Trace Awards na Azam Media Wasaini Makubaliano ya Kurusha Hewani Tuzo za Trace

Dar-es-Salaam, Kampuni ya Trace Awards na Kampuni ya Azam Media Limited Group imezindua na kusaini mkataba wa makubaliano kwa ajili ya tuzo za Trace kwa ajili ya urushaji matangazo ya usiku wa tuzo hizo ambao utafanyika Februari 26, 2025, The Mora Zanzibar.
Akizungumza na wanahabari Januari, 20, 2025, mwakilishi wa Trace Award Tanzania, Seven Mosha amesema kuwa tuzo hizo zitatoa fursa wa wasanii kujulikana kidunia kwa sababu kuna wasanii ambao wanajulikana Afrika, lakini duniani hawajulikani hivyo basi hii ni fursa kwa kila msanii kushiriki katika tuzo hizo na kura za washindi wa vipengele 26 vya tuzo hizi ambazo zitafungwa Februari 15, 2025.

Nae Yahya Mohamed, Afisa Mkuu wa Mahudhui wa Azam Media, amesema ushirikiano huo utawezesha kurusha tukio hilo moja kwa moja na kuhakikisha ubora wa hali ya juu na amewataka wasanii kushindania tuzo hizo na mashabiki wawapigie kura ili mziki wa wasanii uweze kujulikana zaidi.
Tukio hili linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa wasanii wa Kiafrika na kimataifa kuonyesha umahiri wao na kuchangia ukuaji wa muziki wa Kiafrika kwenye anga za kimataifa.

Mkataba huo umesainiwa na Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Azam Media Limited, divisheni ya Maudhui na Utangazaji Yahya Mohamed pamoja na Mkuu wa maudhui Trace Awards, Valerie Gilles- Alexia ambaye amesema waiona fursa kama uchumi wa buluu hivyo wameona ni vyema ikafanyikia Zanzibar.
Mbali na viongozi hao, walioshuhudia ni Msimamizi Mkuu wa Chaneli ya Sinema Zetu, Sophia Mgaza na mwakilishi wa Trace Awards Tanzania, Seven Mosha.