Trump: Sudan Iwalipe Fidia Wahanga Shambulio Dar, Nairobi
RAIS wa Marekani, Donald Trump, amesema serikali anayoongoza itaiondoa Sudan katika orodha ya wafadhili wa ugaidi iwapo italipa fidia ya dola milioni 335 sawa na Sh. Bilioni 737 za Tanzania, kwa wahanga wa mashambulio ya Dar es Salaam na Nairobi.
Waziri Mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok, amejibu kuwa fedha hizo zimeshatolewa tayari lakini hakukuwa na majibu ya haraka kutoka Marekani.
Sudan ilikuwa imewekwa na taifa la Marekani katika orodha ya wafadhili wa ugaidi tangu mwaka 1993 wakati kiongozi wa al-Qaeda, Osama Bin Laden, alipopewa mwaliko na serikali kwenda kuishi kwenye taifa hilo. Marekani inaamini kuwa mpango wa mashambulio yaliyofanyika kwenye balozi zake mbili, Tanzania na Kenya, nchi hiyo ilishiriki.
Fidia hiyo inahusisha mabomu yaliyolipuliwa na al-Qaeda mwaka 1998 katika balozi za Marekani barani Afrika.
Shambulio hilo lililotokea karibu kwa wakati mmoja, Dar es Salaam, Tanzania, na Nairobi, Kenya, lililoua watu zaidi ya 220, linatakiwa kulipwaa fidia hiyo kwa wahanga na familia za waliopoteza ndugu zao,” Rais Trump alisema.
Uhusiano wa Marekani na Sudan umeimarika tangu Rais Omar al-Bashir alipoondolewa madarakani kwa maandamo na baadaye jeshi la nchi hiyo kuchukua hatamu.