Tonombe Aziba Nafasi Tatu Yanga
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mserbia, Zlatko Krmpotic, ameonekana kunogewa zaidi na kiungo mkabaji mpya wa timu hiyo, Mkongomani, Mukoko Tonombe na safari hii ameonekana kumpa majukumu mapya kwenye kikosi chake hicho.
Mkongomani huyo ni kati ya wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga katika msimu huu na kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo akicheza michezo yote minne ya Ligi Kuu Bara.
Kutua kwa kiungo huyo mwenye mabao mawili hadi hivi sasa, moja akifunga kwenye ligi, Yanga ilipocheza na Kagera Sugar pamoja ule wa kirafiki dhidi ya Mlandege FC ya Visiwani Zanzibar, kumeonekana kuleta ahueni kubwa.
Staa huyo mpya ndani ya Yanga, awali alianza kwa kuchezeshwa na kocha Krmpotic namba sita, aliyetokea benchi katika mchezo wa kwanza wa ligi walipocheza dhidi ya Tanzania Prisons uliochezwa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kocha huyo alikuja kumbadilisha majukumu ya kucheza katika kikosi chake kwenye mchezo wa pili wa ligi Yanga
ilipocheza dhidi ya Mbeya City kwa kumchezesha namba nane, huku Zawadi Mauya akimchezesha sita na Feisal Salum ‘Fei Toto’ winga namba saba.
Katika mchezo huo, Zlatko alionekana kunogewa na Tonombe jinsi alivyokamilisha majukumu yake ya kuchezesha timu ndani ya wakati mmoja akipunguza mashambulizi kwa Yanga kumiliki mpira na kupiga mipira mirefu kwa washambuliaji.
Mserbia huyo katika mchezo uliopita wa ligi wakati timu hiyo ikicheza dhidi ya Mtibwa Sugar wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro, alimbadilishia majukumu kwa kumchezesha namba kumi akiwa nyuma ya Mghana, Michael Sarpong aliyecheza namba tisa.
Akicheza nafasi hiyo ya ushambuliaji, Tonombe alionekana kutengeneza nafasi za kufunga mabao huku yeye mwenyewe akijaribu kufunga nafasi mbili ndani ya 18, moja ukiwa mpira wa kona uliopigwa na Muangola, Carlos Carlinhos.
Akizungumzia hilo, kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mwambusi alisema kuwa: “Tuliingia uwanjani katika mchezo huo tukiwa na ‘game plan’ ya ushindi ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ya pointi tatu, katika hilo tunashukuru tumefanikiwa tumechukua pointi kwa Mtibwa.
Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam