The House of Favourite Newspapers

True Memories Of My life-144

wiki iliyopita niliishia kwamba kauli za Edward Lowassa kwenye runinga zilinifanya nianze kuwa na wasiwasi kwamba vurugu zingeweza kuibuka nchini, maana kauli yake moja tu kwa vijana wa taifa letu ingeweza kusababisha maafa makubwa! SASA ENDELEA…

Hofu ya vurugu ilikuwa imetanda, vijana wa Bajaj na bodaboda jijini Dar es Salaam ni kama walikuwa wakisubiri kauli ya Edward Lowassa ili waingie mitaani na kufanya vurugu, jeshi la polisi nalo lilikuwa limejipanga, ilishatangazwa awali kwamba watu hawakutakiwa kukaa kwenye vikundi.

Askari walikuwa wengi mno mtaani, magari ya doria yalikuwa yakizunguka kila kona, hali hiyo ndiyo ilizidisha hofu zaidi, kulikuwa na askari waliovalia kiraia kila mahali, naweza kusema karibu kila mtaa jijini Dar es Salaam kulikuwa na askari akiangalia usalama na wananchi, walishataarifiwa mara tu wakiona dalili ya vurugu popote wapige simu polisi.

Hayo yakiendelea, matokeo yaliendelea kusomwa kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere na Jaji Damian Lubuva, kura za Dk. John Pombe Magufuli zilikuwa zikiongoza kwa karibu kura milioni mbili hivi na bado Kanda ya Ziwa ambayo ndiyo ngome yake ilikuwa bado haijamalizika, usomaji wa matokeo hayo uliashiria kila dalili kwamba Edward Lowassa angeshindwa na watu walisharidhishwa kabisa na jinsi matokeo yalivyokuwa yakisomwa laivu baada ya kupokelewa kutoka kwenye vituo.

Kazi ya kusoma matokeo iliendelea, huku hofu yangu ya vurugu ikizidi kupungua, watu walikuwa wakiomba sana kwenye makanisa na misikiti ili vurugu zisitokee, tarehe 29 ndipo matokeo ya Rais yalitangazwa kwenye ukumbi huohuo, sikuwaona viongozi wa Ukawa ukumbini hapo wakati matokeo ya Urais yakisomwa, sikushangaa sana kwani walishagoma kuyatambua.

Nikiwa nimesimama mbele ya runinga ofisini na wafanyakazi wenzangu, Dk. John Pombe Magufuli alitangazwa ushindi wa nafasi ya Urais wa mwaka 2015, hiyo ilimaanisha ndiye angekuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania! Ilikuwa ni kama naota ndoto ingawa jambo hilo nililitegemea, Magufuli amekuwa rais? Nilijiuliza moyoni mwangu na kumshukuru Mungu.

Katika watu wenye siri duniani ni Dk. John Pombe Magufuli, mara kadhaa nilishamuuliza kama alikuwa na mpango wa kugombea urais lakini alinikatalia kabisa, akidai kazi ya Urais ilikuwa ni ngumu kwake, kumbe alikuwa na siri moyoni ambayo hatimaye ilikuwa imetimia siku hiyo, moyoni nikajisemea “Lazima alishasoma Kitabu cha 48 Laws of Power” ambacho moja ya sheria za kupata nguvu katika jamii ni ile isemayo “Conceal Your Intention” yaani ufiche kabisa nia yako maana ikijulikana mapema adui au wapinzani wako watahakikisha unakwama kuitimiza, sheria hiyo ndiyo Dk. John Pombe Magufuli aliitumia mpaka kufika kileleni, alitangaza nia kugombea bila mbwembwe, akachukua fomu bila kelele na kuzunguka nchi nzima kimyakimya, hakika nilikuwa nimejifunza jambo kubwa kwa ushindi wake.

Jambo lingine nililojifunza ni lile ambalo wazungu huliita kwa lugha yao ya Kiingereza “hard work pays” yaani kufanya kazi wa juhudi kunalipa, kilichomfikisha kwenye ushindi huo Dk. John Pombe Magufuli pamoja na kuwa mtu mwenye bahati, ilikuwa ni tabia yake ya uchapakazi, ni vyema kuwa mchapakazi hata kama watu hawaoni au wanakuzibia, ipo siku uchapakazi wako utakupeleka juu, kwani mafuta ya taa hayawezi kukaa chini ya maji na wema hauwezi kufichwa kwa ubaya, ipo siku utachomoza.

Tarehe 30 alikabidhiwa cheti chake cha urais kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, yote hayo niliyashuhudia kwenye runinga nikiwa bado siamini kama kweli Dk. John Pombe Magufuli ameshinda urais. Kitu kimoja nilichokifahamu ni kwamba nchi yangu Tanzania ilikuwa imepata kiongozi bora ambaye angeweza kuitoa mahali ilipo kwenda hatua nyingine, niliamini hivyo kwa jinsi nilivyomfahamu Dk. Magufuli.

Siku zote niliamini nchi yangu ilihitaji rais mchapakazi, mkali na mfuatiliaji wa mambo asiyetokana na mtandao au matajiri, hivyo ndivyo nilivyowahi kusema huko nyuma kwenye maandishi katika ukurasa huu, nilipotoa sababu zangu za kumpinga Edward Lowassa. Mtu huyo katika watu wote waliogombea alikuwa ni Dk. John Pombe Magufuli.

