WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani imeamua kuunganisha nguvu na wasanii hapa nchini ili kufanikisha Tamasha la Wiki ya Nenda kwa Usalama ambalo hapo awali ilipangwa kufanyika leo Jumamosi, Agosti 5, 2017 na baadaye kuahirishwa hadi Jumamosi ijayo Agosti 12 ambapo litafanyika.
Akizungumza na wanahabari pamoja na wasanii wa muziki na wa filamu hapa nchini leo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Eng. Hamad Masauni amesema, lengo la kuwatumia wasanii ni kuihamasisha jamii kuhusu usalama barabarani kwani wasanii wanasikika zaidi na ujumbe wao ni rahisi kuifikia jamii hasa vijana.
“Watanzania wenzetu wamekuwa wakipoteza maisha yao kwa ajali mbalimbali, huu ni mkakati wa awamu ya pili wa wizara, ambao lengo lake kuu ni kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujiepusha na ajali. Na tunategemea kupunguza ajali hizo kwa asilimia 10. Elimu inatakiwa kuanzia kwa madereva hadi kwa wananchi wa kawaida.
“Katika kutoa elimu hii tumeona tuwashirikishe zaidi vijana kwa kuwa ndiyo wadau wenyewe. Wanaoendesha bodaboda sio wazee, ni vijana. Hivyo wanapaswa waeleimishwe vizuri kujikinga na kuepusha ajali hizo. Kauli mbiu yetu ya mwaka huu ni Hatutaki Ajali Tunataka Kuishi Kwa Usalama,” alisema Masauni.
Aidha Masauni amesema tamasha hilo limeahirishwa kutokana na tukio la Kitaifa ambalo limefanyika leo jijini Tanga ambapo Rais John Magufuli na Rais Yoweri Museveni wamezindua ujenzi wa mradi wa mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani, Bandari ya Tanga.
“Siku hiyo, asubuhi tutaanza na Joggig ambayo Rais Mstaafu, Ally Hassan Mwinyi ataongoza ambapo kutakuwa na vikundi mbalimbali vya jogging, brass band, mpira wa miguu ambapo madereva bodaboda na askari wa usalama baranbarani watamenyana na Mgeni Rasmi atakuwa Rais Magufuli” alimalizia Masauni.