Top Five Warembo Wanaokimbiza Bongo Fleva
MIAKA ya nyuma warembo kufanya muziki hususan wa Bongo Fleva, ilikuwa ni ngumu kidogo. Walishindwa kushindana na vijana wa kiume. Lakini kadiri miaka ilivyozidi kusonga, wanawake wamekuja juu. Nao wanafanya muziki, tena muziki wao mzuri kweli.
Achana na kina Ray C, Zay B, Sista P na wengineo ambao kwa sasa kama gemu limewatupa mkono, wapo warembo ambao wanafanya vizuri kwa sasa. Wapo ambao wametoa ngoma juzikati lakini wengine wana muda kidogo hawajaachia ngoma lakini bado haiondoi maana kwamba wapo sokoni.
Top Five yetu ya leo ni warembo ambao wanafanya makubwa kwenye ulimwengu wa Bongo Fleva. Wana mashabiki wengi na nyimbo zao zinasikilizwa na wengi:
NANDY
Huyu ndio mama lao. Yes, unaweza kusema kwa sasa mrembo huyu ndiye anayeongoza katika listi ya warembo wanaofanya muziki wa Bongo Fleva. Top Five inathibitisha hilo kutokana na maajabu yake kwenye nyimbo zake zinavyotazamwa na watu wengi YouTube.
Wimbo kama Kivuruge umetazamwa na watu Mil. 10.4, Ninogeshe (Mil. 11.9), Wasikudanganye (Mil. 4.4), Kiza Kinene (Mil. 4) na Hazipo (Mil. 3.5).
RUBY
Huyu alikuwa ndio mshindani mkubwa wa Nandy. Lakini hata hivyo kutokana na sababu zisizojulikana, amejikuta akishuka na kuachwa na Nandy. Lakini hata hivyo si haba, anafanya vizuri kwani Top Five ya Risasi Mchanganyiko imempa nafasi ya pili.
Anao wafuasi wanaomuangalia huko YouTube. Ngoma yake kama Ntade ina watazamaji Mil. 3.2, Na Yule (Mil.6.1), Niwaze (Mil. 3.6) na Nadondosha ambayo ina wafuasi 88,611 walioiangalia.
V MONEY
Udadisi wa Top Five umeweza kubaini mrembo huyu kwa sasa ndiye anayeshika nafasi ya tatu baada ya Ruby kwa kuwa na mashabiki wengi na kusikilizwa. V Money amefanya baadhi ya kolabo na wasanii wa nje ya nchi, lakini wigo wake wa mashabiki umepungua kwa sasa.
Nyimbo zake kwenye YouTube zina followers wachache ukilinganisha na Ruby au Nandy.
Nyimbo zake zipo hivi; kuna Hawajui ambayo ina watazamaji Mil. 1.1, Come Over (332,116), Niroge (Mil. 1.1) na Kisela (Mil. 2.6).
JIDE
Huyu ni legendary kwenye Bongo Fleva. Ameanza kuimba kabla ya warembo wote waliopo kwenye chati hii. Licha ya ukongwe wake, lakini wadogo zake wamemuacha kwenye YouTube. Wana wafuasi wengi kuliko yeye aliyeanza gemu kitambo.
Nyimbo zake Jide zenye watazamaji wengi angalau ni kama ifuatavyo; Ndindindi (Mil. 1.7), Historia (122, 480) na Sawa na Wao (514, 234).
LINAH
Huyu ndiye anakamilisha Top Five yetu kwa siku ya leo. Anajitahidi kufanya poa kwenye gemu la Bongo Fleva na kufanya shoo kadhaa nje ya nchi, lakini bado hafurukuti kwa Nandy na wengineo. Huyu kwenye YouTube anawatazamaji kama ifuatavyo:
Marry You ina watazamaji 163,747, Koleza (Mil. 1.1) na Pepea ambayo ina watazamaji 28,000.