True Memories Of My life 138
Wiki iliyopita niliishia pale nilipokuwa nasema sijawahi kusikia furaha kiasi hicho, hakika alichokifanya Padri Ngassa ni kitu cha kuungwa mkono na kila mmoja wetu na ninakusihi wewe unayesoma hapa, kama mtu una wazo la biashara songa mbele ulifanye, Mungu atakupa watu wa kukusaidia kulifanikisha
SASA ENDELEA…
Kwa neema ya Mungu nimefika hapa nilipo maishani mwangu, ndicho ninachoweza kusema lakini pamoja na neema hiyo, sheria ilikuwa NEEMA + KANUNI = MAFANIKIO.
Nimefundisha mara nyingi kwenye mikutano yangu ya kwamba mambo haya mawili ni lazima yaende pamoja, KANUNI peke yake zikitumika bila NEEMA YA MUNGU hakuna kinachoweza kutokea maishani mwako, huu ni ukweli.
Ni kweli kwa NEEMA tunabarikiwa, lakini bila kutumia KANUNI fulani udhihirisho wa Baraka za Mungu maishani mwetu hauwezi kuonekana. Hapa nina maana kwamba ni lazima mambo fulani yafanyike pamoja na hiyo NEEMA ndipo upate kubarikiwa.
Mfano mzuri wa kudhihirisha sheria hii ni kama baba yako alifariki dunia ukiwa mtoto mdogo na kukuachia utajiri wa bilioni mia mbili kwenye akaunti, fedha hizo ingawa ni zako bado ni lazima upitie mchakato fulani ndiyo uzipate, mfano, lazima uende benki kufuata taratibu za kisheria ili uweze kumilikishwa kisheria ingawa kweli ni zako, usipofanya hivyo, fedha hizi zitabaki kwenye akaunti bila wewe kufaidika nazo.
Hivyo ndivyo ilivyo katika ulimwengu wa mafanikio, lazima pamoja na NEEMA ya Mungu, KANUNI kadha wa kadha ni lazima zitumike ili uweze kuzipata BARAKA za Mungu, Wakristo wengi sana wameishi maisha duni ingawa walitakiwa kuishi maisha ya kitajiri kwa sababu tu hawaelewi jinsi ya kutumia sheria hii ya NEEMA + KANUNI = MAFANIKIO.
Ukisoma katika Biblia kwenye Kitabu cha Muhubiri 10:7 neno la Mungu linasema wazi kuwa “Nimeona watumwa wamepanda farasi, na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama watumwa.” Watu waliotakiwa kuishi kama wafalme, wanaishi kama watumwa na waliotakiwa kuishi kama watumwa wanaishi kama wafalme, kwa nini? Hapa hakuna jibu lingine zaidi ya kwamba waliotakiwa kuishi kama watumwa wanaishi kama wafalme kwa sababu wanazijua kanuni na wanazitumia maishani mwao.
Huu ni ukweli, yeyote anayeijua kanuni na anaitumia, bila kujali ameokoka au hajaokoka, lazima aishi kama mfalme! Na asiyeijua kanuni au anaijua lakini haitumii ingawa alitakiwa kuishi kama mfalme ataishi maisha yake kama mtumwa, hivyo basi ndugu zangu, ni lazima tujifunze kanuni za mafanikio, nilipoamua kutafuta mafanikio nililazimika kuzifahamu kanuni hizi na kuzitumia maishani mwangu, ukizifahamu na ukazitumia, bila kujali umeokoka au hujaokoka, una digrii au huna digrii; utaishi kama mfalme!
Ndiyo maana maishani unawashuhudia watu wenye elimu kubwa kabisa, wengine wana digrii au PHD za uchumi, lakini bado wanaishi maisha kama watumwa, huku watu ambao pengine hawakuingia hata darasani lakini walizifahamu tu kanuni barabarani, wakazitumia, ndiyo wanawaajiri wenye PHD.
