The House of Favourite Newspapers

TP Mazembe yawavaa Stand, yamtaka straika

0

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam

MAMBO yameanza kumnyookea aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Simba ambaye sasa anaitumikia Stand United ya Shinyanga, Elias Maguli baada ya kuanza kunyemelewa na miamba ya soka Afrika, timu ya TP Mazembe ya DR Congo.

Maguli, tangu atue Stand hivi karibuni ameonyesha kuwa na kiwango kikubwa cha kuzifumania nyavu ambapo mpaka sasa ameshaifungia timu hiyo mabao tisa katika mechi 10 alizoitumikia na kuiwezesha kuwa ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu huu ambayo sasa imesimama kwa muda wa wiki sita kupisha maandalizi ya timu ya taifa, Taifa Stars.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya timu ya Stand zimedai kuwa, Maguli hivi sasa yupo katika rada za TP Mazembe ambayo imeanza kumfuatilia kwa karibu kutokana na kuvutiwa na uwezo wake mkubwa wa kuzifumania nyavu aliouonyesha hivi karibuni.

Akizungumza na Championi Jumatano, kiongozi mmoja wa juu wa Stand ambaye ameomba kutotajwa jina lake kwa sababu yeye siyo msemaji wa timu hiyo, alisema kuwa TP Mazembe imetuma ujumbe maalumu klabuni hapo kuhusiana na mshambuliaji huyo.

“Wametuambia kuwa wanamhitaji Maguli lakini kabla ya kumsajili itabidi wamuangalie kwanza kwa karibu katika mechi zetu nyingine za ligi kuu ili waweze kujiridhisha kabla ya kuleta ofa yao.

“Wamedai kuwa kutokana na wachezaji wa Tanzania  wanaoitumikia klabu hiyo, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kuwa na msaada mkubwa klabuni hapo, wanaamini kuwa Maguli naye anaweza kufuata nyayo zao kwa sababu aina yake ya uchezaji haina tofauti na nyota hao,” alisema kiongozi huyo na kuongeza:

“Kutokana na hali hiyo kwa upande wetu sisi hatuna kizuizi chochote ila tunachoomba tu ni utaratibu wa usajili ufuatwe pindi watakapokuwa tayari kufanya hivyo kama wataridhika na kiwango chake.”

Maguli kwa sasa yupo kwenye kikosi cha Taifa Stars ambacho Jumamamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, kitacheza na Algeria mechi ya kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia, mwaka 2018, Urusi.

Leave A Reply