True Memories Of My Life -134

Safari yangu ya maisha mpaka hapa nilipo imekuwa ndefu, yenye milima, mabonde na miteremko mingi! Dunia imenifundisha mengi na ninaendelea kujifunza kila siku na kila ninachokutana nacho ambacho kwangu hugeuka kumbukumbu na kuwashirikisha wengine, leo hii kwenye umri wa miaka arobaini na tano nilio nao, si haba, Mungu amenilinda, ninayo kila sababu ya kumshukuru kwani nimepoteza marafiki wengi mno niliokuwa nao mpaka leo.

Ninayo bahati kubwa ya kuishi katika kipindi hiki, kushuhudia yanayoendelea katika nchi yangu ambayo watu waliokufa miaka miwili iliyopita, hawakupata nafasi ya kuyaona, si miaka miwili tu hata ndugu zetu waliopoteza uhai huko Makka walikokwenda kuhiji, hawakupata nafasi ya kumshuhudia rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mimi pia sina uhakika huo, lakini namuomba Mungu anipe uzima ili niweze kushuhudia rais huyu atakayeingia madarakani kwa mbinde akiapishwa.

Sifichi, kwa yale ambayo nchi yangu inapitia, moyo wangu umejawa hofu, sijui kitakachotokea baada ya Oktoba 25, 2015, yaani baada ya uchaguzi kufanyika.

Kwa nini nimejawa na hofu? Kauli za wanasiasa zinanitisha, inavyoonekana lolote linaweza kutokea kama hatutakataa kuchoganishwa, hatutapiga magoti chini na kumuomba Mungu atunusuru, hakika historia ya Tanzania inaweza kubadilika milele kama hatua hazitachukuliwa.

Kuna wakati naamka katikati ya usiku na kukosa usingizi kabisa nikiiwazia nchi hii na huko inakoelekea, mwisho huishia kupiga magoti na kumuomba Mungu aingilie kati. Kwa waliomshuhudia Edward Lowassa akihojiwa na televisheni ya Kenya iitwayo Citizen siku chache zilizopita, watakubaliana nami kabisa kwamba kuna hatari inakuja mbele yetu kwani tayari imekwishaanza kujengeka kichwani mwa Lowassa kwamba ataibiwa kura zake katika uchaguzi huu, jambo ambalo hayuko tayari kukubaliana nalo.

Tafsiri nyingine ya maneno haya au inavyochukuliwa na vijana wengi huko mitaani na hasa wanaposikia kauli kama hizi kutoka kwa wanasiasa wenye ushawishi kama Lowassa ni kwamba ili uchaguzi huu uonekane ni wa haki na huru na haukuwa na mizengwe wala wizi wa kura ni pale matokeo yatakaposema Edward Lowassa, mgombea wa Chadema kupitia Ukawa ameshinda, tofauti na hapo, kuna wizi!

Kauli hiyo ya Lowassa ikiunganishwa na ile ambayo Freeman Mbowe aliitoa wakati akihutubia Baraza la Idd hivi karibuni kwamba, Rais Kikwete amebadilisha makamishina wa Tume ya Uchaguzi hivi karibuni kwa lengo la kutaka kutengeneza mazingira ya kuiba kura, unachokipata ni kwamba, wanajaribu kupandikiza ndani ya akili za vijana wa Tanzania waliohemka katika uchaguzi huu, taswira ya kwamba kura zitaibiwa, kufanya hivi mapema hakika ni kuchochea chuki na machafuko kama matokeo yatakuwa tofauti na jinsi ambavyo watu wamefanywa kutarajia.

Hali hii inanikosesha usingizi, nashindwa kuelewa ni kitu gani hasa kinachojaribu kutengenezwa, je, ni kweli Lowassa na Mbowe wanajaribu kupandikiza chuki ili ikitokea wameshindwa hata kama ni kihalali, machafuko yatokee? Binafsi siko tayari kuona mtu yeyote anachezea amani ya nchi hii, kama kuna kitu niko tayari kupoteza uhai wangu kukilinda, si kwenda ikulu kama wanasiasa wanavyotaka, bali ni kutetea na kulinda amani na utulivu wa taifa ambalo Mungu amenipa la Tanzania.

