TRILIONI 1.2 ZA MENGI NGOMA NZITO JACK, WANAWE WAHURUMIWA

DAR ES SALAAM: UTAMADUNI wa kuandika wosia kwa Watanzania bado haujawaingia akilini watu wengi hivyo jambo hili linafikirisha pia juu ya utajiri mkubwa alionao aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi. 

 

Kwa mujibu wa jarida la Fobes la mwaka 2014, mzee Mengi anashikilia nafasi ya 45 kati ya matajiri 50 zaidi barani Afrika akiwa na utajiri wa takriban Dola za Marekani Milioni 560 sawa na Shilingi Trilioni 1.2.

 

NGOMA NZITO?

Endapo mzee Mengi atakuwa hajaandika wosia na busara ikashindwa kutumika, utajiri huo mkubwa aliokuwanao mfanyabiashara huyo mwenye makampuni ya habari, kiwanda cha vinywaji baridi na madini, unaweza kuwa kaa la moto katika mgawanyo.

 

TUWASIKILIZE WAOMBOLEZAJI

Risasi Jumamosi lilizungumza na baadhi ya waombolezaji waliofika kwenye mazishi ya mzee Mengi katika Kijiji cha Nkuu, Machame mkoani Kilimanjaro ambao waliuelezea utajiri wa mzee huyo hususan baada ya kuona hekalu kubwa aliloliacha marehemu.

 

“Mh! Mwenzangu hapa kazi ipo sio kwa lihekalu hili, angalia na lile alilokuwa anaishi kule Kinondoni Dar, angalia magari ya kifahari kama Mercedes Benz, Toyota Land Cruiser V8 aliyoacha marehemu, bado kuna makampuni ya kuchimba madini, ana kampuni ya vinywaji ukichanganya na vyombo vya habari sasa ngoma lazima iwe nzito.

“Namuonea huruma sana Jacqueline (mkewe) na wanaye kama itatokea lolote litakaloweza kuwanyima haki.

JAMBO LA MSINGI

“Yaani suala la msingi ambalo linaweza kunusuru kusitokee matatizo yoyote katika hili basi ni iwe mzee ameandika wosia kabla hajafariki. Na ninavyomjua mzee kutokana na kuwa alikuwa na jopo la wanasheria, kwa vyovyote vile haiwezekani akawa amefariki dunia bila kuandika wosia,” alisema mmoja wa waombolezaji aliyeomba hifadhi ya jina.

 

MENGI ALIKUWA MAKINI?

Muombolezaji mwingine, Lucas John alisema kwa mtazamo wake, mali za mzee huyo haziwezi kuleta tatizo katika mgawanyo wake kwani Dk. Mengi alikuwa mtu makini ambaye anafanya mambo kwa kujua kuna leo na kesho.

 

“Unajua mzee Mengi alikuwa makini na ndio maana unaona hata kwa marehemu mkewe (Mercy Mengi), enzi za uhai wake walipotengana waligawana mali bila ya mzozo wowote, angalia pia kule Kilimanjaro alijenga nyumba mbili, moja yake na nyingine ya marehemu mkewe,” alisema muombolezaji huyo na kuongeza:

 

“Halafu hawa wenzetu matajiri hawakai kijingajinga, wanakaa kwa kujua nini kinapaswa kufanyika ili kujilinda kisheria. “Unajua kama hivi unavyoona mzee alimuoa Jacqueline akiwa tayari na utajiri wake hivyo anaweza kuwa alimpa masharti fulani ya kisheria.

“Nchi za wenzetu kuna kitu kinaitwa Prenup kama sijakosea, ni makubaliano ambayo wanaingia mke na mume kabla ya kuoana. Mwanaume kama ana utajiri kama hivi Dk. Mengi, anamueleza wazi mwanamke atakayemuoa kwamba likitokea la kutokea wewe utapata hiki na hiki basi akikubali anasaini ndipo wanaoana.”

 

Aliongeza kuwa mzee Mengi amemuacha mdogo wake Benjamin ambaye anaaminika kuwa ni mtu mwenye busara na ndiye amekuwa kiongozi wa familia hiyo, hivyo hakuwezi kuwa na tatizo lolote.

 

PRENUP NI NINI HASA?

Mwanasheria mmoja wa jijini Dar, Emmanuel Elias alipoulizwa kuhusu Prenup alisema ni makubaliano ya kisheria ambayo wanandoa wanaingia kabla ya kuingia kwenye ndoa ili kujilinda kisheria pale inapotokea mmoja wao amefariki dunia au wametengana.

 

“Makubaliano hayo yanatambulika katika nchi za wenzetu lakini kwa hapa nchini, sheria haizungumzi lolote,” alisema mwanasheria huyo. Haitambuliki na kinachozingatiwa zaidi ni Sheria ya Ndoa na Mirathi ya Mwaka 2002. “Sheria hii ndio inayotafsiri masuala yote yanayohusu ndoa na mambo ya wosia na mirathi. Lakini hata kama marehemu ameandika wosia, mahakama ndiyo chombo pekee cha kutafsiri sheria.

 

“Inawezekana kabisa marehemu akawa ameandika wosia lakini ukapingwa mahakamani na mahakama ikiona kuna walakini katika wosia, inaweza kutengua na kuamua inavyoona ni sahihi kulingana na malalamiko ambayo yamefikishwa mahakamani,” alisema mwanasheria Emmanuel na kuongeza:

 

“Mazingira ya kupingwa wosia mahakamani yawezekana aliyeandika alilazimishwa au ikathibitika kwamba wakati anandika alikuwa anaumwa, hakuwa sawa basi wosia unaweza kubatilishwa na mahakama ikaamua vinginevyo.”

 

WATOTO WA MENGI

Hadi umauti unamkuta, Mengi ameacha watoto wanne; Regina Mengi, Abidiel Mengi na pacha wa mkewe wa sasa, Jacqueline. Mengi alifariki ghafla Dubai, Falme za Kiarabu, Mei 2, mwaka huu na maiti yake kusafirishwa kwa ndege hadi jijini Dar ambako uliagwa Mei 6 Dar na Mei 9, Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo mazishi yalifanyika juzi kijijini kwao Nkuu, Machame wilayani Hai.

Tambwe Afunguka kurogwa na Donald Ngoma


Loading...

Toa comment