaonekana kupongezana, wengine wakawa wanampongeza bosi kwani kazi waliyokuwa wameifanya ilikuwa kubwa mno. Kumbuka kwamba pongezi hizo zote ni kwa sababu hisia zao ziliwaambia kwamba ndani ya kisanduku kile kulikuwa na mali nyingi mno.
“Tumefanikiwa Bobby,” alisema Brock huku akimshika Bobby.
“Nani ni bora? Sema nani ni bora,” Lewis alimuuliza bosi wake huku akimwangalia kwa uso wenye bashasha.
“Wewe hapo Lewis,” alijibu Brock huku naye akicheka kwa furaha.
Kwa kuwa sanduku lile lilikuwa la chuma na isingewezekana kufunguka kwa urahisi, wakaagiza mashine ya kukatia vyumba ili iweze kukata kisanduku kile. Haraka sana mashine ikaletwa na kuanza kuikata.
“Nipe sigara yangu,” alisema Brock.
“Hii hapa,” akapewa haraka sana.
Wakati kisanduku kikiendelea kukatwa, Lewis akachukua shampeni na kuifungua kisha kuanza kumwagia kila mtu mahali pale, yote hiyo ilikuwa ni furaha ya kupata kile walichokuwa wakihisi kwamba ni utajiri mkubwa.
Sanduku likafunguliwa. Karatasi kadhaa zikatoka huku kukiwa na tope jingi. Kila mmoja akashtuka, haraka sana Brock akainama chini na kuingiza mikono yake ndani kwa kuhisi kwamba angeshika mali yoyote ile. Hakukuwa na kitu walichokipata zaidi ya karatasi zilizoonekana kuhifadhiwa kwa kipindi kirefu.
Sura ya Brock ikabadilika, tabasamu likapotea ghafla, hakukuwa na mali yoyote aliyoikuta ndani ya kisanduku kile zaidi ya karatasi zile tu.
“Hakuna almasi?” aliuliza Lewis, bosi bado alikuwa kwenye mshangao mkubwa.
“Bosi! Kitu hikihiki kilitokea kwa Geraldo…” aliendelea kusema Lewis huku akimwangalia bosi wake aliyeonekana kuwa na hasira. Brock akainuka.
“Zimeni kamera,” alisema Brock huku akionekana kuwa na hasira.
Ilikuwa ni lazima kuangalia karatasi zile zilikuwa na nini. Wakazipeleka katika vyombo maalum na kuanza kuzisafisha, baadaye wakagundua kwamba karatasi moja ilichorwa picha nzuri ya mwanamke aliyekuwa amelala kwenye kochi huku akiwa uchi wa mnyama, na shingoni alikuwa na cheni yenye madini ya thamani.

 

Je, nini kiliendelea?
Tukutane kesho hapahapa.

Leave A Reply