Niko tayari kutofautiana na mtu yeyote bila kujali cheo chake, urafiki wetu, undugu wetu kama tu atataka kuleta chokochoko kwenye taifa langu! Ni kweli mimi ni kada wa CCM, nimekwishawahi kugombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi, sijahama chama na bado ninaamini CCM ni chama imara ingawa kina mapungufu ya kushughulikiwa, lakini pamoja na ukada wangu, sipo tayari kuona CCM inavuruga amani ya nchi yetu.

Kama kweli itatokea wakashindwa uchaguzi huu, nitakuwa mtu wa kwanza kufungua mdomo wangu na kupaza sauti kubwa na kuwaeleza “CCM chama changu kabidhi madaraka, wananchi wameamua, msituvurugie amani, Tanzania ni zaidi ya Ukawa na Chama Cha Mapinduzi.” Nitasema hivyo kwa sababu naipenda nchi hii, sitaki na sipendi siku moja nijikute mkimbizi katika nchi yoyote nikiwa nimeacha kila kitu nyuma yangu.

Lakini kama itatokea Ukawa wakashindwa au mambo yakaenda tofauti na matarajio yao, nitawataka wakubaliane na matokeo, maana kila ninapoongea nao ni kama tayari wamekwishaingia ikulu, wanachosubiri tarehe ya kuapishwa, jambo ambalo si sahihi hata kidogo! Watu wenye matarajio kiasi hiki huumia sana mambo yakienda tofauti na walivyotegemea na maumivu hayo mara nyingi huwapelekea kwenye uamuzi wa kusema “ni heri wote tukose!”

Mafuriko ya watu yanayokuja kwenye mikutano yao mijini, wanaamini wale wote ni wapiga kura wao bila kuelewa kwamba, kati ya watu wale kuna CCM, Ukawa, washangaaji na wasio na vyama, pia watoto ambao umri wao wa kupiga kura haujafika! Watu hawahawa huhudhuria kila mkutano wa mgombea unapofika, sioni kama ni kipimo sahihi cha kumpa mtu uhakika kwamba atashinda, hili ndilo limesababisha Lowassa na Ukawa kupinga matokeo ya tafiti zote zinazotolewa isipokuwa zile zinazosema wao ndiyo wanaongoza.

Sitaki kuwa mkimbizi, sitaki kuikimbia nchi hii, sitaki kushuhudia watu wakiuana kwa sababu ya siasa! Ugomvi wa watu wawili walioshindwa kuelewana sitaki mwisho wa siku uwe ugomvi wa kila Mtanzania, hili si jambo sahihi, nisingependa kabisa liwemo katika kumbukumbu zangu za siku za usoni, kwa sababu nimepata nafasi ya kuwa hai katika kipindi hiki ni bora nikatoa mchango wangu kwa kuzungumza yaliyoko moyoni mwangu kwa maslahi ya taifa langu, hata kama kuna watu nitawakwaza, maana siku hizi ukiongea kinyume na Lowassa ni lazima utukanwe matusi mazito mtandaoni, siogopi.

Ninachotamani ni kwamba baada ya tarehe 25, awe ni CCM au Ukawa aliyeshinda, nchi yetu Tanzania iendelee kuwa na amani mambo yakisonga mbele kama kawaida na yeyote atakayeshinda aungwe mkono na Watanzania wote, wa dini zote, rangi zote, kabila zote, itikadi zote katika kujenga taifa letu kwa maslahi ya vizazi vilivyopo na vitakavyofuata baada ya sisi, wakati wa kutofautiana ni sasa, Tume ya Uchaguzi ikishatangaza matokeo, muda wa kutofautiana tena haupo bali ni kuungana na kujenga taifa.

Maneno haya ni yangu, si ya wanasiasa ambao wao huwa hawajali kabisa vifo vya watu ilimradi malengo yao yatimie, yatupasa sisi tunaolipenda taifa hili, wamiliki wa taifa hili ambao huwaweka wanasiasa na kuwaondoa, tuwe makini! Na kauli zote zitakazotolewa baada ya Oktoba 25, zote zenye kuchochea vurugu tuzikatae na kuzikemea kwa faida yetu sisi wenyewe.

Wazungu wana msemo wao usemao “It is good to learn from other people’s mistakes” ambao kwa Kiswahili unamaanisha ni vizuri kujifunza kutokana na makosa ya watu wengine, hauhitaji kujimwagia tindikali ili uweze kuona ina uwezo gani wa kuunguza, bali unatakiwa kumuangalia mtu aliyeungua kwa tindikali na hapohapo ufahamu kwamba tindikali si kitu cha kujimwagia.

Mimi huwa naitazama Libya na hali iliyo nayo kwa sasa, watu wake wakikimbia kwenda kutafuta hifadhi katika nchi za Ulaya, wengi wakifia majini baada ya mitumbwi midogo waliyopanda kuzama! Watu hawa waliishi vizuri wakati wa utawala wa Muammar Gaddafi, lakini Nchi za Magharibi zikawapandikiza chuki dhidi ya kiongozi wao huyo aliyewapa maisha ambayo leo wote wanayakumbuka, wakainuka na kumwondoa madarakani, leo hii ni majuto wanatamani kurejea walikoanzia lakini imekuwa ngumu.

Mfano wa Libya peke yake unatosha kabisa kunifundisha mimi kwamba, sihitaji kuchonganishwa na wanasiasa, eti nimchukie Mtanzania mwenzangu kwa sababu tu yeye ni Chadema na mimi ni CCM, haiwezekani! Nakubali kwamba wanadamu hatuwezi kuwa na mtazamo wa aina moja katika jambo, lazima tutofautiane, lakini juu ya tofauti hizi lazima tubaki kuwa kitu kimoja, Watanzania wenye wajibu wa kulinda amani na ustawi wa taifa letu, tusijaribu kabisa kukubali baada ya matokeo kutangazwa kuingizwa katika machafuko na wanasiasa wachache wenye tamaa ya madaraka, sisi tuwe watu wa kwanza kuwanyooshea vidole na kuwaambia tuachieni Tanzania yetu.

Katika hili naongea sana na vijana wa nchi yangu, ambao wamehemka kwelikweli wanataka mabadiliko, kwao mabadiliko ni kuiondoa CCM madarakani hata kama CCM hiyohiyo ina uwezo wa kuleta mabadiliko chini ya uongozi wa mtu mwingine, tofauti na hapo wameambiwa watakuwa wameibiwa.

awaomba watumie vizuri akili zao ambazo Mungu amempa kila mmoja wetu, tufikiri vizuri, tusipelekwe tu kama farasi ambao mwisho wa siku hatujui tunachokitaka bali tunawasaidia waliotupanda kutimiza ndoto zao.

Asubuhi ya Ijumaa iliyopita nilikuwa nikiangalia mbio za farasi kwenye runinga, nikamuona farasi mmoja mweupe akikimbia kwa kasi kuliko farasi wengine, juu yake akiwa amekaa kijana mmoja wa Kizungu, mbio hizo ziliitwa London Horse Race, yaani mashindano ya mbio za farasi ya London, mbio za nini? Za farasi, si za binadamu aliyempanda farasi.

Mwisho wa mashindano farasi huyo mweupe alishinda, kilichotokea ni mwendesha farasi kuruka kutoka mgongoni mwake na kukimbia kwenda kupokea kikombe pamoja na hundi ya fedha nyingi, akatangazwa bingwa wa mbio za farasi! Hakutangazwa farasi, bali alitangazwa mwendesha farasi na ndiye aliyepokea kikombe na hundi wakati farasi aliyeshinda akiwa kando akiendelea kula nyasi.

Mfano huu unanihusu mimi na wewe msomaji, kamwe tusikubali kufanywa farasi na wanasiasa ambao watatutumia kuwafikisha kwenye utukufu, baada ya hapo watatuacha tukila nyasi wakati wao wakienda kupokea kikombe! No way, haiwezekani, ni lazima tuhakikishe tunafanya maamuzi sahihi siku ya Oktoba 25, kuchagua mtu ambaye baada ya kupokea kikombe na hundi, hatamwacha farasi akila nyasi bali ataitumia hundi hiyo ya fedha nyingi kumjengea banda zuri na hata kumtafutia daktari wa kumtibu ili mashindano mengine yakija awe na afya njema.

Na farasi wengine walioshindwa katika mbio hizo wasitumiwe na waendesha farasi kupigana na farasi mweupe na mwisho wa siku kuuana wao kwa wao, ndugu zangu Watanzania ni wakati wa sisi wenye nchi kujitambua na kufanya maamuzi yenye maslahi kwetu sisi si waendesha farasi, Mungu ametupa hekima na busara ya kufanya maamuzi sahihi, basi tuzitumieni akili hizo na tufanye kila kinachowezekana kuhakikisha amani na utulivu kwa taifa letu unaendelea hata baada ya Oktoba 25.
Mungu ibariki Tanzania,
Mungu wabariki Watanzania wote.


Loading...

Toa comment