WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL Corporation) kwa kufanikiwa kufikisha huduma za mawasiliano ya Intaneti kwenye Kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Waziri, Mhe. Nnauye ametoa pongezi hizo alipokuwa katika hafla ya awali kuelekea uzinduzi wa huduma za mawasiliano katika Mlima Kilimanjaro, uliofanyika Makao Makuu ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kusimika huduma za mawasiliano katika kilele cha Mlima kilimanjaro, jambo ambalo litaongeza kasi ya kuutangaza mlima huo duniani na kuvutia idadi kubwa ya watalii kuutembelea.
“Leo ni siku muhimu kwa Shirika letu la TTCL na Tanzania tunapokwenda kushuhudia tukio la kihistoria la uzinduzi wa intaneti katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, utakaofanyika pia rasmi kwenye kileleni cha mlima Desemba 13, 2022 tukiwa huko kileleni,” alisema Mhe. Nnauye.
“Tangu kuzinduliwa kwa huduma za mawasiliano katika vituo vya awali, watalii wanaopanda mlimani wameanza kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki wakiwa mlimani na kuelezea uzuri wa vivutio vyetu jambo ambalo linaendelea kuutangaza utalii nchini, licha ya kurahisisha shughuli za huduma kwa watalii zinazofanywa na taasisi mbalimbali katika Mlima Kilimanjaro,” alisisitiza Waziri Nnauye.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Eng. Peter Ulanga akizungumza alisema uwepo wa huduma ya mawasiliano katika Mlima Kilimanjaro utaboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa watalii mlimani, na pia wanapopata dharura.
Alibainisha kuwa huduma za mawasiliano zitaimarisha shughuli za ulinzi na usalama kwa watalii wakiwa mlimani kupitia mamlaka husika jambo ambalo ni kivutio cha kuchocheza na kuvutia watalii wengi kuutembelea Mlima Kilimanjaro.
“Mkakati wa Shirika wa miaka mitano ni kuhakikisha huduma za mkongo zinawafikia wananchi katika makazi yao, maeneo ya biashara, maofisini na sehemu za vivutio vya utalii wetu, TTCL inatambua umuhimu wa utalii nchini hivyo tutaongeza nguvu kutoa huduma za mawasiliano kupitia mkongo katika maeneo mengine ya utalii ili kuchochea shughuli za utalii nchini,” alibainisha Eng. Ulanga.
|