Uwoya, Ndikumana Walivyopatanishwa Na Global (Tujikumbushe)
“OYA, acheni mambo yenu, gari liko tayari na dereva anawasubiri nyie tu, tuokoeni muda ili tuweze kufanya majukumu mengine,”
Hii ilikuwa kauli yenye kigugumizi kutoka kwa mmoja wa viongozi tuliowahi kufanya nao kazi ofisini kwetu (kwa sasa hatunaye kikazi), akitusisitiza jambo waandishi na wahariri.
Msisitizo huu ulitokana na safari iliyokuwa imepangwa kwenda Mbezi-Jogoo, nyumbani kwao na muigizaji Irene Uwoya, mwaka 2011.
Lengo la kwenda huko ni moja tu, kufanya mahojiano maalumu na familia nzima, ili kuthibitisha ukweli kuhusu madai yaliyoenea kwamba Uwoya na Ndikumana walikuwa wameachana!
Dakika 50 baadaye, tupo nje ya geti la nyumbani kwao Uwoya tukigonga mlango huku tukisemezana kwa mambo mengi ingawa ilikuwa ni kwa sauti ya chini sana.
“Eeeh, kumekucha tena. Haya karibuni jamani. Hadi wewe umekuja? Kweli leo bwawa limeingiliwa na ruba,”anasema Irene Uwoya baada ya kutufungulia geti na maneno ya mwisho yakimlenga mwandishi wa makala haya.
Katika hali ya kushangaza na ambayo hatukuitarajia, ni uwepo wa Ndikumana nyumbani kwa Uwoya.
Sote tunaingiwa na morali ya kufanya kazi kwa juhudi na kila mmoja wetu anajipanga kwa maswali magumu na yenye kuuchimba ukweli.
Mazungumzo yanaanza, muda mfupi baada ya Uwoya kutuletea vinywaji huku akisindikiza na utani kwa baadhi ya waandishi.
“Kuna wenzangu hapa sitaki niwataje kwa majina, naona kama makoo yanawawasha kwa vinywaji vyetu vile, lakini si mbaya kama kuna mtu anataka kusuuza koo kwa maji ya dhahabu pia yapo tena yamejaa tele,” anasema.
Wakati wote huo, Hamad Ndikumana ‘Kataut’ yuko kimya amejiinamia na mara chache sana anainua kichwa na kuachia kikohozi kikavu.
“Tunataka kujua ukweli juu ya madai ya kuachana kwenu, lakini tumeshangaa kuwakuta mkiwa pamoja tofauti kabisa na jinsi ilivyoenezwa.”
Hili lilikuwa swali kutoka kwa mmoja wa wahariri waandamizi.
“Ndiyo kweli, kulikuwa na ugomvi lakini pia nashukuru tunahangaika kuweka mambo sawa, unajua huyu mwanamke anasumbua sana moyo wangu, nadhani kuna watu wanajaribu kudanganya,”anasema Ndikumana huku akimtazama Uwoya ambaye anaishia kutazama chini na kuwaangalia waandishi.
Baada ya mazungumzo ya muda mrefu huku waandishi tukitumia maneno laini na matamu kuwapatanisha, hatimaye kila mmoja wao anakiri makosa yake dhidi ya mwenzake.
Uwoya anainuka na kumuomba msamaha mumewe, Ndikumana naye anaamka na kumshika mkewe na kwa pamoja wanakumbatiana kwa furaha.
UWOYA AWASHUKURU GLOBAL
Baada ya kupatana kwao, Uwoya anasimama na kusema maneno machache.
“Kwa kweli nawashukuru sana jamani, mmetukuta kwenye ugomvi mkali ndiyo maana tuko huku nyumbani kwetu wazazi wakijaribu kutusuluhisha ingawa hamjawakuta, sikuwa na mpango wa kurudiana na huyu mwanaume lakini kutokana na ushauri wenu nimejikuta moyo ukilainika na sasa natamka wazi nimemsamehe mume wangu kwa makosa yote na yeye anisamehe kwa dhati na tumerudiana rasmi,”anasema. Baada ya hapo Uwoya anamsogelea mumewe na kumbusu shavuni mara kadhaa huku uso wake ukiwa na tabasamu.
NDIKUMANA NAYE
Kwa upande wake, Ndikumana alisema: “Huyu anasema tu ila mkitoka hapa anabadilika tena.”
Haya ndiyo maisha yalivyokuwa kati ya Uwoya na Ndikumana ambaye tayari ametangulia mbele ya haki.
NENO LA MWANDISHI
Siku za kuishi mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke ni fupi sana tena zimejaa tabu. Tusihuzunike mioyoni mwetu kama wasio na imani kwani kila nafsi itaonja mauti.
Zamu ya Hamad Ndikumana imewadia na sasa anawasilisha hesabu zake kwa Mungu. Tuendelee kutenda mema ili siku moja tukutane na Ndikumana, basi na tufarijiane kwa maneno haya.
Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.
Makala: Brighton Masalu | Global Publishers