The House of Favourite Newspapers

TOKO: NIMEANZA MUZIKI NA DIAMOND, KIBA

Tiko Hassan ‘Tiko’

UKIZUNGUMZIA miongoni mwa wasanii waliotamba kwenye filamu kisha kuingia kwenye Muziki wa Bongo Fleva ni wazi utawataja Snura Mushi, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ bila kumsahau Tiko Hassan ‘Tiko’.  

Tiko amedhamiria kweli kuonyesha kipaji chake baada ya kuachia ngoma tano hadi sasa ambazo ni Shika, Lambalamba, Nawachefua, Washa na Niache ambazo zote zinahusu mapenzi na zinafanya vizuri.

 

Risasi Vibes limekutana naye na kufanya Exclusive Interview na katika mahojiano yake, Tiko anasema kuwa ameanza sanaa siku nyingi sana tangu enzi hizo akiwa na akina Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Ali Kiba ‘King Kiba’ walipokuwa wakihaso ili kufikia malengo.

 

Tiko anasema, amewahi kukaa kambi moja na Queen Darleen, Diamond pamoja na Kiba lakini kutokana na sanaa ya filamu kumuhitaji kwa wakati huo aliamua kukaa pembeni kidogo kabla ya kurudi tena kwenye muziki anaokimbiza hadi sasa. Msikie mwenyewe.

 

Risasi Vibes: Tiko, mwaka huo unaosema ulikuwa na akina Diamond, Kiba na Queen Darleen uliwahi kutoa wimbo wowote ule?

Tiko: Zipo nilizotoa, nakumbuka Bob Juniour alinitungia wimbo na kunipa… nikaimbaimba lakini niliacha na wala kazi hiyo haikufika mbali kiviile. Lakini pia Prodyuza KGT alinirekodia wimbo, nao haukufika popote kwani nilipata mtu ambaye alinishawishi kuingia kwenye filamu ndio nikahamia huko.

 

Risasi Vibes: Sio kama umeona kwenye filamu kumedoda ndio umeamua kuhamia huko kwenye muziki?

Tiko: Hapana siwezi kusema kwenye filamu kumedoda wakati sijawahi kutoa kazi yangu ya mkononi, nimefanikiwa kupewa kazi za watu na kulipwa, ukinipa changu nafanya ‘scene’ kisha naendelea na mambo mengine. Kwa hiyo kuujua ugumu huo si rahisi.

 

Risasi Vibes: Kwa nini sasa ukaamua kuingia kwenye gemu ya muziki kwa sasa wakati kila mtu analia na kazi, huoni kama nao unaelekea kubaya?

Tiko: Niseme tu ukweli, kwenye filamu nimejifunza mengi na ndio maana hasa nikapata hata ujasiri wa kurudi kwenye muziki kwani sasa najiamini kupita kiasi. Naamini nitadumu kwenye gemu kuliko zamani ambapo sikuwa najiamini sana na kwa upande wa filamu kazi napata kama kawaida tu mbona nafaya kazi na Joti na zinaonekana.

 

Risasi Vibes: Wasanii wenzako wakiwa wanaingia kwenye gemu huwa na tabia ya kutafuta kiki ili wafanikiwe kimuziki, wasikike na kutambulika, wakati mwingine huwa wanawashirikisha wasanii wakubwa kutusua, kwako wewe inakuwaje?

 

Tiko: Mimi naamini kwenye kipaji zaidi na riziki, kama Mungu amekuandikia itakuwa tu na kama una kipaji cha kuimba utaimba tu na watu watapokea vizuri kazi yako bila kutafuta kiki yoyote. Najua kazi hujitangaza yenyewe na najiamini nitaweza, kwani natoa kazi nzuri. Iwapo itafikia wakati natakiwa kumshirikisha mtu kwenye kazi, nitamshirikisha lakini si kwa kutafuta jina kubwa.

Risasi Vibes: Ni changamoto gani unakutana nazo kwenye kazi hii ya muziki?

Tiko: Nakosa menejimenti ya kunisaidia ili nifanye mambo mazuri zaidi, maana muziki nao unahitaji bosi wa kuhakikisha anakusaidia kwani mahitaji yake ni mengi na mimi kila kitu nafanya mwenyewe. Natamani ningepata wa kunipa kampani naamini nitafika mbali.

 

Risasi Vibesi: Mbali na muziki unafanya kazi gani ya kukuingizia kipato? Kwani kama unafanya mwenyewe kila kitu kwenye muziki ni lazima uwe na mtaji wa kutosha.

Tiko: Nina Duka la nguo nauza Jinzi na Top, lakini pia nimekuwa nikishona madera ya akina mama kisha nasambaza. Si unajua madera yanatoka hasa ukipata tenda kubwa za wamama wa maharusi.

 

Risasi Vibes: Wewe ni dada mrembo. Je, umeolewa? Umechumbiwa? Au unadanga kama wengine?

Tiko: Haha haha! Mimi ni mama ujue najiheshimu sanasana, nina mtoto wa kidato cha kwanza hivyo siwezi kudanga kamwe. Ila kifupi nipo kwenye uhusiano siriazi.

 

Risasi Vibes: Msanii gani unapenda anavyofanya kazi zake na anakushawishi?

Tiko: Wasanii ni wengi akiwemo Vanessa Mdee, Diamond, Harmonize, Kiba na Ruby.

Makala: HAMIDA HASSAN

Comments are closed.