Moja ya kanuni ambayo mimi ndugu yenu naifahamu na nimeitumia sana maishani mwangu ni KANUNI ya kusaidia maisha ya watu wengine kubadilika, yaani kila siku kujiuliza “Hivi nawezaje kutumiwa na jamii yangu?” Au “Nawezaje kuleta tofauti katika maisha ya watu wengine?” mtu ambaye hujiuliza maswali haya na kupata namna ya kusaidia wengine, hakika hawezi kukwama maishani mwake maana kama vile ambavyo yeye huwasaidia wengine, Mungu atamwamini na vitu ili aweze kumwakilisha vizuri hapa duniani.
Hivi huwa hushangai kwamba watu bahili na wachoyo sana huwa hawasongi mbele kifedha!? Wapo watu hapa duniani hawatumii vitu vyao kabisa na watu wengine lakini hawapigi hatua maishani, tofauti na watu ambao kila siku wanawaza jinsi ya kusaidia watu wengine kunyanyuka, ambao kila siku utawasikia wanazidi kusonga mbele, hii ni siri kubwa sana ya mafanikio ilimradi tu uwe unamfanyia Mungu siyo kufanya ili wanadamu waone.
Nawaelezeni yote haya kwa lengo moja la kuwafanya mzijue siri za mafanikio, ziko kama kumi hivi, ukitafuta kitabu changu cha Sheria Kumi Zilizothibitishwa za Kutoka Kwenye Umasikini Kwenda Kwenye Utajiri, utazisoma zote na kuzielewa na kama utazitumia, nakuhakikishia kwamba haijalishi hapo ulipo leo, haijalishi kiwango chako cha elimu, haijalishi kabila wala rangi yako ya ngozi; UTAFANIKIWA UTAKE USITAKE.
Hapa siwezi kuacha kuwaeleza historia ya msichana aitwaye Sikujua Mjalifu ambaye siku moja baada ya ibada ya kumshukuru Mungu kwa maisha ya baba yangu iliyofanyika kijijini kwetu Bupandwamhela, alifika nyumbani asubuhi sana, nilipotoka tu nje nilimkuta ameketi kwenye kiti akinisubiri, kama nakumbuka vizuri alikuwa ameongozana na kaka yake. Kwa kumwangalia tu mara moja niligundua kuwa msichana yule alikuwa mgonjwa, kidevu chake kilikuwa kimekuwa kikubwa kikikaribia nusu ya kichwa chake, meno yalikuwa nje na alionekana kuwa kwenye maumivu makali.
Kwa umri anaweza kuwa na miaka kama kumi na tano au na sita hivi, sawasawa kabisa na mwanangu Butogwa, nikamsogelea karibu na kumsalimia, akiniamkia kwa sauti iliyotoka kwa tabu kubwa kwa sababu ya maumivu. Nikaketi kwenye kiti kando yake nikitaka kufahamu nini hasa lilikuwa tatizo lake.
“Naumwa!”
“Nini?”
“Nimevimba hivi, sina fedha ya kwenda hospitali, familia yangu ni masikini!”
Moyoni mwangu nilisikia maumivu makali mno, nikakumbuka nilipotokea mpaka nilipokuwa, sauti ikaniambia kutoka ndani “Eric nimekuletea huyu mtoto umsaidie” ndivyo nilivyojisikia kutoka ndani, ni kweli ninazo shida nyingi na kwa hakika ninahitaji fedha ili nizitumie kutatua matatizo yangu, lakini mara ninapokutana na hali kama niliyokuwa nayo baada ya kumsikiliza binti huyo, husahau matatizo yangu yote.
“Usijali binti, Mungu atakuponya!”
“Nisaidie, bila wewe nitakufa.”
“Mungu atatuelekeza tufanye nini!”
Sikuwa na jibu kwa wakati huo, lakini ndani yangu nilisikia kabisa sauti inayoniambia kwamba binti huyo angepona, kama ambavyo binti aitwaye Ng’endelaki ambaye miaka mingi nilikutana naye Kigogo, Dar es Salaam akiwa katika hali ya kufa, Mungu akatuwezesha kuchangisha fedha nyingi kutoka kwa wasamaria wema akasafirishwa kwenda India kwa matibabu ya moyo, akarejea akiwa mzima na leo hii ninavyoandika alishafunga ndoa na ni mama wa watoto wawili.
Baada ya kuongea na binti huyo nilimwambia siku iliyofuata nilikuwa naondoka kurejea Dar es Salaam, nikiwa huko ningefanya mipango yote ili yeye asafirishwe kuletwa aidha Dar es Salaam au Mwanza kwa matibabu! Nilitamka maneno hayo nikiamini Mungu angesaidia, nilikuwa nimejawa na huruma mno, nikifikiria ni kiasi gani mimi na familia yangu Mungu alitupendelea maana binti huyo aliyelazimika kuacha shule kwa sababu ya ugonjwa hakutaka kuwa mgonjwa, bali aliamka tu siku moja akajisikia hayuko sawa na baadaye akaanza kuvimba.
Nilimpa msaada kidogo ambao Mungu alinielekeza umsaidie nikiwa sipo, kweli siku iliyofuata nikasafiri kurejea Dar es Salaam ambako kitu cha kwanza nilichokifanya pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kuanza kumtafutia binti huyo daktari wa kumtibu, kichwani mwangu likaja jina la rafiki yangu mmoja daktari wa Hospitali ya Bugando aitwaye Dk. Gitti, kijana mdogo tu lakini Mungu ameibariki mikono yake na kuwa daktari bingwa wa upasuaji.
“Daktari nina shida sana, naomba unisaidie.” Nilimwambia katika mazungumzo yetu na baadaye akanitaka nimtumie picha ya binti huyo kwa njia ya simu kwenye Mtandao wa WhatsApp, sikuwa nayo picha, hivyo niliwasiliana na mdogo wangu aitwaye Tony huko kijijini nikimtaka apige hiyo picha haraka na kunitumia, ndani ya saa mbili jambo hilo lilishafanyika, picha ikawa kwenye simu yangu nami nikamtumia daktari.
“Eric huu ni ugonjwa uitwao Ameloblastoma, unahitaji umlete haraka sana Mwanza aonane na daktari bingwa wa sikio, pua na koo, anaitwa Dk. Gustave Bunane, ni kijana pia, mtu safi atakuwa tayari kukusaidia!”
“Naomba unipe namba yake ili niwasiliane naye!”
Dk. Gitti ambaye wakati huo alikuwa Itigi mkoani Singida akifanya upasuaji kwenye moja ya kambi za upasuaji alinitumia namba hiyo nami nikawasiliana na Dk. Gustave ambaye alinipokea vizuri na kusema binti huyo aletwe haraka iwezekanavyo.
Kama wiki tatu hivi zilipita ndipo tukafanikiwa kumpeleka Mwanza ambako alipokelewa na kufanyiwa vipimo vyote, madaktari wakathibitisha kwamba alikuwa na tatizo ambalo Dk. Gitti aliniambia, njia pekee ya kumsaidia ilikuwa ni kuiondoa taya yote kwa upasuaji kwani lilikuwa limeoza na baadaye kumwekea vyuma ili kumwacha na shepu yake ya zamani, vidonda vikipoma angewekewa mfupa wa taya wa bandia na kutengenezewa meno ya bandia ambayo yangemwezesha kuishi kama kawaida.
Huwezi kuamini ndugu msomaji kwamba upasuaji kama huu umefanywa na vijana wa Kitanzania kwenye Hospitali ya Bugando jijini Mwanza wakimsaidia Sikujua Mjalifu mpaka ninavyoandika kumbukumbu yangu hii bado yuko hospitali, anaendelea vizuri, akicheka na kutabasamu tena! Moyo wangu una furaha kwa sababu kwa mara nyingine tena nimemfanya mwanadamu mwenzangu aliyekuwa akiteseka acheke.