The House of Favourite Newspapers

TTCL KUITIKISHA DAR NA TAMASHA LA ‘RUDI NYUMBANI KUMENOGA’

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Corporation linatarajia kufanya matamasha makubwa matatu jijini Dar es Salaam katikaa wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni ikiwa ni mwendelezo wa kampeni ya Rudi Nyumbani Kumenoga, inayofanyika sambamba na kutoa burudani.

 

Hii ni kuunga mkono hamasa iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli siku ya tar 21 Juni 2018 alipokuwa akipokea gawio la Tsh Bilioni moja na nusu kutoka TTCL Corporation.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo wa Shirika la Mawasiliano Tanzania-TTCL Corporation, Bw. Ally Mbega alisema tamasha hilo litapambwa na wasanii Shilole, Man Fongo, Belle 9, Dully Skykes pamoja na Chege Chigunda.

 

Alisema burudani hiyo itaanza siku ya Ijumaa Desemba 21, katika Uwanja wa CCM Mwinjuma, Mwananyamala, na siku ya Jumamosi Desemba 22, Kampeni hizo zitafanyika Wilaya ya Ilala katika Uwanja wa Karume huku fainali za burudani hizo kumalizikia Jumapili Desemba 23, Wilayani Temeke katika Viwanja vya Mbagala Zakhem.

 

“Hadi tunavyozungumza leo, Kampeni hii imetembelea Mikoa yote ya Tanzania Bara na Miji mashuhuri na Wikiendi hii ni zamu ya Jiji la Dar Es Salaam. Katika Kampeni za mikoani, tumefanya kazi na Wasanii wawili maarufu, Shilole na Man Fongo.

“Katika kila Mkoa tumekuwa na utaratibu wa kuwapa fursa Wasanii Chipukizi wa Mikoa hiyo na Wasanii Wenyeji kushirikiana na sisi katika Matamasha yetu yanayofanyika kukamilisha Wiki nzima ya Kampeni ya kutoa Elimu kwa Umma, kutangaza fursa zilizopo TTCL pamoja na kusajili Wateja Wapya na Mawakala wa Huduma zetu za Simu za Mezani, Simu za Mkononi, Data na Fedha Mtandao-(T PESA) ambazo ni bora, nafuu na salama,” alisema Mbega.

 

Akifafanua zaidi alisema kwa Jiji la Dar Es Salaam, TTCL imewaongeza wasanii wakubwa watatu ili Washirikiane na Shilole na Man Fongo katika kutoa burudani hivyo Belle 9, atakuwepo katika Kampeni za Wilaya ya Kinondoni, Dully Skykes katika Kampeni Wilaya ya Ilala huku Chege Chigunda akifunga kazi katika fainali za burudani na kampeni Wilaya ya Temeke.

 

“Natumia fursa hii kuwakaribisha Wananchi wote kuhudhuria kwa wingi katika maeneo yaliyotajwa. Wasanii chipukizi  katika fani mbalimbali nao kutumia fursa hii kuonesha uwezo wao juu ya Jukwaa la kisasa na Vifaa vya kisasa vya muziki vitakavyowawezesha kujinadi.”

 

“Matamasha haya hayana kiingilio, ni bure na wazi kwa Wananchi wote. Kigezo muhimu kwako ni kuwa na laini ya TTCL au kuja na Kitambulisho chako ili usajiliwe kuwa Mteja wetu. Laini zetu zitatolewa bure kwa wote watakaojiunga nasi. Muda ni kuanzia saa 8 kamili Mchana.”

Comments are closed.