The House of Favourite Newspapers

Tujikumbushe: Safari Ya Kifo Ya Mwalimu Nyerere!

MIAKA 20 iliyopita Taifa la Tanzania liligubikwa na majonzi mazito kutokana na kifo cha mwasisi wake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

 

Mwalimu Nyerere alifariki dunia Oktoba 14, 1999, Alhamisi saa 4:30 asubuhi katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas (St Thomas Hospital) jijini London, Uingereza kutokana na maradhi ya saratani ya damu.

 

Tunamkumbuka Baba wa Taifa kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa katika kupigania uhuru wa nchi yetu na ukombozi wa taifa letu na nchi za Bara la Afrika zilizokuwa zikitawaliwa na wakoloni.

 

Nitaandika matukio muhimu yaliyotokea katika kuelekea kwenye kututoka kwake, nikiegemea zaidi wiki ambazo zilielekea mwisho wa maisha ya Mwalimu Nyerere katika dunia hii na safari yake ya kifo kutoka Butiama hadi London, Uingereza.

 

AGOSTI 22, 1998;

Mwalimu aligundulika ana kansa ya damu, lakini akaendelea na shughuli zake za kutafuta suluhu kwa Taifa la Burundi.

 

AGOSTI 26 NA 27, 1999; Vyombo vya habari Tanzania, kwa mara ya kwanza vilisema wazi kuwa hali ya Mwalimu haikuwa nzuri, hasa baada ya kumuona akitokea Butiama na kuja Dar, lakini wasaidizi wake wakawa na kigugumizi kusema ukweli, kwa kisingizio kuwa wao siyo madaktari.

 

SEPTEMBA MOSI, 1999; Mwalimu, akisindikizwa na mkewe, Mama Maria na daktari wake, Profesa David Mwakyusa, waliondoka nchini kuelekea Uingereza, kuchekiwa afya yake na familia ya Mwalimu wanawaambia waandishi wa habari kuwa angerudi tarehe 28, Septemba, 1999.

 

SEPTEMBA, 22 1999;

Rais Benjamin Mkapa, alitangaza rasmi akizungumza na CNN, kuwa hali ya Mwalimu kule Uingereza siyo nzuri.

 

SEPTEMBA, 24 1999;

Mwalimu anazidiwa akiwa huko London, Uingereza na kukimbizwa Hospitali ya Mtakatifu Thomas ambako analazwa akiwa hoi.

 

SEPTEMBA 25, 1999;

Rais Benjamin Mkapa, anamtembelea Mwalimu huko hospitalini London na kumpelekea salam za pole kutoka kwa Rais Jimmy Carter wa Marekani, siku hiyo usiku, kwa sauti yenye kutetemeka na majonzi, Rais Mkapa, anaitangazia rasmi dunia kuwa Mwalimu anaumwa kansa ya damu.

 

SEPTEMBA, 26, 1999;

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, anapitia London hospitalini kumuona Mwalimu na kumpa salam za pole Rais Mkapa.

 

SEPTEMBA, 27 1999;

Gazeti la Alasiri kwa kutumia vyanzo vyake, linabaini kuwa hali ya Mwalimu ni mbaya mno na anapumulia mashine baada ya kuwekwa kwenye mitambo ya kusaidiwa kupumua.

 

SEPTEMBA 28, 1999;

Mkewe Mama Maria, na wanawe Anna na Rose Nyerere, wanaanza kumuangalia Mwalimu kwa saa 24 huku ikulu yetu ikisema kuwa hali yake inaendelea kuwa nzuri kidogo, huku ikimtuma Waziri wa Tawala za Mikoa, Kingunge Ngombale Mwiru kwenda huko London kusimamia utoaji wa habari za ugonjwa na hali ya Mwalimu kwa ujumla.

 

Siku hiyohiyo, Simba wa Vita, Rashid Kawawa, alilitaka taifa kumuombea Mwalimu apone haraka huku akionesha kusikitishwa sana na hali ya Mwalimu kuzorota sana kwa kasi ya ghafla katika afya yake, akisema “…Tunamuhitaji zaidi Mwalimu kuliko wakati wowote mwingine uliopita….”

 

SEPTEMBA 29, 1999;

Ikulu yatangaza kuwa Mwalimu amepatwa na ugonjwa mwingine ambao ni sawa na ugonjwa wa homa ya manjano, lakini madaktari wake huko London walisema hali yake ni ya kawaida.

 

SEPTEMBA 30, 1999;

Ikulu inasema hali ya Mwalimu inaendelea vizuri na ameanza kukubali matibabu, anageuka mwenyewe kitandani kwa mara ya kwanza tangu alazwe na anaanza kula kidogokidogo kwa kutumia mpira maalum.

 

OKTOBA MOSI, 1999:

Ikulu inatoa kauli mbili tofauti zikisema hali ya Mwalimu, inabadilika kila wakati ila inakuwa mbaya zaidi na kwamba amekosa tena kauli na kuhamishiwa chumba cha wagonjwa mahututi.

 

OKTOBA 2, 1999;

Madaktari wanasema kuwa wanapigana kiume kuyanusuru maisha ya Baba wa Taifa letu.

 

OKTOBA 3, 1999;

Rais Benjamin Mkapa, awataka wananchi kuendelea kumuombea duwa Baba wa Taifa.

 

OKTOBA 5, 1999;

Vyombo vya habari vinasema hali ya Mwalimu ni mbaya kwa sababu inaelekea ubongo wake sasa haufanyi kazi.

 

OKTOBA 11, 1999;

Familia imeitwa na madaktari na kuelezwa hali halisi ya Mwalimu. Mjadala unaendelea kama wazime mashine ya kupumulia au la kutokana na kile kilichoelezwa ‘kufa kwa ubongo’.

 

OKTOBA 14, 1999;

Rais Benjamin Mkapa, atangaza rasmi kifo cha Mwalimu Julius Nyerere kilichotokea katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas huko London, Uingereza. Akatangaza kutuma ujumbe mzito wa viongozi wetu wakiongozwa na Makamu wa Rais, Dk Omari Juma, kwenda huko kuurudisha mwili wa Mwalimu nyumbani. Alizikwa Butiama, Oktoba 21, 1999.

 

Hivyo ndivyo ilivyokuwa, tangu kuugua hadi kufariki kwake dunia.

Mwalimu, Mungu aweke roho yako mahali pema peponi. Amina!

Comments are closed.