Tshabalala: Al Ahly Tutawafunga Nje Ndani
IKIWA kesho Jumanne Simba wanakwenda kucheza mchezo wao wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya National Al Ahly, nahodha msaidizi wa timu hiyo, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, amefunguka na kudai kuwa uwezo wa kuwafunga Waarabu hao nyumbani na ugenini ni mkubwa.
Tshabalala alisema soka limebadilika na sasa Simba ni kati ya timu kubwa na bora Afrika ambayo inaweza ikashinda kwenye uwanja wowote, hivyo suala la kupata alama sita mbele ya Al Ahly linawezekana kwa asilimia kubwa.
Akizungunza na Championi Jumatatu, Tshabalala alisema kwa namna ambavyo wachezaji wapo na morali ya hali ya juu wana ana kila sababu ya kuamini kuwa wanaweza kushinda kwenye mchezo wowote na hatua yoyote kwenye uwanja wowote, hivyo hata Al Ahly wanaweza wakawafunga kesho na kwenye mchezo wa marudiano kule Cairo wanaweza kushinda tena.
“Unajua sisi tumejiandaa vizuri sana msimu huu, tunataka kufikia malengo kwa asilimia kubwa sana, timu yetu imeshakuwa kubwa na bora Afrika, hivyo inaweza kushinda mbele ya timu yoyote na kwenye uwanja wowote, kwa hiyo hata Al Ahly tunaweza kuwafunga hapa kwetu na kwao, yote yanawezekana,” alisema Tshabalala.
Simba wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kupata alama tatu ugenini dhidi ya As Vita wakishinda 1-0. Lakini pia wanaingia wakiwa na kumbukumbu ya kuwafunga Al Ahly kwa bao 1-0 la Meddie Kagere kwenye mchezo wao wa mwisho kukutana jijini Dar, 2019.
ISSA LIPONDA, Dar es Salaam