Nilijua angetubana, utaratibu wa maisha ungebadilika, ujanjaujanja ungeondoka lakini mwisho wa siku maisha ya watu yalikuwa ni lazima yabadilike, kama ningebanwa mimi lakini shangazi yangu kijijini akapata matibabu asife kwa sababu ya kukosa dawa, lilikuwa ni jambo jema! Nilimpigia kura nikijua angenibana lakini nilikuwa tayari.

Baadaye nikasikia mhubiri mashuhuri kutoka Nigeria, Nabii TB Joshua ameingia nchini kwa ndege yake binafsi na kupokelewa na Dk. Magufuli pamoja na mkewe uwanja wa ndege, nilikuwa na taarifa juu ya urafiki wa watu hao uliotokana na Dk. Magufuli kukutana na nabii huyo nchini Nigeria, hivyo sikushangaa, akakaribishwa ikulu na kukutana na Rais Kikwete na baadaye Edward Lowassa nyumbani kwake Masaki, huyu pia walikuwa na uhusiano wa karibu.

Ujio wa mtu huyu ulinifanya niamini ulilenga kuepusha machafuko, lazima angetumika kutuliza hali ya hewa na pia kwa uwezo wake wa kuwasiliana na Mungu lazima angefanya maombi maalum na amani ingedumu kama ambavyo Watanzania walikuwa wamekwishaomba, sikumwona tena baada ya hapo nikitarajia pengine angekuwepo uwanjani siku ya kuapishwa kwa rais.

Haikuwa hivyo, uwanjani hakuonekana, nilikuwa miongoni mwa watu waliohudhuria, nikanyeshewa na mvua kiasi cha kutosha na suti yangu nyeusi lakini sikujali nikisubiri kwa hamu kumwona Dk. John Pombe Magufuli akiapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo hilo lilipotokea, mizinga ikapigwa, akakagua gwaride ndipo nilinyanyua uso wangu juu kuangalia mbinguni nikisema “Ahsante Mungu”.

Nilianzisha mazungumzo na mtu aliyekuwa ameketi kando yangu, nikamhakikishia kwamba kwa kuapishwa kwa Dk. Magufuli, Tanzania ilikuwa imebadilika, isingekuwa ile tena tuliyoizoea, yeye pia aliniunga mkono! Nyuma yangu alikuwa ameketi Daudi Machumu, mkurugenzi wa baa mashuhuri nchini Tanzania iitwayo Break Point, tuligonganisha mikono kwa furaha, kila mmoja wetu alionekana kufurahia Rais Magufuli kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Suala gumu likabaki visiwani Zanzibar ambako uchaguzi ulikuwa umetangazwa kufutwa kwa sababu ya udanganyifu uliofanyika na Chama cha Wananchi CUF, kilikuwa kimegomea uamuzi huo wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kikidai hakikuwa tayari kuona uchaguzi unarudiwa, huku ndiko kulikuwa na mtihani, hakuna aliyejua nini kingetokea ingawa jitihada za chinichini zilikuwa zikifanyika kuona kama mgogoro huo ungemalizika kwa amani bila damu kumwagika maana historia ya Zanzibar ni ya machafuko.

Sikukaa mpaka mwisho uwanjani, nikarejea ofisini ambako niliendelea kufanya kazi huku nikiendelea kufuatilia kupitia kwenye runinga, nikashuhudia Rais John Pombe Magufuli na familia yake wakiwasili Ikulu ya Magogoni na kupokelewa na wafanyakazi wa ikulu, pia nikamshuhudia mama yake mzazi akiwa amezungukwa na walinzi, nikaipima furaha ambayo mama huyo alikuwa nayo kushuhudia jambo kubwa kama hilo maishani mwake.

Siku hiyohiyo alimuapisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali bila kupoteza wakati, nikajua kweli mzee wa HAPA KAZI TU alikuwa ameanza utekelezaji, uvivu miongoni mwa Watanzania sasa ulikuwa unachimbiwa kaburi ili uzikwe, moyoni mwangu nilikuwa na matumaini makubwa mno.

Siku moja baadaye, wakati akitembezwa na wafanyakazi wa ikulu kuoneshwa mazingira ya ikulu, walifika getini, akaona jengo limeandikwa Wizara ya Fedha, wafanyakazi wa ikulu wakashangaa kumwona anazidi kuendelea na safari nje kabisa ya ratiba, kwa sababu si rahisi kumzuia rais au kumuuliza “Mzee unakwenda wapi?” wakalazimika kumfuata nyuma taratibu mpaka wakaingia ndani ya Jengo la Wizara ya Fedha na kukutana wafanyakazi wengi hawapo kwenye meza zao za kazi.

“Wa hapa? Na wa hapa? Na wa hapa?” aliendelea kuuliza aliowakuta kila alipogusa meza ambayo haikuwa na mtu.

Nina uhakika presha za waliokutwa ofisini siku hiyo zilipanda nusura zipasue mishipa, jasho jembamba lilikuwa likiwatoka, sawasawa na mtu aliyekuwa akiangalia sinema ya kutisha! Hali hiyo ikikutokea ni rahisi sana kulowanisha nguo ya ndani kama ulikuwa hujaenda msalani nusu saa kabla.

Utekelezaji wa HAPA KAZI TU ulikuwa umeanza, baadaye rais alifanya kikao na uongozi wa wizara na kutoa maelekezo ya kubana matumizi ikiwemo kufuta kabisa safari za nje zilizokuwa zikitafuna mabilioni ya fedha za wavuja jasho, haikuwa habari nzuri sana kwa wafanyakazi wengi wa serikali.

Comments are closed.