TPF: Tumuunge Mkono Magufuli Vita Dhidi ya Corona

Mwenyekiti wa Taasisi ya Amani Tanzania, Sadiki Godigodi (kulia) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati akielezea taasisi hiyo inavyomuunga mkono Rais John Magufuli katika mapambano dhidi ya janga la Corona. Katikati ni Mkurugenzi wa Siasa na Dini wa taasisi hiyo Alhaji Dk. Sule Seif na kushoto ni Mshauri wa taasisi hiyo, Issa Mkalinga.

TAASISI ya Amani Tanzania (TPF) imesema ni vema wanasiasa nchini wakaungana na Rais John Magufuli na serikali kwa ujumla, kupambana na janga la corona, ambalo halichagui vyama wala dini.

Pia imewaonya wanasiasa, kuacha kugeuza janga hilo kama mtaji wa kisiasa, kufanikisha malengo yao ya kujijenga kisiasa.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkurugenzi wa Siasa na Dini wa taasisi hiyo, Alhaj Dk. Sulle Seif wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala mbalimbali, yanayoendelea nchini, ambapo pia alimpongeza Rais Magufuli kwa msimamo wake usioyumba katika kukabiliana na ugonjwa wa corona.

Dk. Seif alisema wapo baadhi ya wanasiasa, wamekuwa wakitumika kupotosha ukweli wa jambo hilo na kusababisha hofu kwa wananchi, kitu ambacho hakiwezi kumsaidia kutokomeza ugonjwa huu.

Issa Mkalinga (kushoto) akiongea jambo.

Aliwaasa wanasiasa wa aina hiyo, kuacha kupotosha umma na kuleta hofu bali kushirikiana katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Aidha, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Sadiki Godigodi alisema misimamo ya Rais Magufuli katika kukabiliana na ugonjwa huo, imesaidia kuimarisha afya za Watanzania.

Alisema endapo rais angeamua kuwafungia Watanzania wasifanye shughuli zozote, ingeweza kuchangia maafa na ukosefu wa amani zaidi, tofauti na uwepo wa ugonjwa wenyewe, ambao unahitaji umakini kujikinga huku wananchi wakichapa kazi.

 

Sadiki Godigodi (kulia) akisisitiza jambo.

Alisema katika kipindi hiki, Watanzania wengi wametambua kuwa serikali iliyopo madarakani ni ya wanyonge, kwa kuwa imefanya maamuzi, ambayo yamesaidia watu wa kipato cha chini.

Godigodi alisema kwa sasa mataifa mengi duniani, yameanza kutumia mbinu alizozitumia Rais Magufuli katika kupambana na ugonjwa huo.

“Pongezi kubwa kwa Rais wetu kwa kuliona jambo hili mapema na kuamua kutowatesa wananchi licha ya maneno makali ya shutuma. Hivyo kwa sasa kinachohitajika ni ushirikianao na kufuata maelekezo ya wataalamu,” alisema Godigodi.

Akizungumzia hotuba ya Rais Magufuli aliyotoa mwishoni mwa wiki akiwa Chato mkoani Geita, alisema imeamsha ari mpya kwa wananchi wengi, kuanza kufanya kazi kwa kujituma zaidi, tofauti na awali ambako kuna baadhi ya watu walianza kuwakatisha tamaa.

NA MWANDISHI WETU


Loading...

Toa comment