The House of Favourite Newspapers

Trump Asitisha Misaada Ya Kijeshi Ukraine

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesitisha misaada yote ya kijeshi kwa Ukraine kufuatia kuvunjika kwa mkutano kati yake na Rais Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House, jijini Washington.

Hatua hiyo inakuja kufuatia msimamo wa Trump tangu alipoingia madarakani wa kutaka kumalizika kwa vita kati ya Urusi na Ukraine kwa njia ya usuluhishi.

Ijumaa iliyopita, Trump alimtuhumu Zelensky kwa kile alichodai ni ukosefu wa shukrani kutokana na msaada uliotolewa na Marekani tangu kuanza kwa vita hivyo.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Ikulu ya White House kililiambia Shirika la Habari la Reuters kuwa msimamo wa Trump upo wazi — kwamba anataka amani kati ya Ukraine na Urusi.

“Rais anataka washirika wake wote wajue hilo. Ameamua kusitisha msaada huo ili kufanya tathmini kama unasaidia kuelekea kwenye njia anayoitaka.”

Hata hivyo, chanzo hicho kimeeleza kwamba bado suala la mkataba wa madini kati ya Marekani na Urusi lipo palepale.